Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe (wapili kushoto)
akiwasalimia wacheza ngoma ya asili ya nchini Kongo iliyokuwa ikichezwa
na wakimbizi wenye asili hiyo wakati alipokuwa anaingia katika Ukumbi wa
Mikutano uliopo katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, Kasulu mkoani
Kigoma kwa ajili ya kuzungumza nao. Waziri Chikawe alifanya mkutano na
baadhi ya wakimbizi hao na kuwataka kulinda amani pamoja na kupinga ndoa
za utotoni ambazo zinaendelea kushika kasi katika kambi hiyo kubwa
inayowahifadhi zaidi ya wakimbizi 60,000.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe akizungumza na Wakimbizi wa
Kambi ya Nyarugusu wakati alipofanya ziara ya kikazi katika kambi hiyo
inayowahifadhi zaidi ya wakimbizi 60,000. Katika hotuba yake Waziri
Chikawe aliwataka wakimbizi hao kupinga ndoa za utoto ambazo
zinaendelezwa na baadhi ya familia za wakimbizi hao ambapo
inawasababishia watoto hao wa kike kupata matatizo mbalimbali wakati
wanapojifungua.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe (kulia) akipokea zawadi
kutoka kwa Wakimbizi wa Kambi ya Nyarugusu, Wilaya ya Kasulu mkoani
Kigoma. Waziri Chikawe ambaye yupo katika ziara ya kikazi katika kambi
hiyo, aliwataka wakimbizi hao wadumishe amani pamoja na kupinga ndoa za
utotoni ambazo zimeshika kasi katika kambi hiyo kubwa ambayo ina
wahifadhi zaidi ya wakimbizi 60,000. Kushoto kwa Waziri ni Mwakilishi
Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR),
Joyce Mends-Cole.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe (kushoto) akiwasalimia
watoto wa wakimbizi wakati Waziri huyo alipokuwa anatembelea baadhi ya
familia za wakimbizi hao kwa lengo la kuwasalimia pamoja na kuangalia
jinsi maisha yao wanavyoyaendesha kambini hapo. Waziri Chikawe alifanya
mkutano na wakimbizi hao na kuwataka kulinda amani na pia kupinga ndoa
za utotoni ambazo zinaendelea kushika kasi katika kambi hiyo kubwa
inayowahifadhi zaidi ya wakimbizi 60,000. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa
Idara ya Wakimbizi, Harrison Mseke. Picha zote na Felix Mwagara, Wizara
ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
WAZIRI
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amewataka Wakimbizi wa Kambi
ya Nyarugusu kuacha mara moja tabia ya kuwaozesha watoto wao wenye umri
mdogo kwani tabia hiyo inawaletea matatizo makubwa watoto wao wakati
wanapojifungua.
Akizungumza
na mamia ya wakimbizi hao katika Ukumbi wa Mikutano katika kambi hiyo
iliyopo wilayani Kasulu, Mkoa wa Kigoma, Waziri Chikawe alisema katika
maisha yake, yeye ni mpambanaji wa kupinga ndoa za utotoni ambazo
zinawaletea madhara makubwa watoto.
Chikawe
alifafanua kuwa, tabia hiyo inayofanywa na wakimbizi hao dhidi ya
watoto wao inawasababishia watoto hao kupatwa na matatizo makubwa
kipindi wanapojifungua kwani viungo vyao vya uzazi havipo tayari kwa
ajili ya kuzaa hivyo aliwataka familia za wakimbizi hao kuacha tabia
hiyo ya kikatili dhidi ya watoto wao na pia inawakosesha haki zingine za
msingi watoto hao.
“Wapeni
haki zao watoto wenu, utamaduni huu sio mzuri wa kuwaozesha watoto
wadogo, mnatakiwa kuuacha na kuulaani kwani mkifanya hivyo mtakuwa
mnawaletea matatizo makubwa watoto wenu hasa wanapojifungua,” alisema
Chikawe.
Aidha,
Waziri Chikawe aliwataka wakimbizi katika kambi hiyo kuwa makini na
ugonjwa wa Ukimwi kwani ugonjwa huo unaendelea kuua maelfu ya watu
duniani na pia bado hauna dawa, na kuwataka wakimbizi hao kuacha tabia
ya ufuska na endapo watashindwa basi watumia kondomu kwa ajili ya
kujikinga na ugonjwa huo hatari.
Kwa
upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la
Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR), Joyce Mends-Cole, aliwaonya wakimbizi hao
kuacha tabia hiyo ya kuwaoza watoto wao ambao wapo chini ya miaka 18
kwani kwa kufanya hivyo Wakimbizi hao watashindwa kupata nafasi ya
kwenda nchini Marekani.
“Si
mnajua tunawaandaa kwenda Marekani?, kama mnalijua hilo basi endapo
mkimbizi yeyote akimpa mimba mtoto mdogo basi hataweza kupata nafasi ya
kwenda nchini humo, hivyo kuweni makini ili muweze kwenda nchini
Marekani,” alisema Joyce.
Zaidi ya wakimbizi 30,000 wa Kambi ya Nyarugusu wanatarajiwa kuhamishiwa katika nchi ya Marekani kuanzia mwaka 2015.
Waziri
Chikawe ambaye aliambatana na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wakimbizi
nchini, Harrison Mseke pamoja na maafisa wengine wa wizara yake,
amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Kigoma ambapo katika siku
hizo alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma.
Pia
alikitembelea Kituo cha Mpito cha Wakimbizi (NMC) kilichopo mjini Kigoma
na baadaye akamalizia ziara yake katika Wilaya ya Kasulu mkoani humo
kwa kuitembelea Kambi kubwa ya wakimbizi ya Nyarugusu inayowahifadhi
wakimbizi zaidi ya 60,000 ambapo wengi wao wakiwa ni kutoka nchini
Kongo, Burundi na wachache kutoka mataifa mengine.
Post a Comment