Washtakiwa
watatu wanaokabiliwa na mashtaka ya mauaji dhidi ya mtoto Nasra Rashid
Mvungi, wamelazimika kubadilishiwa hakimu baada ya hakimu wa awali,
kupata dharura na kutokuwepo mahakamanani hapo.
Washtakiwa hao ambao kesi yao imekuwa
ikifikishwa na kutajwa, mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya
hakimu mkazi mkoa wa Morogoro, Mary Moyo, walilazimika kupandishwa
kizimbani mbele ya hakimu Agripina Kimanze na kusomewa mashtaka yao,
baada ya hakimu moyo kutokuwepo mahakamani, ambapo tofauti na nyakati
zingine, shauri hilo lilichelewa kuanza.
Mwendesha mashtaka wa polisi Aminatha
Mazengo, akisoma shitaka, aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa shauri
hilo bado haujakamilika na kwamba jalada bado lipo kwa mwanasheria mkuu
wa serikali, hivyo kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa
kwa kesi hiyo.
Mahakama iliridhia ombi hilo, na
kupanga Agosti 20 mwaka huu, kufikishwa tena kwa kesi hiyo kwaajili ya
kutajwa, kutokana na mahakama hiyo kukosa uwezo kisheria kusikiliza
shitaka la mauaji na washtakiwa kurudishwa rumande kutokana na kesi hiyo
kutokuwa na dhamana.
Kesi hiyo ya mauaji inawakabili
washitakiwa watatu akiwemo baba mzazi wa mtoto Nasra, bw. Rashid Mvungi
pamoja na waliokuwa walezi wake, Bi Mariam Said na mumewe Mtonga Omary,
ambao awali walikuwa wakikabiliwa na shitaka la kula njama na kufanya
vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto Nasrah Mvungi kabla ya baadaye
mashitaka yao kubadilishwa na kuwa ya mauaji baada ya mtoto huyo
kufariki dunia.
Post a Comment