Dar
es Salaam, Shahidi wa pili katika kesi ya kujipatia Sh29.6 milioni kwa
njia ya udanganyifu inayomkabili mganga wa jadi, Dunia Salumu (37)
‘Manyaunyau’ amedai kuwa walilazimika kuuza kiwanja na nyumba ya urithi
kutafuta fedha za kununua mabeberu saba na mafuta ya ngamia ili kumpa
mganga huyo kama masharti ya kumfufua ndugu yao aliyefariki dunia.
Manyaunyau
alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala,
Desemba mwaka 2013 akikabiliwa na shtaka la kujipatia fedha hizo kutoka
kwa Tecla Modest.
Akiongozwa
na Mwendesha Mashtaka, Nassoro Katuda shahidi huyo, Diana Steven (26)
alidai kuwa baada ya kumaliza matanga ya mjomba wake, Saimon Modest
aliyefariki mwaka 2008, wakiwa nyumbani Mchikichini, Dar es Salaam
walisikia sauti ya mtu ikisema kuwa ‘mimi sijafa’.
Wakati
Diana akiendelea kutoa ushahidi huo mrefu, Hakimu Wilberforce Luhwago,
alimkatisha akieleza kuwa ameisikiliza kesi hiyo kwa muda mrefu na kuna
nyingine za kusikiliza, hivyo itaendelea Agosti 13, mwaka huu.
Ushahidi wenyewe
Alisema
siku tatu baada ya mazishi ya mjomba wake, ndugu yao aitwaye Hamisi
akiwa na Manyaunyau walifika nyumbani kutoa pole na walipofika
Manyaunyau alidai kuwa marehemu hajafa, bali ameuawa na kaka yake na
amechukuliwa na Mpemba kwa ajili ya kwenda kuuza duka.
“Mimi na
mama zangu wawili tulishtushwa na kuhoji, mtu aliyekufa anaweza akawa
hai?” alisema Diana katika ushahidi wake uliochukua saa nane.
“Baada ya
hapo alituambia siku iliyofuata twende ofisini kwake (Manyaunyau),
Mburahati, tukiwa na Sh100,000. Mama zangu walisema hawana, lakini ndugu
yetu mmoja aitwaye Bright Steven alikwenda kwenye ATM na kuchukua
Sh80,000 na safari ikafanikiwa,” alidai.
Diana
alisema baada ya kupeleka fedha hizo, Manyaunyau aliwapangia kwenda siku
nyingine, akiwataka kurudi wakiwa na kitambaa cheusi na walipokipeleka
alisema alikichukua na kukifunika kikaanza kutoa sauti ya mtu mzima
ikisema: “Karibuni sana wajukuu zangu na maelezo yote mtapewa na
mwenyeji wenu.”
Alisema
Manyaunyau pia aliwataka wapeleke chupa sita za mafuta ya ngamia
wakiyakosa wampelekee Sh1.8 milioni. Alisema walimpelekea fedha hizo
walizozipata kwa kuuza sehemu ya kiwanja walichorithi kwa mama yao.
“Siku
tuliyopeleka hiyo hela pia tulipeleka mtama, jogoo mwekundu na
tulipelekwa katika pori lililopo Kibamba na kila tulipokuwa tukienda
kule Kibamba tulikuwa tunakodi teksi kwa Sh40,000,” alidai Diana.
Alidai
kuwa kabla ya kufika katika pori hilo, Manyaunyau aliwaagizia soda
wakanywa na baada ya kumaliza aliwaambia wapige makofi huku wakisema
hodi hodi mkubwa!
“Tuliingia
katika pori hilo saa 2: 00 usiku, tukaona mwanga kama radi imepiga na
tukaona kitu cheupe kama mtu kafunikwa sanda... ile tuliyoipeleka kwa
Manyaunyau siku chache kabla ya kwenda katika pori hilo.
“Alituambia
mtu wenu ndiyo huyo ila msimfunue kwa sababu ni mchafu, akasema
inatakiwa hela ya kununua mafungu mawili ya dawa ya kumsafishia.
Sisi
hatukuelewa, ndipo alipotuambia siku iliyofuata twende ofisini kwake
atufafanulie. Tulipofika alituambia anataka mbuzi saba madume na Sh2
milioni na kwenda naye tena Kibamba.
“Tukiwa
porini hapo tulisikia sauti ya babu ikisema marehemu wenu ameshikiliwa
na wachawi, wanataka damu ya mbuzi saba, hivyo tulirudi nyumbani na
kwenda kuuza tena kiwanja kilekile kwa mtu mwingine na kupata Sh4.9
milioni na kuzipeleka kwa Manyaunyau kununulia mbuzi hao,” shahidi
alidai na kuongeza kuwa ‘babu’ alizidi kuongeza madai, mara hii akisema
anataka nguo, mkeka na chakula nyumbani kwa Manyaunyau.
“Baada ya
kauli ya babu, tulipeleka chakula kwa Manyaunyau na hapo alituambia
tujiandae kwa safari ya Majohe na huko tulikwenda mimi na mama zangu
wawili na mke wa Manyaunyau na tulipofika tuliongea tena na ‘babu’ na
kutuambia tutafute Sh2 milioni nyingine kwa ajili ya kumkomboa ndugu
yetu.”
Waliporudi
kutoka Majohe, alidai kuwa walikwenda kukopa kwa riba na Manyaunyau
alisema fedha hizo wazifunge katika kitambaa cheusi na kuziweka katika
ndoo na kuzipeleka katika Msitu wa Majohe.
“Tulipofika
Majohe tulipiga makofi na kuziweka zile pesa na siku iliyofuata
Manyaunyau alituambia tutoe Sh3.5 milioni kwa ajili ya kukanyagia na
sisi tulizipelekea hukohuko Majohe.”
Alidai
kuwa siku iliyofuata walikwenda ofisini kwa Manyaunyau na kuambiwa kuwa
wapeleke chakula nyumbani kwake baada ya hapo waende kumwangalia mchawi
aliyemchukua ndugu yao huko Kibamba eneo la makaburi.
“Tulipofika
eneo hilo la makaburi alitokea mtu mrefu sana akiwa ameshikilia mkia na
akapiga magoti na hapo hapo alitokea tena mtu mnene na kusema hamuwezi
kumuona ndugu yenu kwa sasa.”
Diana alidai kuwa baada ya kuambiwa hivyo, ilisikika sauti ya ‘babu’ ikisema watafute Sh5 milioni nyingine.
“Tulivyosikia
hiyo sauti ya ‘babu’ akisema tutafute ndugu zangu walisema hawana hiyo
hela na sauti ya babu iliendelea kusema kuwa nyie leteni tu hiyo hela
marehemu akija atailipa,” alieleza.
-www.udakuspecially.com
Post a Comment