Katika
hali isiyo ya kawaida, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
wanadaiwa kuwafanyia ukatili mkubwa vijana 11, wakazi wa eneo la Keko
Magulumbasi B, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam kwa kuwapiga na
kuwalazimisha wanywe maji machafu yenye kinyesi.
Tukio
hilo ambalo limefananishwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,
linadaiwa kutokea Septemba 12 mwaka huu, saa 11 jioni, katika eneo la
Keko Magulumbasi B.
Inadaiwa
kuwa, wanajeshi hao ambao walikuwa saba wakiwa na sare za jeshi hilo,
walifika Keko Magulumbasi B wakiwa na kijana mmoja mwenye asili ya
Kiarabu na kuwavamia vijana waliokuwa wakila chakula kwenye kibanda cha
chipsi.
Mashuhuda
wa tukio hilo walidai kuwa, wanajeshi hao waliwakamata vijana hao na
kudai wanahusika kupora simu ya kijana mwenye asili ya Kiarabu aina ya
Tecno yenye thamani ya sh. 25,000.
Pamoja
na vijana hao kukataa kuhusika na tukio hilo, waliwekwa chini ya
ulinzi, kufungwa mikono kwa kamba, kulazwa kifudifudi na kuanza kupigwa
mikanda ya jeshi.
Mashuhuda
hao waliongeza kuwa, vijana hao walichukuliwa hadi kwenye bwawa la maji
machafu yaliyochanganyika na kinyesi cha binadamu wakazamishwa vichwa
vyao ndani ya bwawa hilo la kulazimishwa kunywa maji hayo.
Waliongeza
kuwa, vijana hao wakiwa wamelowana kwa maji machafu walichukuliwa na
wanajeshi hao hadi Kituo Kidogo cha Polisi Keko na kuswekwa rumande na
mmoja wao aliachiwa baada ya dakika 10.
Baadhi
ya wakazi wa eneo hilo, walilazimika kuvamia kituo hicho na kufanya
vurugu wakiwarushia mawe askari wa kituo hicho kwa lengo la kuwatoa
vijana hao kwa nguvu wakidai wameonewa.
Hata
hivyo, wananchi hao walitawanywa kwa risasi za moto zilizopigwa hewani
na askari wa Kituo Kikuu cha Polisi Chang’ombe walioitwa kuongeza nguvu
kituoni hapo.
Bw.
Omary Abdu (30) ambaye ni mkazi wa eneo hilo ambaye alikuwepo kwenye
eneo la tukio, alidai kutofurahishwa na kitendo kilichofanywa na
wanajeshi hata kama vijana hao wameiba kwani walipaswa kufikishwa katika
mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.
“Walichokifanya
wale wanajeshi ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na haki za
binadamu…naamini wanafahamika, itakuwa vizuri kama watachukuliwa hatua
za kisheria,” alisema.
Mkazi
mwingine wa eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliwashutumu
wakazi wenzake kwa kitendo cha kuvamia Kituo cha Polisi na kufanya fujo
kwa kuwarushia mawe polisi.
Katika
hatua nyingine, mkazi huyo alimtuhumu Mwenyekiti wa Mtaa wa Magulumbasi
B, Bw. Mohamed Fundi ambaye alidai kupitia kikao chake na wananchi
Agosti 29 mwaka huu, alihamasisha wagome kukamatwa na polisi.
Alidai kauli kama hiyo inaweza kuleta vurugu na uvunjifu wa amani hivyo zinatakiwa kukemewa na kila mkazi wa eneo hilo.
Mwandishi
alimtafuta Bw. Fundi ambaye alikiri kufanya kikao na wananchi kwa
tarehe hiyo ambacho kilikuwa na lengo la kuhamasisha maendeleo na
kuwafahamisha wananchi haki zao si kuhamasisha vurugu au kuzuia
wasikamatwe na polisi kama inavyoelezwa.
Alisema
miongoni mwa haki hizo ni namna polisi anavyotakiwa kumkamata raia na
asikamatwe usiku bila kuwepo kwa kiongozi wa eneo lake.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Kihenya Kihenya amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo akidai taarifa alizonazo ni kwamba, vijana
waliokamatwa wanajihusisha na wizi wa mifukoni.
Alisema
wakiwa Kituo Kidogo cha Polisi Keko, wananchi walikivamia na kufanya
vurugu hadi walipotawanywa na askari kutoka Kituo Kikuu cha Polisi
Chang’ombe kwa kupiga risasi hewani.
“Taarifa
zinazosema vijana hao waliteswa na kunyweshwa maji machafu na wanajeshi
bado sijazipata ila hawa vijana wanashikiliwa Kituo cha Polisi
Chang’ombe wakisubiri kufikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika,” alisema.
Inaelezwa
kuwa, wiki moja iliyopita kijana huyo mwenye asili ya Kiarabu mkazi wa
Keko Toroli, alivamiwa na vijana eneo la Keko Magulumbasi B, ambao
walimpora simu ya mkononi tukio ambalo liliripotiwa kwenye Kituo Kidogo
cha Polisi Keko.
Post a Comment