Na Mwandishi wetu
MAHAKAMA
ya Mwanzo Mbagala, Dar es Salaam imesema haiwezi kumuamuru Mmiliki wa
nne za Shule za Sekondari, St Mathew na St Marks ,Thadei Mtembei kutoa
talaka kwa Magreth Mwangu kutokana na ndoa yao kuwa batili.
Akisoma
hukumu hiyo leo, Hakimu Rajab Tamambele alisema ndoa aliyofunga Mwangu
pamoja na Mtembei ambayo ni ya kimila ni batili kwa kuwa mdai hakutoa
cheti cha ndoa hiyo ilipofungwa.
Alisema
kwa misingi hiyo, mahakama haiwezi kumuamuru Mtembei kutoa talaka kwani
aliwasilisha cheti cha ndoa ya mke mmoja aliyoifunga mwaka 1985.
pia
alisema mahakama hiyo haiwezi kugawa mali kama ambavyo mdai ameiomba
mahakama, ambapo amesisitiza kuwa mgawanyo wa mali unatokana na ndoa
halali ambayo baba na mama wanaishi pamoja.
‘’Mashahidi
wote wameeleza kuwa Mtembei na Mwangu walikuwa wanakutana hoteli ya
Sleep Inn. Kwa hivyo mahakama inaona kuwa uhusiano kati ya mdai na
mdaiwa ulikuwa wa kimapenzi pekee au hawara na kwa lugha ya kistaarabu
tunaita mzazi mwenzie,’’ aliongeza Tamambele.
Alifafanua kuwa kulipa mahari ambapo mdai aliieleza mahakama kuwa
alitolewa ng’ombe watano, sio njia ya kufunga ndoa bali ni kuelekea
kufunga ndoa.
Aliendelea
kusema kuwa kitendo cha baba kupewa mahari akiwa peke yake bila ya kuwa
na mzee wa kabila hilo kuthibitisha, sio sahihi katika sheria za ndoa.
Akisoma
hukumu hiyo kwa saa moja, Hakimu Tamambele alisema kuwa watoto watatu
kati ya Mtembei na Mwangu ni batili kwani wamezaliwa nje ya ndoa, hivyo
mahakama haiwezi kuamuru watoto hao kupatiwa matunzo.
‘’Mdaiwa
anatakiwa kushukuru kitendo cha mdai kujenga nyumba tatu kwa ajili ya
watoto kwani wengine hawawezi kufanya kitu kama hicho. Kila mzazi
anatakiwa kuwatunza watoto hao, ’’ alisema.
Akizungumzia
kuwakilishwa kwa mdaiwa, alisema kwa mujibu wa sheria ya kama mdaiwa
ni mgonjwa anaweza akawakilishwa ambapo mtoto wake, Peter ndiye
alichukua nafasi ya kumuwakilisha baba yake.
Aidha, alisema haki ya kukata rufaa kwa mdai iko wazi na kwamba inatakiwa kukatwa kwa siku 45.
Katika
kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Juni 5, mwaka huu, Mwangu aliiomba
mahakama kumuamuru mdaiwa kutoa talaka, matunzo ya watoto na ya machumo
ya pamoja yenye thamani ya Sh milioni 800.
Alisema kesi hiyo ilikuwa na jumla ya mashahidi nane ambapo watano kutoka upande wa mdai na watatu upande wa mdaiwa.
Alisema
mdai alifungua kesi kupitia ofisi ya Ustawi wa jamii na ilipoanza
kusikilizwa mdai alisema walianza mahusiano mwaka 1995 ambapo walizaa
watoto watatu na walijenga shule nne, nyumba pamoja na hoteli tatu za
Dar es Salaam na Bukoba.
Post a Comment