KADA wa siku nyingi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru ‘ametoroka’ chama hicho kutokana na kile alichokieleza kimepoteza mwelekeo.
Akizungumza
na waandishi wa habari nyumbani kwake leo jijini Dar es Salaam Kingunge
amesema, hatojiunga na chama chochote cha siasa “lakini kuanzia sasa
mimi sio mwanachama wa CCM,” amesema.
Katika
mazungumzo yake na waandishi wa habari, neno ‘mabadiliko’ lilitawala
kinywa chake huku akionya kuwa, nguvu ya kupinga mabadiliko ni kubwa.
“Nguvu
ya kupinga mabadiliko ni kubwa sana lakini kwa utafiti wangu mimi mzee
ni kuwa, nguvu ya kuleta mabadiliko ni kubwa zaidi. Watu wajiamini zaidi
na wasubiri tarehe 25 Oktoba mwaka huu,” amesema.
Akielezea
namna CCM ilivyopoteza mwelekeo Kingunge amesema chama hicho kimelewa
madaraka kutokana na kutawala kwa muda mrefu na kuongeza kuwa ‘wananchi
sasa wanataka mabadiliko.”
Hata
hivyo, kiongozi huyo aliyejiunga na TANU siku saba baada ya kuanzishwa
kwake na baadaye TANU na ASP ya Zanzibar kuungana na kuanzisha CCM mwaka
1977 amesema chama hicho tayari kimeishiwa pumzi.
“Kuongoza
nchi ni kama kupanda mlima, utafika mahala pumzi zinakwisha na huwezi
kuendelea mbele na ukijaribu kwenda mbele unabaki pale pale, na hivi
ndivyo CCM ambapo kimeishiwa pumzi na kimebaki pale pale hakiwezi tena
kupanda mlima,” amesema Kingunge.
Baada
ya kutangaza uamuzi wa kujiondoa CCM, amesema hakusudii kujiunga na
chama chochote, Kingunge ameeleza kuwa alipigana ndani ya CCM kutaka
kuhakikisha chama hicho kinabaki salama kwa kumchagua ama kumpitisha mtu
aliye na sifa na kukubalika.
“Nilipigana
nikiwa ndani ya CCM kuangalia nani anafaa ili kuileta nchi kwenye
mstari. Niliangalia ili kujua ndani ya chama nani tukimpata anaweza
kuipeleka nchi mbio.
“Nilimwona
Edward Lowassa kuwa ana sifa kuliko wengi waliojitokeza. Kiongozi
lazima akubalike na watu, hii ni sifa tangu wakati wa TANU,” amesema Kingunge na kuongeza;
“Lowassa anakubalika ndani ya CCM na nje ya CCM, ni hivyo pamoja na kutangaziwa mambo ya ajabu kwa miaka minane mfululizo.”
Lowassa
ambaye alihama CCM na kujinga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), alipitishwa na chama hicho kuwania urais wa Tanzania kwenye
Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Chadema
ni miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)
ikiwa ni pamoja na Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.
Kabla
ya kujiunga na chama hicho, ndani ya Serikali ya awamu ya nne, Lowassa
aliwahi kuwa Waziri Mkuu ambapo alijiuzilu nafasi hiyo kutokana na
kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Pia Kingunge ameshngazwa na hatua ya CCM kutoa kauli zinazoonekana kung’ang’ania madaraka.
Amesema “kauli
zinazotoka sasa hivi, wapinzani hawawezi kushinda. Nyinyi mnajuaje kama
hawawezi kushinda? Ukiritimba wa chama kimoja kwa karne moja umetosha,
madaraka hulevya.”
Akizungumiza
chama tawala kuacha utamaduni wake Kingunge amesema chama hicho
kimeacha ‘itikio’ lake lililoasisiwa tangu kuanzishwa kwa chama hicho.
“Wamebadilisha kauli mbiu ya chama badala ya kidumu Chama Cha Mapinduzi – kidumu, sasa wanaitikia kidumu chama tawala,” anasema na kuongeza; “niliwaambia NEC kwamba ukisema hivyo maana yake wewe unataka kubaki kwenye utawala.”
Akimzungumzia
mgombea urasi wa CCM, Dk. John Magufuli, Kingunge amesema nafasi hiyo
ameipata kutokana na chama hicho kuvunja katiba ya chama.
Hata hivyo ameeleza kuwa, tatizo kubwa la wananchi ni uchumi na ajira, “umasikini uanondolewa na uchumi bora,” amesema.
Amesema,
Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliacha uchumi ukikua kwa
asilimia saba na kuingiza nchi kwenye orodha ya nchini zinazokwenda mbio
kiuchumi.
“Tazama,
Kikwete (Rais Jakaya Kikwete) kapokea uchumi ukikuwa kwa silimia saba
na sasa ni miaka 10 uchumi unakuwa karibu na asilimia saba -miaka 10 hii
yote tumepiga make time na kiukweli tumerudi nyuma. Mabadiliko ni
muhimu ili upate watu wengine wenye pumzi mpya,” amesema.
Post a Comment