TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
*Ataka iundwe timu ya watu wachache kusimamia kiwanda
*Amtaka mwekezaji kukubali kufanya kazi na timu ya Serikali
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka Wakala wa Wakulima Wadogo wa Chai pamoja
na Bodi ya Chai nchini waangalie uwezekano wa kuunda timu ya watu wawili
au watatu itakayosimamia mwenendo wa kiwanda cha chai Mponde, kilichopo
wilayani Lushoto mkoani Tanga. Waziri
Mkuu ambaye aliwasili jijini Tanga jana asubuhi (Jumamosi, Septemba 13,
2014) akitokea Dodoma, alipokea taarifa fupi ya mgogoro wa kiwanda
hicho kabla ya kuzungumza na wakulima, wadau wa zao la chai na viongozi
wa mkoa na wizara kadhaa kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga.“Wakala
wa Wakulima pamoja na Bodi ya Chai itabidi watusaidie kuunda timu kwa
sababu tunahitaji kuwa na jicho la Serikali ndani ya kiwanda… tunahitaji
watu wenye uzoefu mkubwa na mambo ya chai ili wasimamie uendeshaji wa
kiwanda pindi kitakapoanza kazi,” alisema.
“Vilevile
mwekezaji itabidi akubali kufanya kazi na timu ya Serikali ili tuweze
kujua kwa leo kiwanda kiko katika hali gani na tukitaka kukifungua ni
lazima tufanye nini,” aliongeza.
Waziri
Mkuu alisema timu hiyo kwa kushirikiana na mwekezaji hawana budi
kuandaa mpango-kazi wa miaka miwili hadi mitatu wa kufufua kiwanda ili
uzalishaji wa chai ufikie pazuri. “Kiwanda wakati kinabinafsishwa
kilikuwa na uwezo wa kusindika kilo 20,000 za majani ya chai lakini
kilikarabatiwa na kufikisha uwezo wa kusindika kilo 120,000 kwa siku.
Sasa tuangalie uwezekano wa kuongeza uzalishaji kwani hapo tutaweza pia
kuongeza mavuno kwa wakulima wetu,” alisema.
Alisema
ili kuweza kusonga mbele, itabidi Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali (CAG) aende kufanya ukaguzi kwenye kiwanda hicho ili kuweza
kutoa picha halisi ya kiwanda hicho kwa sababu Serikali ina hisa.
Kiwanda
cha Chai cha Mponde kinamilikiwa na Chama cha Wakulima wa Chai cha
UTEGA (Usambara Tea Growers Association) ambacho kilitafuta mwekezaji
ambayo ni Kampuni ya Chai ya Lushoto (Lushoto Tea Company). Wakulima wa
Chai walikifungia kiwanda hicho kisifanye kazi kwa madai kuwa walikuwa
hawalipwi walipo kwa wakati, wamiliki kutumia lugha chafu,
Baada
ya kusikiliza pande zote, Waziri Mkuu alikubaliana na rai iliyotolewa
na pande hizo kwamba kuna haja ya kufungua kiwanda hicho ambacho
kilifungwa tangu Mei 26, 2013 ili kuwasadia wakulima wapate soko la chai
lakini pia waweze kujikimu mahitaji yao.
Mapema,
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Bibi Chiku Gallawa alisema mkoa wa Tanga
ulijipanga kukuza kiwango cha ukusanyaji mapato ili kuendana na mpango
wa Serikali wa matokeo makubwa sasa lakini kufungwa kwa kiwanda hicho,
kumeshusha pato la mtu mmoja mmoja, pato la mkoa na pato la Taifa kwa
ujumla.
“Changamoto
kubwa ambayo tumekabiliana nayo kwa kipindi chote hiki ambacho kiwanda
kilikuwa kimefungwa, ni kwa wananchi kushindwa kuuza chai yao,”
aliongeza.
Naye,
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Bw. Majjid Mwanga akitoa taarifa mbele ya
Waziri Mkuu alisema kiwanda cha Mponde kilikuwa na uwezo wa kusindika
kilo 70,000 za majani mabichi ya chai kwa siku lakini hadi kinafungwa
uwezo huo ulishuka na kufikia kilo 25,000 kwa siku.
Alisema
idadi ya wakulima walioathirika kutokana na kufungwa kwa kiwanda hicho
ni 3,908 ambao walikuwa wakilima hekta 1,951. “Bei ya kilo moja ya chai
ilikuwa ni sh. 225/- wakati wastani wa pato la mkulima kwa nusu hekta
ilikuwa ni sh. 180,000/- kwa mwezi lakini kwa sasa limeshuka na kufikia
sh. 90,000/- kwa mwezi kwa nusu hekta hiyo hiyo,” alisema.
Alisema
zaidi ya tani 1,800 zimeshindikana kusindikwa na hivyo kuikosesha
Halmashauri yao kiasi cha sh. milioni 21.6/- ambazo zilikuwa zikilipwa
kama ushuru kwa kila kilo moja iliyokuwa ikiuzwa. “Wakulima kwa ujumla
wao wamepata hasara ya sh. milioni 370.8/-” alisema.
Mkutano
huo pia ulihudhuriwa pia na Mawaziri wa OWM-TAMISEMI; Kilimo, Chakula
na Ushirika; Viwanda na Biashara, Wabunge wa Mlalo, Bumbuli na Lushoto;
viongozi wa Mkoa na Halmashauri za Korogwe, Lushoto na Bumbuli, viongozi
wa UTEGA na mwekezaji, ambaye ni mmiliki wa kiwanda cha Lushoto Tea
Company.
Post a Comment