MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), kwa mara ya kwanza amefunguka na kusema ana nia ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 iwapo chama chake kitaridhia.
Ametoa kauli hiyo ikiwa ni miaka miwili tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), alipojitokeza hadharani akisema kwamba hatawania tena ubunge katika jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu ujao na badala yake atajitosa kwenye urais.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Zitto ilisababisha mvutano mkubwa kati yake na viongozi wenzake ndani ya chama hicho, huku mmoja wa waasisi wake, Edwin Mtei, akipinga uamuzi wa mwanasiasa huyo na akidai hakuutoa wakati mwafaka. Mtei alisema hatua ya Zitto kutangaza kutaka kuwania urais wa mwaka 2015 haikuwa na shida kwa sababu alionyesha hisia zake lakini alikuwa ikitengeneza mzozo ndani ya chama.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA mwishoni mwa wiki iliyopita, Lissu alisema ana uzoefu wa uongozi hivyo yuko tayari kuwania urais iwapo vikao vya chama chake vitaridhia.
“Mimi ni Mwenyekiti wa Movement For Change Kanda ya Kati, pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama, vile vile ni mwanasheria mkuu wa chama.
“Kwa kuwa nina uzoefu mzuri wa uongozi, nitakuwa tayari kugombea urais iwapo vikao vya chama vitaamua,” alisema Lissu.
Huku akitabasamu, Lissu alimtania mwandishi wa habari hizi na hata kumhoji kama kauli yake itapewa nafasi ya juu katika gazeti lake.
“Tena hiyo kesho inaweza kuwa headline eeh!” alisema Lissu huku akitabasamu.
Lissu alisema kazi ya ubunge imempa fursa ya kuwatumikia wananchi katika kutatua matatizo yao, kuibua hoja na masuala yanayolitatiza taifa.
Alisema katika kipindi chote cha ubunge, pia alitumia utaalamu wa sheria kuboresha mfumo mzima wa ubunge ikiwa ni pamoja na kulifanya Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano kuwa bora na machachari kuliko Bunge la Tisa.
Lissu, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Sheria na Katiba, alisema hana hofu na watu wanaotaka kugombea ubunge katika Jimbo la Singida Mashariki ambako aliwakaribisha kwa mikono miwili.
“Sina wasiwasi. Ninawakaribisha sana Singida Mashariki waje tupambane kwenye uchaguzi mkuu unaokuja,” alisema.
Akizungumzia uamuzi huo wa Lissu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kauli ya mwanasiasa huyo haina tatizo.
“Sioni tatizo la Lissu kutangaza nia kwa sababu kila mtu anao uhuru wa kutamka na kugombea urais,” alisema Mbowe.
Chanzo: Mtanzania
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment