Makamu
Mkuu wa Chuo cha International Medical and Technological University
(IMTU), Profesa PV Prabhak Rao (mwenye koti la blue) na viongozi wengine
wakisindikizwa na polisi kuingia kwenye Kituo cha Oysterbay, Dar es
Salaam jana, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na upatikanaji wa viungo
vya binadamu eneo la Mpigi Bunju.
Wakati
ikibainika kuwa viungo vya miili ya binadamu vilivyookotwa juzi katika
Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika
Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la
Polisi liliwatia nguvuni watumishi wanane wa chuo hicho kuhusiana na
sakata hilo. Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa na Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa ni baada ya
uchunguzi wa awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya mwisho vilikuwa
katika maabara ya IMTU.Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni eneo la
Bonde la Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85 yenye
mabaki ya viungo vya binadamu.Kutokana
na tukio hilo, Polisi imeunda jopo la wapelelezi saba likiongozwa na
Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Jafari Mohamed kusaidiana na daktari wa
jeshi hilo kufanya uchunguzi wa miili hiyo.“Katika
uchunguzi wetu tulibaini kuwa hivyo viungo vya binadamu vilitolewa
katika Chuo cha IMTU na kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa
ajili ya kutupwa eneo la Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova.Alisema
mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa na viungo vya aina mbalimbali vikiwamo
vichwa, miguu, mikono, moyo, mapafu, vifua na mifupa ya aina
mbalimbali. “Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema. Alisema
katika eneo hilo walikuta vifaa vinavyotumika hospitali kama glovu,
nguo maalumu (apron) 20 na karatasi mbili zenye maswali ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema
jeshi hilo limefungua jalada la uchunguzi ili kujua sheria gani
imevunjwa na kwa nini viungo hivyo vilitupwa hapo na kwa nini wasitumie
utaratibu mzuri wa kuhifadhi na kwamba endapo kuna makosa ya kisheria,
hatua zitachukuliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Muhimbili wapokea mabaki
Meneja
Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema jana kuwa hospitali hiyo
imepokea vifurushi 40 vyenye mabaki ya miili ya binadamu na kuhifadhiwa
wakisubiri maelekezo ya polisi... “Hili ni suala la polisi, ninachoweza
kusema ni kweli tumepokea vifurushi hivyo jana (juzi) usiku.”
IMTU yakiri kuhusika
Wakati
Kova akisema hayo, uongozi wa IMTU ulikiri kuhusika na mabaki ya miili
hiyo yaliyotupwa katika mto huo usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita.
Naibu
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Dk Fariji Mtango alisema jana kwamba
anaamini miili hiyo inaweza kuwa ni ile iliyotoka katika chuo hicho,
ambayo imekuwa ikifanyiwa mazoezi na wanafunzi kwa kuwa walihitaji
kuiteketeza na walishatoa agizo hilo.
Alisema
walitoa agizo kwamba mabaki hayo yapelekwe Muhimbili kwa mujibu wa
utaratibu wao kwa kuwa hayakuwa na matumizi tena, kwa kuwa ndiyo sehemu
yenye uwezo wa kuyateketeza na kutoa jukumu hilo kwa mmoja wa wakufunzi
wa chuo hicho ambaye jana alikuwa safarini.
“Sasa
zaidi hatujui kilichoendelea lakini tulipoangalia jana (Jumatatu)
tulikuta sehemu yalipohifadhiwa imesafishwa, hivyo inawezekana ni sehemu
ya vile vilivyoondolewa hapa. Hatukutarajia kwamba vingetupwa katika
eneo lisilokuwa sahihi kama ilivyofanyika,” alisema.
Dk
Mtango alisema hiyo ilikuwa moja ya hatua za kupisha wakaguzi ambao
walitarajiwa kukuta maeneo yote ya kufundishia yakiwa katika hali ya
usafi na unadhifu.
“Hawa
wakaguzi wanapokuja wanatakiwa waone vitu vyote vikiwa sawa. Hata kama
wangeona hayo mabaki ya miili ya binadamu isingekuwa tatizo, bahati
nzuri wamekuja jana na wamefanya kazi yao vizuri,” alisema.
Muda
mfupi baada ya kutolewa kauli hiyo, viongozi tisa wa chuo hicho na
walinzi wawili walikamatwa mnamo saa 7.30 mchana na kupelekwa katika
Kituo cha Polisi Oysterbay ambako wanashikiliwa, lakini baadaye Kova
alisema waliokamatwa ni wanane.
Jana
mchana eneo la chuo cha IMTU lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi
waliotanda kuanzia getini, mapokezi na kwenye bustani za chuo hicho na
wengine waliovalia sare maarufu kama ‘tigo’ ambao walikuwa wakishika
doria mbele ya chuo hicho.
Hatua kuchukuliwa
Dk
Mtango alisema uongozi wa chuo hicho umeshtushwa na kutupwa kwa mabaki
hayo katika utaratibu usiokubalika na utafanya uchunguzi na kuchukua
hatua kwa wote waliohusika.
“Tunaanza
na huyu ambaye tulimpa hili jukumu. Yeye ndiye aliyetakiwa kusimamia na
anaujua wazi utaratibu wetu. Kwa sasa hajafika hapa na hata simu yake
haipatikani. Tunaarifiwa kwamba amekwenda Zanzibar,” alisema.
Jinsi ilivyotokea
Juzi
jioni, ilitokea taharuki baada ya wananchi kubaini viungo hivyo na
taarifa kuanza kusambaa katika mitandao ya kijamii na baadaye vyombo vya
habari na hadi jana mjadala kuhusu suala hilo ulikuwa mzito na wananchi
wakihoji miili hiyo ni ya watu gani, imetoka wapi na imetupwa na watu
gani.
Shuhuda
wa tukio hilo, Mariam Nkumba alisema mara ya kwanza aliona mifuko yenye
viungo hivyo Jumapili alipokwenda kuponda kokoto katika eneo hilo
lakini hakubaini kulikuwa na nini.
Siku
hiyo, Nkumba alisema aliondoka katika eneo hilo saa 12 jioni bila kujua
nini kilikuwa ndani ya mifuko hiyo na siku iliyofuata (Jumatatu),
alikwenda kuchukua mfuko mmoja ili ahifadhie kokoto zake, ndipo
aliposhtuka kuona viungo vya binadamu.
“Mifuko
ilikuwa mingi kweli, yote ilikuwa imejaa viungo vya binadamu. Mpaka
sasa sijala na sina hamu ya kula. Ukiiona ile miili huwezi kula
chakula,” alisema.
Mfanyakazi
wa Kampuni ya Ujenzi ya Skol iliyopo karibu na eneo hilo, Supery
Kaijunga alisema mara alipopata taarifa kutoka kwa Nkumba alianza kutoa
taarifa kwa wananchi wengine ili kwa pamoja wajue la kufanya.
Baadaye walitoa taarifa polisi ambao walifika saa mbili usiku na kukusanya mabaki yote na kuondoka nayo.
Hata hivyo, Kaijunga alieleza wasiwasi wake kuhusu wingi wa miili hiyo na kuhoji walikuwa watu gani na walitoka maeneo gani.
“Tukio
hili siyo la kawaida na halijawahi kutokea huku kwetu. Tunakuwa na
wasiwasi sana labda nasi maisha yetu yatachukuliwa kama hawa; polisi
wafanye uchunguzi wa kina kubaini ukweli wake,” alisema
Kaijunga.MWANANCHI
Post a Comment