Polisi wamefanikiwa kumnasa mwanamke anayedaiwa kumtesa kwa kipigo na kumng’ata mtoto Merina Mathayo (15), kumsababishia majeraha makubwa kichwani.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura akizungumza na Mwananchi jana alisema walifanikiwa kumnasa juzi, mwanamke huyo akiwa mafichoni Mbagala wilayani Temeke.
“Tumefanikiwa kumnasa juzi usiku akiwa mafichoni kwa jamaa zake, ni mwanasheria wa kujitegemea ana umri wa miaka 44, lakini inashangaza kwa hayo aliyoyatenda, anaendelea kuhojiwa wiki ijayo tunatarajia kumpandisha kizimbani,” alisema Wambura.
Mtuhumiwa huyo ambaye ni mkazi wa Boko, anadaiwa kumtesa mtoto huyo ambaye ni mtumishi wake wa kazi za nyumbani, ambaye sasa amelazwa katika wodi ya dharura ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa(MOI) Muhimbili Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Uongozi wa MOI umejizatiti kulinda usalama wa mtoto huyo, kwa kuzuia vyakula kutoka nje ya taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti watu kumtembelea na kuzungumza naye.
Mmoja wa wauguzi katika wodi aliyolazwa alieleza mtoto huyo kwa sasa anahudumiwa kila kitu na taasisi hiyo.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Patric Mvungi , alieleza kwamba majibu ya kipimo kikubwa cha CT Scan alichofanyiwa yametoka, ambapo yameonyesha hakuna mfupa uliovunjika kichwani.
Mtoto Merina amelazwa Moi baada ya kupewa rufaa na Hospitali ya Mwananyamala alipokuwa amelazwa awali, kutokana na majeraha hayo ya kung’atwa meno na kupigwa na vitu mbalimbali.
Post a Comment