Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii na Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa
mwezi Julai 2014 kwa waandishi wa habari jijini Dar es salaam.
Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imeeleza kuwa ongezeko dogo la mfumuko wa bei nchini
kutoka asilimia 6.4 za mwezi June hadi asilimia 6.5 za mwezi Julai 2014
linatokana na kupanda kwa bei za baadhi ya bidhaa na huduma katika
maeneo mbalimbali.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Takwimu
za Jamii na sensa ya Watu na Makazi Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa
bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo Bia, Sigara, mavazi kwa wanaume na
yale ya watoto zimechangia ongezeko hilo.
Aidha,
huduma na bidhaa nyingine zilizochangia ongezeko hilo ni gharama za
udobi, kodi za pango, mazulia na mkaa wa kupikia Bw. Kwesigabo
amefafanua kuwa hali ya mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na migahawa
kwa mwezi Julai umepungua hadi 7.9 kutoka asilimia 8.5 kutoka asilimia
8.7 za mwezi Juni huku badiliko la fahirisi za bidhaa zisizo za vyakula
likiongezeka hadi asilimia 4.9 kwa mwezi Julai 2014 kutoka asilimia 4.8
iliyokuwepo mwezi uliopita.
Kuhusu
mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi amesema kuwa umeongezeka
kwa asilimia 0.1 ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.6 kama
ilivyokuwa kwa mwezi Juni mwaka huu, huku fahirisi za bei za taifa
zikiongezeka hadi kufikia 149.16 kutoka 148.98 za mwezi Juni 2014.
Kwa
upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma za jamii kutoka mwezi Septemba 2010 hadi Julai 2014 umefikia
shilingi 67 na senti 04 kutoka shilingi 67 na senti 12 za mwezi Juni
mwaka huu.
“Kuongezeka
kwa bei ya baadhi ya bidhaa na huduma kwa mwezi uliopita kunamaanisha
kwamba, uwezo wa fedha yetu katika kununua huduma na bidhaa hizo
unaupungua hii inamaanisha mfumuko wa bei unapopanda thamani ya shilingi
nayo inashuka” Amebainisha.
Kuhusu
ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa mfumuko
wa bei nchini Kenya umeongezeka na kufikia asilimia 7.67 kwa mwezi Julai
2014 ikilinganishwa na asilimia 7.39 za mwezi Juni huku Uganda ikiwa na
mfumuko wa bei wa asilimia 4.3 mwezi huu ikilinganishwa na asilimia 5.0
za mwezi Juni.
Post a Comment