WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe akiondoka uwanjani hapo mara baada ya kuzindua ligi hiyo
WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison
Mwakyembe,amezindua rasmi ligi ya mpira wa miguu itakayowashirikisha madereva
wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda inayojulikana na Cocacola bodaboda cup
2014.
Uzinduzi huo ulifanyika jana jumamosi
katika viwanja vya Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe iliyopo Ilomba jijini Mbeya
ambapo zvikundi kumi vya madereva wa bodaboda vitashiriki ligi hiyo.
Akizindua ligi hiyo Mwakyembe amewataka
madereva wa bodaboda kuendesha pikipiki zao kwa uangalifu na kuacha ulevi ili
kupunguza ajali zisizokuwa za lazima.
Alisema waendesha boda boda wanapaswa
kutumia mashindano kama njia ya kujikumbusha juu ya masuala muhimu ya usalama
barabarani kwa kuepuka ulevu watumiapo vyombo hivyo huku akipongeza wadau wa
michezo mkoani hapa kwa kuleta mapinduzi katika michezo nchini.
Alisema uwepo wa mikakati madhubuti
baina ya wadau wa michezo mkoani Mbeya umewezesha kuibuka upya kwa
amani,mshikamano na upendo baina ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya na kusababisha
mshikamano wa hali ya juu tofauti na miaka kadhaa iliyopita.
Dk Mwakyembe pia aliwataka waratibu wa
mashindano hayo kampuni ya City Sign Promotion and Marketing Agency kuwaalika
wabunge wote wa Mkoa wa Mbeya siku ya mchezo wa fainali ili kwa pamoja waweze
kujionea namna michezo ilivyowezesha watu wa makundi yote kukutana na
kuzungumza mambo ya msingi wakiweka tofauti zao pembeni.
Awali mmoja wa Wakurugenzi wa City sign
Promotion, Geofrey Mwangunguru alisema timu zinazoshiriki michuano hiyo
zimegawanywa katika makundi mawili ya A na B ambapo kila kundi lina jumla ya
timu tano na kila kundi litatoa timu mbili zitakazoingia hatua ya nusu fainali
na baadaye kupatikana bingwa wa michuano.
Aidha Mwangunguru alisema dhamira ya
kuanzisha ligi hiyo ni kutambua mchango wa sekta hiyo katika usafirishaji
pamoja na kuwaunganisha na jamii ambayo imekuwa ikiamini kuwa kundi hilo
halipaswi kuweko katika jamii.
Aliongeza kuwa kabla ya kuanzisha kwa
ligi hiyo kampuni yake ilijiwekea vipaumbele vitatu ambavyo ni kuhakikisha
umoja wa bodaboda unaanzisha saccoss, kujiunga na taasisi za Pensheni pamoja na
kutafuta bima za afya kwa ajili ya maisha yao kutokana na ajali za mara kwa
mara.
Kwa mujibu wa Mwangunguru katika kundi A
zipo timu za waendesha bodaboba za Mbalizi standi Umalila,Iyunga,Shewe
Sae,Kadege na Uyole wakati kundi B zipo timu za Mbalizi standi
Chunya,Ilomba,Soweto,Kabwe na Mafiati.
Mwangungulu alisema bingwa wa mashindano
hayo yatakayoendeshwa kwa muda wa siku 31 anatarajiwa kuzawadiwa pikipiki aina
ya Boxer yenye thamani ya shilingi milioni 2.5,mshindi wa pili shilingi laki
saba,mshindi wa tatu shilingi laki tatu na mfungaji bora shilingi laki moja.
Naye Katibu wa Umoja wa waendesha boda
boda Mbeya, Msenda Mdesa, akisoma Risala mbele ya Mgeni rasmi ambaye alikuwa ni
Waziri wa Uchukuzi Dk. Harison Mwakyembe, alisema umoja huo umefanikiwa
kuwaunganisha madereva wa bodaboda Mkoa mzima.
Aliongeza kuwa kutokana na umoja huo
wamefanikiwa kuanzisha benki yenye wanachama 312 iliyosajiliwa kwa mujibu wa
sheria za uanzishwaji wa benki na kupewa Baraka zote na Benki kuu ya Tanzania.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
Post a Comment