Naibu
Waziri, Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu
akizungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Habari, Bungeni
alipokutana nao kutoa Tamko kwa niaba ya Waziri kuhusu Siku ya kupambana
na Kuenea kwa hali ya Jangwa na Ukame Dunia leo tarehe 16 Juni, 2014.
Picha na Owen Mwandumbya
……………………………………………………..
TAMKO
LA MHESHIMIWA DKT. BINILITH MAHENGE (MB), WAZIRI WA NCHI, OFISI YA
MAKAMU WA RAIS (MAZINGIRA) LILILOSOMWA NA MHE. UMMY MWALIMU – NAIBU
WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MAZINGIRA) KUHUSU SIKU YA KUPAMBANA NA
KUENEA KWA HALI YA JANGWA NA UKAME DUNIANI TAREHE 16 JUNI 2014
Ndugu Wananchi,
Tangu
mwaka 1994 Baraza la Umoja wa Mataifa liliazimia kuwa kila tarehe 17
Mwezi Juni nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana
na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame, ziadhimishe siku ya Kupambana na
Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame. Tanzania ni mwanachama wa mkataba
huu na hushirki maadhimisho haya kila mwaka. Madhumuni ya maadhimisho
haya ni kuimarisha utekezaji wa mkataba huo kwa kutambua juhudi za nchi
mbalimbali na changamoto zilizopo na kushirikishana katika kuzitafutia
ufumbuzi. Afrika ndilo bara linaloathirika sana na hali ya jangwa na
ukame. Takriban asilimia 73 ya ardhi ya Afrika inakabiliwa na hali ya
ukame na inakadiriwa kuwa kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa
kubadili hali hii, ifikapo mwaka 2030 Afrika itakuwa imepoteza theluthi
tatu za ardhi iliyo bora kwa kilimo na ufugaji.
Ni
kwasababu hii, kesho tarehe 17 Juni, Watanzania tunaungana na wenzetu
kote duniani katika kuadhimisha siku hii. Kauli mbiu ya mwaka huu ni
“Ardhi ni mustakabali wa maisha yetu, tuilinde dhidi ya athari za
mabadiliko ya tabianchi” (‘Land Belongs to the Future, Let’s Climate Proof It’).
Kauli mbiu hii ina lengo la kuhimiza nchi zote duniani kuongeza juhudi
za matumizi endelevu ya ardhi katika juhudi za kuhimili mabadiliko
ya tabianchi ili kufanisha upatikanaji wa chakula. Sekta ya kilimo
sasa inahitaji kulisha watu takriban bilioni tano kote duniani na watu
bilioni tisa ifikapo 2050. Bila mipango madhubuti ya matumizi bora ya
ardhi yanayozingatia mabadilko ya tabianchi itakuwa vigumu kuhakikisha
usalama wa chakula kwa kizazi cha sasa na kijacho hasa kwa nchi za
Afrika.
Ndugu Wananchi,
Pamoja
na kukumbushana juu ya kuweka juhudi zaidi katika matumizi bora ya
ardhi, siku ya kesho tarehe 17 inatukumbusha kuweka juhudi katika kuzuia
uharibifu mwingine unaosababisha kuenea kwa hali ya jangwa na ukame
hususan ukataji wa miti na ufyekaji wa misitu ovyo. Lazima tuongeze
juhudi katika kuongoa na kuhifadhi maeneo ya ardhi kame yaliyoharibika
kwa kufyeka misitu, kilimo cha kuhama hama na ufugaji usio bora. Hata
kama maeneo siyo kame, vitendo vya uharibifu wa mazingira kama hivi
vinaweza kubadili eneo likawa jangwa kama juhudi za kuyaongoa na
kuyatunza hazitafanywa.
Ndugu wananchi,
Tatizo
la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame ni kubwa pia hapa nchini.
Inakadiriwa kuwa kiasi cha asilimia 45 hadi 75 ya nchi yetu ni eneo kame
na linakabiliwa na tatizo hili la kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.
Maeneo ya katikati ya nchi ikiwa ni pamoja na mikoa ya Dodoma na
Singida; na baadhi ya sehemu katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu,
Mara, Iringa, Manyara na Arusha na baadhi ya maaeneo ya Mkoa wa
Kilimanjaro kama vile Same ndiyo yameathirika kwa kiwango kikubwa. Ni
maeneo haya ambayo pia yana upungufu mkubwa wa misitu.
Hali
hii inasababisha madhara makubwa yatokanayo na uharibifu wa ardhi ikiwa
ni pamoja na kupungua kwa uwezo wa ardhi kuzalisha mazao bora; na
upungufu wa malisho bora ambao pia umepunguza uzalishaji kwa upande wa
mifugo. Aidha ukataji wa misitu umesababisha kupungua kwa mvua katika
baadhi ya maeneo haya na hivyo kusababisha kuongezeka kwa hali ya
ukame. Wote tumeshuhudia maeneo haya yakikumbwa na uhaba wa chakula wa
mara kwa mara na moja ya sababu kubwa ni kuenea kwa hali ya jangwa na
ukame; pamoja na kutambua ukweli kuwa kwa kiasi kikubwa hali hii
imesababshwa na mabadilko ya tabianchi.
Ndugu Wananchi,
Serikali
inachukua hatua mbalimbali kuepuka changamoto hizi. Tayari Ofisi ya
Makamu wa Rais imeweka Mpango wa Taifa wa Kupambana na Kuenea kwa Hali
ya Jangwa na Ukame (NAP) ambao umeweka nyenzo muhimu ya kuongeza
uzalishaji katika kilimo; kuondokana na tatizo la uhaba wa chakula;
kuongoa maeneo yaliyoharibika na kurejesha misitu katika maeneo ya
nyanda kame; na kupunguza umasikini kupitia usimamizi endelevu wa ardhi.
Aidha mwaka 2006, Ofisi ya makamu wa Rais pia iliweka Mkakati wa kuzuia
uharibifu wa ardhi na vyanzo vya maji ili kuhakikisha tatizo la kuenea
kwa hali ya jangwa na ukame linakuwa shirikishi kuanzia Serikali za
Mitaa hadi Serikali Kuu. Mkakati huu umesaidia sana kuhifadhi maeneo
ambayo yalikuwa yanaelekea kugeuka kuwa jangwa kutokana na kilimo
kisicho endelevu, ufugaji holela na ufyekaji misitu ovyo. Mkakati huu
umekuwa muhimu sana hasa kwa kushirikisha wananchi na taasisi mbalimbali
katika tuzo ya Rais ya upandaji na utunzaji miti kama hatua muhimu
katika hifadhi na matumizi bora ya ardhi.
Mwaka
2012 Serikali ilipitisha pia Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na
mabadilko ya tabianchi ambao pia kwa kiasi kikubwa umesadia kukabiliana
na changamoto za kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.
Ndugu Wananchi,
Kwa
kumalizia naomba nitoe wito tena kwa kusisitiza kauli mbiu ya mwaka
huu kuwa “Ardhi ni mustakabali wa maisha, tuilinde dhidi ya
uharibifu”. Kila mmoja wetu kwa nafasi yake kesho afanye kitendo ambacho
kwa namna moja au nyingine kitasaidia katika utunzaji na matumizi
endelevu ya ardhi. Inawezekana kuzuia kuendelea kwa mmomonyoko wa ardhi
kwa kutumia njia mbalimbali za kuhifadhi ardhi; kupanda miti ili
kurejesha misitu pale ambapo imetoweka ili kuwezesha ardhi kuwa na
rutuba ya kuweza kuzalisha zaidi katika maeneo kame na yasiyokuwa na
rutuba.
Ofisi
ya Makamu wa Rais itaendelea kuzihimiza Serikali za Vijiji na
Halmashauri kutunga na kusimamia sheria ndogondogo za Hifadhi ya Ardhi
na Misitu.
Napenda
kuchukua fursa hii kuviomba vyombo vya habari kuendelea kuhamasisha na
kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuchukua hatua muafaka za kupambana
na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kwa kufanya shughuli mbali mbali
zinazochangia kutatua tatizo hili. Aidha, napenda kuchukua fursa hii
kuhimiza, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi kuongeza
uwekezaji katika hifadhi ya misitu na matumizi endelevu ya ardhi ili
kuhakikisha kwamba kunakuwepo na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Ofisi
ya Makamu wa Rais kama msimamizi wa suala hili itahakikisha inazidi
kuweka mazingira bora ya ushirkishwaji ili kuhakikisha juhudi hizi
zinakuwa zetu wote kwa ajili ya kizazi hiki na kizazi kijacho katika
mazingira yanayokabiliwa na mabadilko ya tabianchi.
Asanteni kwa kunisikiliza.
DKT. BINILITH S. MAHENGE (MB.)
WAZIRI WA NCHI,
OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MAZINGIRA
Post a Comment