Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za rambirambi na maombolezo kumlilia Mwenyekiti wa Chama cha Siasa cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye alipoteza maisha katika ajali ya gari iliyotokea alfajiri ya Jumapili, Oktoba 4, 2015, katika Kijiji cha Msolwa, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Chama cha DP, Rais Kikwete amesema: “
Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mwenyekiti wenu na
Mtanzania mwenzetu, Mchungaji Christoher Mtikila ambaye nimeambiwa
amepoteza maisha katika ajali ya gari Mkoani Pwani akiwa njiani kurejea
mjini Dar es Salaam akitokea kwao Njombe.”
“Kwa
hakika, kifo cha Mchungaji Mtikila ni pigo kubwa kwa Chama cha
Democratic Party ambacho kimempoteza kiongozi wake mkuu. Aidha, kifo
hicho ni pigo kwa medani za siasa katika Tanzania na kimetunyang’anya
mmoja wa viongozi hodari na wazalendo, aliyekuwa na msimamo thabiti na
usioyumba katika kutetea mambo ambayo aliyaamini katika maisha yake
yote,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Ni
jambo la kusikitisha pia kuwa tunampoteza Mchungaji Mtikila katika
kipindi cha mchakato muhimu wa kisiasa nchini ambako mchango wake
ulikuwa unahitajika sana. Hakika, tutamkosa mwenzetu katika uwanja wa
siasa za nchi yetu.”
Ameendelea Rais Kikwete,
“Nawatumieni nyie wana-democratic Party salamu za dhati ya moyo wangu
na pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi wetu mkuu, wa miaka mingi na
wenye uzoefu wa uongozi wa chama cha siasa.”
“Aidha
kupitia kwenu, napenda kuitumia pole zangu nyingi familia ya Mchungaji
Mtikila. Nawapa pole sana wanafamilia, ndugu na marafiki na napenda
wajue kuwa niko nao katika kipindi hiki cha majonzi ya kuondokewa na
mhimili wa familia. Naungana nao katika majonzi. Aidha, naungana nao
katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema roho ya
Mchungaji Christopher Mtikila. Amen”.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
04 Oktoba, 2015
Post a Comment