Mwandishi wa makala hii ni Ananilea Nkya ambaye ni Mkurugenzi Mstaafu wa TAMWA.
******
Watu wanaokampeni kushawishi Watanzania wamchague John Magufuli kuwa Rais wa tano wa Tanzania kwa kutumia kigezo cha uadilifu wanadhani ataweza kuzuia serikali ya CCM kuwa fisadi na hivyo umaskini wa wananchi kupungua.
Kimsingi
wanajidanganya maana Magufuli akichaguliwa ufisadi wa kimfumo
unaofanywa na serikali ya CCM ili chama hicho kibaki madarakani
utaendelea kwa kasi na hivyo pengo kati ya watawala wachache kutajirika
kufuru na mamilioni ya wananchi maskini wa kutupa litaongezeka mara
dufu.
Nchi
yetu ilipopata uhuru maadui wa ustawi wa wananchi walikuwa ni
watatu—adui mkuu ujinga— na adui wengine wawili wanaotokana na
ujinga—adui umaskini na adui maradhi.
Lakini
katika zama hizi za utandawazi na demokrasia ya vyama vingi vya
siasa ameongezeka adui mwingine hatari nchini kwetu–adui ufisadi.
Ufisadi ameshamiri nchini baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanza mwaka 1992.
Chanzo
cha ufisadi nchini ni CCM kung’ang’ania madaraka kwa kutumia nguvu
ya fedha na hivyo serikali yake kila inapochaguliwa hugeuka kuwa
fisadi na kuiba fedha na mali za umma.
Hivyo,
ikitokea Magufuli akichaguliwa wananchi wengi wataendelea kuwa
maskini kwa sababu inaelekea Magufuli mwenyewe au hajui au haamini
kwamba chanzo cha umaskini nchini ni serikali ya CCM kuwa fisadi
na kuendekeza rushwa, ubabe, giliba, uongo na siasa za maji taka
kushinda uchaguzi.
Inaelekea
Magufuli hajatambua kuwa kuzuia ufisadi unaozaa mafuriko ya wananchi
maskini Tanzania kunahitaji nchi iweke misingi ya kikatiba, lakini CCM
kwa kukataa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi isiandikwe
2014 iliikataa misingi hiyo kwa sababu kinajua kinanufaika na udhaifu
wa kikatiba uliopo sasa.
CCM
inachofanya sasa ni Magufuli kuwapumbaza wananchi kwamba eti baada ya
yeye kuteuliwa kugombea Urais kwa tiketi ya CCM, mafisadi wameanza
kuikimbia CCM.
Magufuli
anataka kuwaaminisha Watanzania kuwa umaskini unakabili mamilioni ya
Watanzania umesababishwa na wanaCCM walioondoka kwenye chama hicho
baada ya yeye kuteuliwa kugombea Urais!
Pengine
ndiyo sababu Magufuli anaahidi kwenye kampeni zake kwamba akichaguliwa
Rais ataanzisha mahakama ya mafisadi kama alivyokaririwa kwenye
mikutano yake ya kampeni huko Dodoma.
Ninanukuu: ‘’Baadhi
ya mafisadi wezi wameanza kukimbia baada ya CCM kuniteua mgombea urais
lakini nikiingia Ikulu, nitawafuata huko waliko ili niwashughulikie
vizuri ndiyo maana nimesema nitaunda mahakama ya mafisadi’’
Wananchi
wanajiuliza kama ufisadi wa fedha na mali za nchi unafanywa na
serikali inayopewa dhamana ya kuwa mlinzi wa fedha na mali za
Watanzania endapo Magufuli atachaguliwa na serikali yake kuunda
mahakama ya mafisadi, je majaji wa mahakama hiyo watapata wapi ujasiri
wa kumtia hatiani fisadi mkuu (serikali) wakati kiongozi mkuu wa
serikali (Magufuli) ndiye atakuwa amewateua majaji wa mahakama hiyo?
Je serikali inaweza kujihukumu yenyewe?
Aidha
wananchi wanajiuliza je serikali ya CCM imekuwa ikishindwa
kuchukua hatua za kisheria kudhibiti ufisadi wa fedha na mali za umma
unaofanywa na serikali ya kwa vile nchi haina mahakama maalumu ya
kushughulikia kesi za ufisadi au ni kwa vile chama chao ni mnufaika wa
ufisadi?
Wananchi wanauliza swali hili kwa sababu ipo mifano mingi kuonyesha serikali ya CCM ni fisadi .
Mfano wa kwanza:
Ufisadi wa EPA kuiba kwenye Akaunti ya EPA benki kuu jumla ya shilingi
bilioni 133 mwaka 2005/6. Wananchi walishangaa kuona Rais wa Jamhuri
yetu alivyopata kigugumizi kwenye ufisadi huo.
Wananchi
wanajiuliza ilikuwaje mlinzi mkuu (serikali ya CCM) kama kweli
haikunufaika na ufisadi wa EPA haikuchukizwa na kitendo hicho cha aibu
na kuchukua hatu za kisheria?
Kadhalika
wananchi wanajiuliza, kama kweli wizi huo wa EPA haukuhusisha serikali
yenyewe kunufaisha CCM ni kwa nini serikali ya CCM ilisema waliokwapua
fedha hizo wamepewa muda wa kuzirejesha benki na hadi leo (miaka 10
baadaye) haijawatangazia Watanzania hatma ya fedha hizo?
Mfano wa pili: Ufisadi
wa Richmond. Kukotana na ukosefu wa umeme nchini serikali ya CCM
iliingia mkataba na kampuni ya kigeni Richmond ili nchi ipate umeme.
Kabla kampuni hiyo kuanza kuzalisha umeme zilitoka tuhuma kwamba Richmond ilikuwa ni kampuni feki.
Wakati
huo Edward Lowassa alikuwa Waziri Mkuu, kimamlaka hakuwa Waziri wa
Nishati, lakini aliamua kujiuzulu kulinda heshima ya serikali.
Lakini
cha kushangaza baada ya kujiuzulu Lowassa kampuni ya Dowans
iliyoirithi Richmond iliendelea kulipwa fedha nyingi kila mwezi hadi
zikafikia bilioni 172.
Wananchi
wanajiuliza kama CCM ilikuwa hainufaiki na mabilioni hayo
yaliyokuwa yanalipwa Dowans na kwamba mnufaika wa ufisadi huo alikuwa
ni Lowassa ni kwa nini Dowans waliendelea kulipwa baada ya Lowassa
kuachia ngazi? Ni kwa nini Lowassa hajafikishwa mahakamani hadi leo kama
tuhuma dhidi yake zina ushahidi?
Wananchi
wanajiuliza kama CCM na serikali yake wanajinasibu ni walinzi
waaminifu wa mali na rasilimali za Tanzania na kwamba wanastahili
kuendelea kuajiriwa kuwa mlinzi mkuu wa fedha na mali za Tanzania baada
ya uchaguzi tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015 ni kwa nini serikali ya CCM
ilipata kigugumizi kumpeleka Lowassa mahakamani kumdai alipe hizo
shilingi bilioni 172 kama kweli ndiye aliyenufaika na ufisadi huo?
Mfano wa tatu: Ufisadi
wa kuuza kwa bei chee nyumba za Watanzania zenye thamani ya mabilioni
ya shilingi huku leo hii serikali ikitumia fedha nyingi za umma
kuwapangishia makazi hotelini watawala.
Wananchi wanafahamu kuwa msimamizi wa uuzwaji wa nyumba hizo ulifanyika wakati Magufuli akiwa na Waziri nyumba na makazi.
Karibu
nyumba za umma elfu kumi ziliondoka mikononi mwa umma na hadi leo
Watanzania hawajaelezwa zilipatikana shilingi ngapi kwenye mauzo ya
nyumba hizo na zilitumika kufanya jambo gani la kuwaondolea wananchi
umaskini.
Aidha katika uuzaji wa nyumba za umma Magufuli anatuhumiwa kuwauzia baadhi ya ndugu zake.
Wananchi
wanajiuliza kama Magufuli na Lowassa wote walikuwa ni watendaji katika
serikali ya CCM, na wote ufisadi umefanyika kwenye maeneo ambayo
walikuwa na dhamana, ni kwa nini leo Magufuli anashabikiwa na CCM
kuwa ni mwadilifu ili hali Lowassa akipakaziwa ufisadi ?
Aidha,
wananchi wanauliza ufisadi kwa Magufuli katika kusimamia kwa niaba
ya serikali ya CCM uuzaji kwa bei poa nyumba za umma umetoweka kwa
vile tu anagombea Urais kwa tiketi ya CCM na tuhuma za ufisadi kwa
Lowassa mkataba wa Richmond umebaki kwa sababu tu ameamua kuondoka CCM
na kugombea Urais kwa tiketi ya CHADEMA –chama kinachowakilisha vyama
vinne vya upinzani vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi-UKAWA?
Mfano wa Nne:
Ufisadi wa Tegeta escrow 2014, serikali ya CCM ilifisadi bilioni 306.
Watuhumiwa wa ufisadi huo walienea ofisi mbali mbali za serikali hadi
ofisi kuu ya ya nchi –Ikulu inayopaswa kuwa mahali patakatifu
ilihusishwa na ufisadi huo!
Tena
wananchi walielezwa jinsi mabilioni ya fedha hizo zilivyokwapuliwa
kibabe nyingine zikibebwa kwa magunia na tandarusi mchana kweupe.
Watawala
wa CCM waliopaswa kujiuzulu kama Lowassa alivyojiuzulu na kisha
kupakaziwa ufisadi tuliona jinsi walivyosafishwa na serikali ya CCM
yenyewe!
Wananchi
wanajiuliza kama ufisadi wa Richmond haukuwa mkakati wa CCM wa kutumia
siasa za maji taka kumtoa Lowassa kafara wa ufisadi kudanganya
wananchi kwamba serikali ya CCM siyo fisadi bali fisadi ni Lowassa ni
kwa nini Magufuli kwa dhamana yake kama Waziri wa Nyumba alisimamia
ufisadi wa nyumba za umma CCM inamuona mwadilifu na Waziri wa nishati
Muhongo aliyekuwa na dhamana wakati wa ufisadi wa Tegeta escrow
alisafishwa ili hali Lowassa aliyesimamia ufisadi wa mkataba wa
Richmond anapakaziwa ufisadi?
Zaidi
wananchi wanajiuliza kama chanzo cha ufisadi nchini kama vile Magufuli
na CCM wanayotaka kuaminisha umma ni LOwassa na wengine walioondoka
CCM, je ni kwa nini serikali ya CCM imekumbwa na ufisadi wa Tegeta
escrow miaka saba baada ya Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu?
Hakika
ziko fisadi nyingi zilizohusisha viongozi wa serikali ya CCM iwe ni
kwenye miradi ya kitaifa au kwenye halmashauri na mikataba ya mali za
nchi kama vile madini kuonyesha kwamba umaskini wa wananchi
unasababisha na ufisadi wa serikali ya CCM.
Ndiyo
sababu kwa kutumia mifano hii minne wananchi wanajiuliza ni kwa
nini CCM imtoe Edward Lowassa kafara wa ufisadi ili hali serikali
ya CCM ndiyo fisadi?
Kadhalika
wananchi wanajiuliza ni kwa nini Edward Lowassa ambaye ameamua
kuondoka CCM kutumia haki yake ya kikatiba kutimiza ndoto yake ya
kugombea Urais , CCM inamuona tishio na hafai kuwa Rais?
Kama
alikuwa hafai kuwa Rais kutokana na ufisadi ilikuwaje alipewa dhamana
kubwa ndani ya serikali ya CCM kuanzia uwaziri hadi Waziri Mkuu na
akajiuzulu uwaziri mkuu ili kuzuia serikali ya chama chake isianguke
kutokana na ufisadi?
Wananchi
wanajiuliza hivi tatizo hapa ni ufisadi wa Lowassa kweli au ni CCM
kutaka kung’ang’ania madaraka ya kuongoza hata kama wananchi hawakitaki
tena chama hicho kiongoze nchi?
Wananchi
pia wanajiuliza hivi tatizo ni Lowassa ambaye anao uzoefu mkubwa wa
kuongoza serikali na ambaye rekodi yake inaonyesha kuwa ni mchapa kazi
au tatizo ni kwa vile anagombea Urais kupitia CHADEM-UKAWA na
wananchi wamemkubali ingawa CCM ilidhani umma ungemkataa kutokana na
kuchafuliwa kimkakati kwa ufisadi?
Wananchi
wanajiuliza kama Magufuli ni mwadilifu kuliko Lowassa na kwamba
CCM siyo inayonufaika na ufisadi unaofanywa na watumishi wa serikali
yake ni kwa nini CCM wamekataa kuandika Katiba Mpya inayotokana na maoni
ya wananchi ili kuweka misingi ya kikatiba kuziba mianya kwa
serikali ya chama chochote kuwa fisadi wa fedha na mali za wananchi?
Wananchi
wanajiuliza ni kwa nini CCM inahaha kumzuia Lowassa kuwa Rais wa
Jamhuri kama CCM haiogopi hatari ya kuachia chama kingine kuingia
madarakani wakati nchi haijaweka misingi ya kuzuia serikali kuwa fisadi
na hivyo wanaogopa kuwa serikali ya CHADEMA na UKAWA nayo itakuwa
fisadi kama ilivyokuwa serikali ya CCM?
Vile
vile wananchi wanajiuliza, kama Rais Jakaya Kikwete ambaye mwaka 2005
alipigiwa kampeni na CCM kuwa ni mwadilifu, kama anavyonadiwa
Magufuli sasa lakini kwa miaka 10 umaskini wa wananchi umeongezeka
–deni la taifa limeongezeka kila Mtanzania anatakiwa kulipa shilingi
800,000/-—je Magufuli atakuwa na ubavu gani wa kuifanya CCM na serikali
yake isiendelee kuwa fisadi?
Ni
kutokana na hoja hizi ndiyo sababu wananchi wengi wanaona kumchagua
Magufuli kuwa Rais wa Tanzania ni kuchagua ufisadi na ni kuchagua
mamilioni ya watanzania waendelee na umaskini. HAIKUBALIKI.
Tena
wakati mamilioni ya wananchi wanaendelea kuwa maskini watawala wa
serikali ya CCM, familia zao, wapambe wao kwenye kampeni na marafiki
zao wataendelea kujitajirisha kufuru na kwa kujigawia fedha na mali
zinazopaswa kunufaisha Watanzania wote.
Ndiyo
sababu wananchi sasa wanahamasishana kutambua kuwa kumchagua Magufuli
ni kuichagua CCM na ni kama kumpa tenda ya ulinzi mlizi mwizi!
Wananchi
wanaona ni afadhali kuichagua CHADEMA-UKAWA kwa sababu kwanza mgombea
wake wa Urais Lowassa huenda akaonyesha uadilifu na uchapakazi wa
hali ya juu kuwathibitishia Watanzania kwamba CCM amepakaziwa na
kutolewa kafara ufisadi ili CCM iendelee kubaki madarakani bila
kujulikana kwamba serikali yake ndiye malkia wa ufisadi nchini.
Wananchi
wanatambua kuwa kuirejesha CCM Ikulu kasi ya umaskini itaongezeka
kwa wananchi wengi kuaendelea kukosa kipato, kukosa elimu bure na bora
hadi chuo kikuu kuondoa adui ujinga na wizi, biashara chafu, uvunjifu
wa haki za binadamu na serikali kuwa mbabe, dikteta mminya
demokrasia vitaongezeka na hivyo kuvuruga amani ya nchi yetu.
Hivyo
ni muhimu serikali ya CCM ikaacha sauti na maamuzi ya wananchi isikike
katika uchaguzi mkuu tarehe 25 Oktoba 2015 ili endapo wananchi
wataamua kumchagua Lowassa kama Rais wao kupitia CHADEMA
inayowakilisha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA), waandike Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi na
wasipofanya hivyo uchaguzi wa 2010 wananchi wawanyang’anye madaraka.
Katiba
mpya siyo tu itampunguza madaraka ya Rais kuhusu uteuzi wa watendaji
ikiwa ni pamoja na majaji wa mahakama, bali pia itaweka misingi ambayo
mihimili mitatu ya utawala wa nchi —Serikali, Bunge na Mahakama
vitakuwa haviingiliani.
Kwa
hivyo serikali ya chama chochote ikiiingia madarakani na ikafanya
ufisadi itawajibishwa na wananchi nao wataacha na wizi na ujambazi wa
kutumia silaha kujitajirisha kama watawala wao wanavyoiba fedha za umma
kwa kutumia ujambazi wa kalamu.
Katiba
Mpya ya wananchi ikiandikwa, serikali ikifisadi fedha na mali za
wananchi itashtakiwa na majaji hawataogopa kuihukumu serikali bila
kuipendelea kwa sababu hawatakuwa na woga wa kupoteza ajira.
Hayo
ndiyo mabadiliko wanayotaka wananchi wa Tanzania katika kukomesha
ufisadi wa kimfumo ili kuepusha ongezeko la wananchi masikini wa kutupa
kunakohatarisha amani na umoja wa kweli katika nchi yetu.
Lakini
CCM na serikali yake vikitumia rushwa, ubabe na uchakachuaji katika
uchaguzi wa tarehe 25 na kushinda uchaguzi, tuendako serikali ya CCM
itafanya ufisadi mkubwa zaidi, tena ikitumia ubabe, udikteta na
dharau kubwa kwa vyama vya upinzani na wananchi kwa ujumla. Mungu
ibariki Tanzania.
Note: Ninaruhusu yeyote anayetaka kutumia , kuchapisha au kusambaza andiko hili afanye hivyo.
------******------------******---------------------*********______
Mwandishi wa makala hii ni Ananilea Nkya ambaye ni Mkurugenzi Mstaafu wa TAMWA.
Anapatikana anapatikana kwa E-mail:ananilea_nkya@yahoom.co
Post a Comment