TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Siku
ya Vijana Duniani itafanyika tarehe 12 Agosti, 2014 ikiwa na lengo la
kuyafanya masuala mbalimbali ya vijana kutambulika katika jamii ya
Kimataifa. Mwaka huu, ujumbe ni “Vijana na Afya Kiakili”. Tarehe
hii iliamuliwa kuwa Siku ya Vijana Duniani na Umoja wa Mataifa mwaka
1999. Hii ni Siku maalum inayodhihirisha kutambua kazi muhimu
zinazofanywa na vijana na umuhimu wake katika jamii pamoja na kuwapa
fursa kwa ajili ya kuongeza ufahamu juu ya changamoto na matatizo
yanayoukabili ulimwengu wa vijana.Mijadala
katika maeneo maalum pamoja na taarifa juu ya kampeni mbalimbali
zitafanyika katika maeneo na nchi mbalimbali ulimwenguni kwa ajili ya
kutoa hamasa kwa nchi wanachama pamoja na jamii ili kuelewa mahitaji ya
vijana, utekelzaji wa sera mbalimbali katika kusaidia kupambana na
changamoto zilizopo, pamoja na kuwasaidia vijana kushiriki katika
michakato ya utoaji wa maamuzi.
Siku
ya Vijana Duniani ni kutambua na kuthamini kuwa kipindi cha ujana
kinaambatana na mabadiliko makubwa na ya haraka na safari ya kutoka
utotoni kufikia utu uzima inaweza kuwa ngumu na yenye changamoto nyingi
na hivyo kuhitaji utulivu na ukomavu wa akili. Kwa Tanzania kijana ni
mtu yeyote mwenye umri kati ya miaka 15 hadi 35.
Katika
Siku hii na siku za mbeleni itakuwa fursa ya kuweza kutoa ufahamu juu
vikwazo mbalimbali vinavyowakabili vijana ikiwemo kunyanyapaliwa na
kubaguliwa, lakini pia kuwapa vijana nguvu ili waweze kutimiza malengo
yao.
Tanzania
kama sehemu ya duania inatambua na kuthamini changamoto maalum
zinazowakabili vijana walioko katika mazingira hatarishi pamoja na
umuhimu wa kuhakikisha kuwa wanahusishwa kikamilifu katika malengo ya
maendeleo katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Tanzania
itaendelea kufanya kazi kwa karibu na vijana pamoja na wadau wa
maendeleo ili kuunga mkono programu za elimu ya afya kwa vijana walioko
ndani na nje ya shule, walioko katika taasisi za mafunzo rasmi na zisizo
rasmi ili kukuza uwezo wa taarifa na mawasiliano ya kisasa.
Katika
ngazi ya kitaifa Tanzania imedhamiria kukuza na kuboresha misingi ya
kuwashirikisha vijana katika maeneo ya sera mbalimbali, programu ya
mikakati ya maendeleo ya vijana ambapo lengo ni kuhakikisha kuwa sauti
zao zinasikika na kufanyiwa kazi.
Katika
kutekeleza eneo hili Tanzania inalenga kuweka fursa zitakazowawezesha
vijana kukuza utaalamu na ujuzi utakaowawezesha kufanikiwa katika
kipindi cha mpito kutoka ujana kwenda katika utu uzima kwa kuzingatia
hali halisi ya mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea duniani.
Kwa
kutambua umuhimu huu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
inatumia fursa hii kuwakaribisha vjana pamoja na wadau mbalimbali katika
Maonyesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa ya mwaka huu ambayo yatafanyika
Mkoani Tabora kuanzia tarehe 08 – 14 Oktoba ikiwa ni mwedelezo wa kuwapa
vijana na wadau taarifa mbalimbali kuhusiana na maendeleo kwa ujumla
wake.
Tukiwa
tunasherehekea Siku ya Vijana Duniani Wajibu wetu mkubwa ni kuona kuwa
vijana wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii
katika jamii wanazoishi.
Katika
Siku hii Vijana wote wanakaribishwa kuandaa hadithi mbalimbali fupi
zenye mafunzo, mashairi, picha mbalimbali, video na kazi za sanaa ili
kazi itakayoonekana inafaa iweze kuwa miongoni mwa kazi
zitakazojumuishwa katika Chapisho la Umoja wa Mataifa ‘Kuwajumuisha
Vijana Kijamii kwa kuzingatia Afya Kiakili’.
Imetolewa na wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
Post a Comment