Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God jijini Dar, Dk. Getrude Rwakatare.
Sakata
la Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Assemblies of God jijini Dar, Dk.
Getrude Rwakatare (pichani) kufunguliwa kesi ya uharibifu wa mali katika
Kituo cha Polisi cha Wazo Hill, limechukua sura mpya baada ya faili la
kesi hiyo kupotea katika mazingira ya kutatanisha, huku ikidaiwa kwamba
limeibwa.
Kufuatia
kudaiwa kuibwa kwa faili hilo lililopewa namba WH/RB/9029/ 2014,
UHARIBIFU WA MALI, mlalamikaji, Grayson Justine Mghamba amemwandikia
barua mkuu wa upelelezi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni akilalamika kwamba
anahisi kuna njama zinaendelea ili kumnyima haki yake.
Taarifa
zilizopatikana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, Kinondoni jijini Dar,
zinadai kwamba Grayson alimwandikia barua mkuu huyo wa upelelezi Desemba
2, mwaka huu akiomba msaada kuhusu shitaka hilo aliloripoti polisi
Novemba 20, 2014 akimtuhumu mama Rwakatare kumvunjia nyumba yake na
kumpora kiwanja kilichopo eneo la Bunju B, Kinondoni.
Sehemu ya barua hiyo ambayo Uwazi inayo nakala yake, inasomeka:
“Nasikitika
kusema kuwa kila nifuatiliapo faili langu ili niweze kumjua mpelelezi
wa kesi yangu, naambiwa kwamba halionekani wakati wao ndiyo waliniambia
nifuatilie.”
Uwazi lilipomtafuta
Grayson na kumuuliza kuhusu sakata hilo, alikiri kuandika barua hiyo na
kusema kwamba amefuatilia zaidi ya siku tano kwenye Kituo cha Polisi
cha Wazo Hill alikofungulia kesi hiyo lakini anaambiwa faili
halionekani.
“Nimejaribu
kuwaambia kama hilo faili la kwanza limeibwa basi wafungue lingine
lakini wamekataa,” alisema Grayson ambaye habari yake ya kuvunjiwa
nyumba na mama Rwakatare iliripotiwa kwa mara ya kwanza na Gazeti la Uwazi wiki iliyopita ikiwa na kichwa cha habari: MAMA RWAKATARE AFIKISHWA POLISI.
Katika
malalamiko yake, Grayson anadai kuvunjiwa nyumba yenye thamani ya zaidi
ya shilingi milioni 20 na mchungaji huyo, ambayo aliijenga kwa fedha
alizochukua mkopo kazini kwake.
Grayson
alidai kwamba nyumba yake hiyo ilivunjwa na greda kipindi alipoenda
Moshi kwenye msiba wa baba yake na kiwanja chake anachodai kukinunua
kihalali kwa kuandikishana na aliyemuuzia kwenye Ofisi za Serikali ya
Mtaa wa Bunju B, kuzungushiwa ukuta.
Uwazi lilipomtafuta
Mchungaji Rwakatare na kumhoji kuhusu sakata hilo, alisema kwamba
kiwanja hicho ni mali yake tangu mwaka 2005 na alivunja nyumba hiyo kwa
sababu alikuwa akikifanyia usafi kiwanja hicho alichodai kilivamiwa.
CHANZO:GAZETI LA UWAZI
Post a Comment