Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameupa wiki moja uongozi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro, kuwapatia viwanja vya kujenga nyumba wahanga
wa mafuriko ya kiasi cha miaka minne iliyopita mjini Kilosa.
Rais Kikwete ametoa
agizo hilo leo, Jumapili, Agosti 24, 2014 wakati alipozungumza na wananchi wa
Kilosa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kilosa baada ya kutembelea
Wilaya hiyo kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo.
Rais Kikwete amerejea
Mkoani Morogoro asubuhi ya leo kuendelea na ziara yake ya siku saba mkoani huo
baada ya kuikatisha jana, Jumamosi, Agosti 23, 2014, kwenda kwenye Chuo cha
Uongozi wa Kijeshi, Monduli, Mkoani Arusha, ambako alikwenda kutoa kamisheni
kwa maofisa wapya wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (TPDF).
Baada ya kuwa
amelalamikiwa kwa maneno na kwa mabango na wahanga hao kuwa hawajapatiwa
viwanja vya kujenga nyumba za kudumu baada ya kuwa wameahidiwa viwanja hivyo na
Rais Kikwete mwenyewe wakati alipowatembelea kufuatia mafuriko ya Mto Mkondoa
miaka minne iliyopita, Rais Kikwete amesema:
“Ni jambo la kusikitisha kuwa bado ahadi zangu
kwenu hazijatimizwa. Niliahidi mambo mawili wakati nilipokuja kuwaoneni – moja
niliahidi kuwa tutawapatia viwanja vya kuweza kujenga nyumba za kudumu na pili
niliwaahidi kuwasaidia kujenga nyumba. Sasa tuanze na la kwanza,”alisema Rais Halmashauri hiyo kujieleza mbele ya wananchi hao
kuhusu ahadi hizo.
Baada ya kuambiwa kuwa
vimepimwa viwanja 800 katika Halmashauri hiyo, Rais Kikwete aliamuru kuwa kiasi
cha viwanja 400 vitengwe kwa ajili ya wahanga hao wa mafuriko.
“Katika muda wa wiki moja, yaani kuanzia kesho
Jumatatu hadi kufikia Ijumaa, nataka taratibu zote kuwa zimekamilika na kila
mtu kuwa ameonyeshwa kiwanja chake. Tutazingumzia habari ya ujenzi baadaye,” alisema Rais Kikwete.
Mapema asubuhi, Rais
Kikwete ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme katika eneo la
Msolwa, Wilaya ya Kilosa, mradi ambao unajengwa na Shirika la Watawa wa Madonda
Matakatifu ya Yesu la Stigmatine Fathers
and Brothers la Kanisa Katoliki
ambalo lilianza shughuli zake katika Wilaya ya Kilosa Novemba 1989.
Mradi huo wa Yovi Mini
Hydropower Project unajengwa kwenye
milima na maporomoko ya Mto Yovi na unalenga kuzalisha megawati kati ya moja na
2.3 kwa ajili ya mamia kwa mamia ya watumiaji katika eneo hilo ikiwamo shule
maarufu na ya mfano ya sekondari ya Msolwa St. Gaspar iliyofunguliwa na Shirika
la Stigmatine mwaka 1994.
Mradi huo ambao
unagharimu Sh. bilioni tisa utaondoa gharama kubwa za kuzalisha umeme kwa
mafuta ya dizeli, utawezesha Shule ya Msolwa kuwa na umeme wa uhakika,
utawezesha wananchi za vijiji vya Kisanga, Msolwa na Madizini kupata umeme wa
uhakika kwa bei nafuu na utaunganishwa moja kwa moja kwenye gridi ya taifa
katika jitihada za kupunguza tatizo la umeme nchini.
Gharama za umeme huo
ambao utaanza kuzalishwa Januari mwakani zimechangiwa na Serikali ya Tanzania
kupitia Mradi wa Umeme Vijiji – REA- na wananchi wa eneo hilo ambao wametoa
eneo kwa ajili ya ujenzi wa mradi.
Rais Kikwete anaendelea
na ziara yake katika Mkoa wa Morogoro leo.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
24 Agosti,2014



Post a Comment