TIMBWILI! Jamaa
mmoja na mkewe ambao wote hawakujulikana majina mara moja wamezua
varangati la aina yake mahakamani kisa kikiwa ni kufutiwa kesi na
kushindwa kuheshimu amri za maafande.Tukio hilo la aina yake
lililoshuhudiwa na mwanahabari wetu lilijiri kwenye Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu jijini Dar baada ya mume huyo kufutiwa kesi iliyokuwa
ikimkabili ya unyayasaji wa watoto wake wa kuwazaa.
Jamaa
huyo na mkewe walizua timbwili hilo wakati mtuhumiwa huyo akitolewa
chumba cha mahakama kwenda kuweka sawa nyaraka ili awe huru.
Huku
akiwa na hasira, mwanaume huyo alianza kuzozana na polisi huku akiungwa
mkono na mkewe wakikataa kutii amri ya askari aliyekuwa akiwaelekeza
kwenda chumba kingine ili kukamilisha taratibu za kuwa huru.
Akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Wawili
hao walisikika wakitoa maneno makali kuwa wasisukumwe kwani hakimu
alikuwa ameshamwachia mwanaume huyo huru, jambo ambalo liliwakera askari
na kuwaambia kuwa wanatakiwa kutii sheria na taratibu za mahakama.
Katika
sekeseke hilo huku askari wakilazimika kutumia nguvu, jamaa huyo
alifanya mgomo baridi akipiga kelele na kufoka hivyo kusababisha watu
kushangaa.
Hata
hivyo, polisi hao walitumia mbinu ya kuwadhibiti kistaarabu ili
kuhakikisha amani inakuwepo mahakamani hapo hivyo mambo yakawa shwari.
Mwanamke huyo akidhibitiwa.
Habari
ndani ya mahakama hiyo zilidai kwamba jamaa huyo alikuwa akikabiliwa na
tuhuma hiyo ya unyanyasaji wa watoto wake ambao alizaa na mwanamke
mwingine. Madai yalishushwa kwamba mwanaume huyo alikuwa akishirikiana
na mkewe huyo mpya kuwafanyia manyanyaso kwa watoto wake hali ambayo
iliyosababisha shirika moja la kutetea haki za binadamu kumchukulia
hatua ikiwa ni pamoja na kumfikisha mahakamani hapo.
Ilisemekana
kwamba jamaa huyo alionywa na kupewa maelekezo kuwa kama ikiwezekana
watoto hao watafutiwe sehemu nyingine ya kuishi ikiwa ni pamoja na
kupata mahitaji muhimu, jambo ambalo mwanaume huyo alilitekeleza na
kumaliza ishu hiyo.
Post a Comment