Uteuzi wa wakuu wa wilaya umepokelewa kwa hisia tofauti na wasomi na wanasiasa, ambao wamedai nafasi hiyo imekuwa kama kichaka cha kuwahifadhi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho .
Rais
Jakaya Kikwete juzi aliteua wakuu wa wilaya wapya 13 na wengine
kuwahamisha katika vituo vyao vya kazi zikiwa zimebakia siku 18 kabla ya
kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ambao wananchi watatumia
demokrasia yao kumchagua Rais mpya, wabunge na madiwani.Miongoni mwa
walioteuliwa wamo makada wa CCM ambao walichukua fomu ya kuwania ubunge
lakini wakaangushwa kwenye mchakato wa kura za maoni.
Walioangushwa
lakini wametueliwa kuwa wakuu wa Wilaya ni Richard Kasesera ambaye
anakuwa Mkuu wa wilaya Iringa. Kasesera aliangushwa kwenye kura za maoni
katika jimbo la Rungwe Magharibi mkoani Mbeya.
Wengine
ni Asumpta Mshama ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe
aliyeangushwa Jimbo la Nkenge, mkoani Kagera, Vita Kawawa ambaye
aliangushwa katika kura za maoni Jimbo la Namtumbo ameteuliwa kuwa Mkuu
wa Wilaya ya Kahama, Mrisho Gambo, ambaye aliangushwa Jimbo la Ilala
anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma.
Kufuatia
uteuzi huo, wasomi na wanasiasa wameuponda wakidai hakukuwa na maana
hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwani kufanya hivyo
ni kutumia vibaya fedha za umma.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Kitila Mkumbo, alisema
CCM imekuwa ikiwazawadia makada wake walioshindwa kwenye kura za maoni
za ndani ya chama kwa kuwapa ukuu wa wilaya ili kulipa fadhila.
“Ukuu
wa wilaya hauna maana kwa sababu imekuwa ni kama hifadhi ya kuwahifadhi
makada wa CCM walioshindwa kwenye kura za maoni za ndani ya chama,” alisema.
Naye
Rais Mtendaji wa Chama cha APPT Maendeleo, Peter Kuga Mziray, alisema
uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya katika kipindi hiki ambacho serikali ya
awamu ya nne imebakiza siku chache kuondoka madarakani ni matumizi
mabaya ya fedha za umma.
“Kinachoudhi
katika uteuzi huu ni kuteua wale waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani
ya CCM ina maana tuseme hiki cheo cha ukuu wa wilaya ni cha makada wa
CCM?,” alihoji.
Mziray
alisema kufanyika kwa uteuzi huo katika kipindi hiki ni sawa na
kumchagulia Rais mpya ajaye watu wa kufanya nae kazi wakati naye
atapanga safu yake ya uongozi na pengine walioteuliwa wanaweza
wasiteuliwe kwenye uongozi wa serikali mpya.
Alisema
kuna haja ya kwenda mahakamani kufuta zisiwapo nafasi ya mkuu wa wilaya
kwa sababu inaongeza gharama kwa taifa na pia imekosa maana kwa sababu
inakuwa kama vya kuwapeleka wanasiasa wa kukilinda chama tawala.
Kwa
upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi,
alisema kitendo cha Rais Kikwete, kufanya uteuzi huo kipindi hiki cha
kuelekea uchaguzi mkuu hakina mantiki bali ni kulipa fadhila ili
atakapoondoka madarakani asiwe na maadui.
Wengine
walioteuliwa ni Shaaban Athuman Ntanambe ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya
ya Chato, Thobias Mwilapwa Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Ruth Msafiri
(Kibondo) na Abdallah Njwayo ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa,
mkoa wa Lindi. Pia wapo Mohammed Mussa Utaly ambaye anakuwa Mkuu wa
Wilaya ya Mpwapwa, Daudi Yasin (Makete), Honorata Chitanda (Ngara),
Christopher Ng’ubyagai, (Mkalama), Hawa Ng’humbi ( Kishapu).
Wakuu
wa wilaya waliohamishwa vituo vya kazi ni Fadhili Nkurlu ambaye anatoka
Mkalama kwenda wilaya ya Arusha, Wilson Nkambaku amehamishiwa Arumeru
kutoka Kishapu, Francis Miti anahama wilaya ya Hanang kwenda Monduli,
Jowika Kasunga anahamia wilaya ya Mufindi kutoka Monduli, Muhingo
Rweyemamu kutoka wilaya ya Makete kwenda Morogoro; Hadija Nyembo
anahamia wilaya ya Kaliua kutoka Uvinza na Benson Mpyesya anahamia
wilaya ya Songea kutoka Kahama.
Post a Comment