Mwakilishi
Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa MONUSCO, Bw. Martin Kobler akisisitiza
jambo wakati wa mazugumzo yake na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania,
Balozi Tuvako Manongi. Bw. Kobler alifika katika Ofisi za Uwakilishi wa
Kudumu, kuishukuru Tanzania kwa mchango wake wa ulinzi wa amani katika
Mashariki ya DRC. Mchango ambao amesema umeleta tofauti kubwa.
"Tafadhali
nifikishie salamu na shukrani zangu kwa Mhe. Rais, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Waziri wa Ulinzi" maneno ya Bw.
Martin Kobler kwa Balozi Manongi walipokuwa wakiagana baada ya
mazungumzo yao mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Maalum, New York
Ushiriki wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Misheni ya kulinda Amani
ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (
MONUSCO), kumeelezwa kutoa mchango mkubwa katika kurejesha hali ya Amani
na utulivu katika baadhi ya maeneo ya Mashariki ya nchi hiyo.
Hayo
yameelezwa mwishoni mwa wiki, na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa katika DRC na Mkuu wa MONUSCO Bw. Martin Kobler,
wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Tuvako Manongi, Mwakilishi wa
Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.
Bw.
Kobler na ambaye alitumia fursa hiyo kuaga na kuishukuru Tanzania
kwa ushiriki na mchango wake, amesema, katika maeneo mengi ambayo
walinzi wa Amani wa Tanzania wanayalinda hali ya Amani imerejea
kiasi ambacho wananchi waliokimbia vita wamerudi na kuendelea na
shughuli zako za kila siku.
“
Katika maeneo kwa mfano la Kamango ambako wapo wanajeshi wa
Tanzania, nilipowauliza wananchi wa eneo lile ni nini wanachotaka,
jibu lao lilikuwa moja tu, waliniambia wanataka amani na
usalama, wanaomba walinzi wa Amani wa Tanzania wasiondoke kwa
sababu wakiondoka hawana uhakika wa usalama wa maisha yao”
anasimulia Kobler.
Akasema mji
huo wa Kamango wenye wakazi wapatao 80,000 ambao ulikuwa magofu na
usiokuwa na watu, hivi sasa hali imebadilika, watu
wamerejea, mji umestawi biashara zimeshamiri na wananchi wanaendelea
na shughuli zao pasipo kuwa na mashaka ya usalama wao.
“
Ninazo simulizi nyingi kuhusu utendaji mzuri wa wanajeshi wenu, ni wazi
pia katika utekelezaji wa majukumu yao, wapo waliopoteza maisha, lakini
mchango wao na maisha yao hayakupotea bure wamefanya kazi nzuri.
Mimi
binafsi naomba unifikishie salamu zangu na shukrani zangu za dhani
kabisa kwa viongozi wako wakuu, Mhe. Rais Kikwete, Waziri wa Mambo
ya Nje na Waziri wa Ulinzi ambao sikupata nafasi ya kuwashukuru
mimi mwenyewe”. anasema Kobler.
Jeshi la
Wanachi wa Tanzania linahudumu katika Misheni ya
MONUSCO kupitia Force Intervention Brigade ( FIB) ambayo inaundwa na
wanajeshi kutoka Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi.
Mwakilishi
Maalum wa Katibu Mkuu, amesisitiza umuhimu na nafasi ya Afrika na
hususani Nchi za Maziwa Makuu wa kuhakikisha kwamba wanaendelea
kuisaidia DRC ili iweze kuwa na Amani ya kudumu.
Kwa
upande wake, Balozi Tuvako Manongi amemshukuru Bw. Martin Kobler
kwa kuwajibika katika pindi cha miaka miwili ya uwakilishi wake, na
mchango wake katika kujaribu kuwakutanisha wadau mbalimbali kwa lengo
la kuhakikisha Amani na utulivu unakuwapo katika DRC.
Akasisitiza
kuwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine inataendelea kusaidia kwa
kadri inavyowezekana na kwa kushirikiana na wadau wengine ili wananchi
wa DRC hususani mashariki mwa nchi hiyo na ambao kwa miaka mingi
wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na hatari wanakuwa na fursa
ya kuendesha maisha yao kwa Amani na utulivu.
Post a Comment