Mbunge
wa jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo mkoani Kigoma kupitia chama cha
NCCR Mageuzi Felix Mkosamali amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya
Kibondo akituhumiwa kumzuia karani mwandikishaji wapiga kura kwa ajili
ya uchaguzi wa serikali za mitaa na vijiji kufanya kazi yake.
Mh.Mkosamali ambaye alilala rumande baada ya kukamatwa na polisi
Jumatatu jioni amefikishwa mbele ya hakimu wa wilaya ya Kibondo Erick
Maley na kusomewa shitaka lake na mwendesha mashtaka wa jeshi la polisi
Peter Makala.
Ilidaiwa kuwa Mkosamali alimzuia karani mwandikishaji wapiga kura
Kadiri Hamidu katika kituo cha Nduta katika kitongoji cha Nduta kijiji
cha Kumuhasha kata ya Murungu wilayani Kibondo kuendelea na zoezi la
kuandikisha wapiga kura baada ya kuchukua vitabu na karatasi alizokuwa
akiandikia kinyume cha sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa na
vijiji.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, mh.Felix Mkosamali alikana na ameachiwa kwa dhamana hadi Disemba 29 kesi yake itakapotajwa tena.
Tukio hilo liliilazimu jeshi la polisi wilayani kibondo kuimarisha
ulinzi katika eneo la mahakama kutokana na idadi kubwa ya watu waliofika
kushuhudia ambapo baadhi yao wameshauri viongozi kushirikiana ili
uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Disemba 14 uende
vizuri
Post a Comment