Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Alik Iddi alisema ushirikiano
ulioonyeshwa kati ya wananchi wa Wete – Gando na Mjenzi wa Bara bara ya
Wete Gando umesaidia kufanikisha ujenzi wa bara bara hiyo kwa zaidi ya
asilimia Thamanini.
Balozi
Seif alisema hayo wakati akizungumza na wajenzi wa bara bara hiyo
Kampuni ya Mecco, wahandisi wa Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano
Zanzibar pamoja na Wananchi wa Gando mara baada ya kuitembelea Bara bara
hiyo kutoka Wete hadi Gando.
Alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajitajidi kuwa na miundo mbinu
mizuri na ya kisasa ya mawasiliano na Bara bara katika kiwango
kinachokubalika Kimataifa ili watumiaji wake waendelee kufaidikia nayo
katika kujiharakishia maendeleo ya Kiuchumi na ustawi wa Jamii.
“
Tunahitaji kuwa na Bara bara zilizo katika kiwango kinachostahiki
kimatumizi ili wananchi waendelee kufaidika katika kujiletea maendeleo
yao ya kiuchumi na kiustawi wa Jamii “. Alisema Balozi Seif.
Aliupongeza
Uongozi wa Kampuni ya Mecco chini ya Mkandarasi wake kwa juhudi
inayochukuwa ya ujenzi wa Bara bara hiyo ambayo kukamilika kwake italeta
ukombozi mkubwa na kuwaondoshea usumbufu wa usafiri wananchi wa ukanda
wa kaskazini mwa Kisiwa cha Pemba.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi wa Kampuni ya Mecco
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kadri ya uwezo
uliopo katika kuipatia fedha za vifaa Kampuni hiyo ili ikamilishe ujenzi
wa Bara bara hizo kwa wakati.
Balozi
Seif alimuomba Mkandarasi wa ujenzi huo aendelee kuwa mstahamilivu kwa
vile ameonyesha muelekeo mkubwa wa uzalendo wa kusimamia maendeleo ya
kiuchumi katika sekta ya mawasiliano kwa upande wa bara bara.
Akitoa
maelezo Meneja wa Kampuni ya Mecco Bwana Abdullkadir Mohamed Bujeti
alisema mradi huo umepangwa kukamilika kazi zilizobakia mwezi Disemba
mwaka huu iwapo fedha za ununuzi wa vifaa vilivyobakia zitapatikana kwa
wakati.
Bwana
Bujeti alisema hadi sasa gharama za ujenzi huo kwa awamu ya kwanza
zimeshafikia Shilingi za Kitanzania Bilioni sita wakati zile
zinazohitajika kwa ununuzi wa vifaa hivyo ni kiwango hicho hicho cha
shilingi Bilioni Sita.
Meneja
huyo wa Mecco alivitaja vifaa vitakavyohitajika katika ukamilishaji huo
ni pamoja na lami, mafuta, rangi pamoja na vifaa vya kuashiria uwepo
wa sehemu za hatari katika bara bara hiyo.
Mapema
msimamizi wa ujenzi wa Bara bara hiyo kutoka Wizara ya Miundo Mbinu na
Mawasiliano Zanzibar Mhandishi Japhet Malambi alisema kasi ya
utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa bara bara ya Wete – Gando imekuwa
kubwa na ya kuridhisha ikizingatia viwango.
Mhandishi
Japhet alisema mkandarasi wa ujenzi huo aliamua kusitisha shughuli zote
za ujenzi na kusababisha kudorora kwa mradi huo baada ya kutokuwa na
mhandisi Mkaazi ambae ndie msimamizi na mshauri wa mradi.
Alisema
hatua hiyo iliyochukuwa muda mrefu imepelekea wananchi wa wanaotumia
bara bara hiyo kupoteza matumaini ya kukamilikwa kwa mradi wa bara bara
hiyo.
Mhandisi
Japhet Malambi alitahadharisha kwamba ili kunusuru hasara nyengine
inayoweza kutokea endapo mradi huo utasimama tena ni vyema Serikali
ikajikita katika upatukanaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya
kukamilisha kazi hiyo.
Wakati
huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alikuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ms Shimoja kutoka
Jimbo la Michigan Nchini Marekani Dr. Robert Shumake.
Mazungumzo
hayo yamefanyika katika chumba cha watu mashuhuri { VIP } kilichopo
kwenye uwanja wa ndege wa Pemba ambapo Balozi Seif aliwasili akitokea
Mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa Bunge Maalum la Katiba.
Katika
mazungumzo yao Mkurugenzi Mkuu huyo wa Kampuni ya Ms Shimoja Dr. Robert
Shumake ambaye amepata heshima ya kuwa Balozi wa Heshima wa Tanzania
Nchini Marekani alielezea kuridhika na mazingira mazuri ya uwekezaji
kisiwani Pemba.
Dr.
Shumake alisema Uongozi wa Kampuni yake utaangalia maeneo ambayo
inaweza kuwekeza vitega uchumi kama alivyomuahidi Balozi Seif wakati wa
ziara yake katika Jimbo la Seattle Nchini Marekani mwaka jana.
“
Muda wangu mfupi niliopata kutembelea maeneo tofauti ya Tanzania
ikiwemo Zanzibar umenipa faraja na shauku ya kuangalia fursa zilizopo za
uwekezaji na namna uongozi wa Kampuni yangu utakavyochangamkia fursa
hiyo “. Alisema Dr. Robert Shumake.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliuhakikishia Uongozi wa Kampuni hiyo ya Ms. Shimoja kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuupa msaada wakati unaohitaji
kuwekeza hapa Zanzibar.
Balozi
Seif alimueleza Dr. Shumake kwamba Zanzibar tayari imetoa fursa kwa
wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza miradi na vitega uchumi vyao ili
kusaidia kunyanyua pato la taifa sambamba na kuongeza soko la ajira.
Alisema
yapo maeneo na sekta ambazo Kampuni ya Ms Shimoja inaweza kuyatumia
kuwekeza akiyataja kuwa ni patoja na upanuzi wa uwanja wa ndege wa
Pemba, Bandari ya Wete, Sekta ya utalii pamoja na nyumba za mkopo nafuu.
Alifahamisha
kwamba miradi ya nyumba za mikopo nafuu kwa kiasi kikubwa inaweza
kuwasaidia zaidi vijana wenye ajira mpya ili wajenge hatma bora ya
maisha yao ya baadaye.
Dr.
Robert Shumake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ms. Shimoja ambae pia ni Balozi
wa Heshima wa Tanzania Nchini Marekani alikuwepo Nchini Tanzania kutia
saini mkataba wa uanzishwaji wa treni iendapo kwa mwendo wa kasi kati
yake na Wizara ya Uchukuzi ya Tanzania.
Treni
hiyo itakapokamilika itakuwa ikitoa huduma ya usafiri kati ya Dar es
salaamu na pugu kwa kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius
Kambarage Nyerere.
Imetolewa na:
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/10/2014.

.jpg)

Post a Comment