Ofisi hiyo, kwenye chumba cha choo.
DAR ES SALAAM: Hii ni kali ya mwaka! Mwenyekiti na Wajumbe wa Mtaa wa Mkwajuni Kata ya Kigogo, jijini Dar wamejikuta wakihamishia ofisi yao kwenye choo baada ya kushindwa kulipa kodi katika jengo walilokuwa wamepanga tangu mwaka 2006.
Mweneyekiti waSerikali ya Mtaa, Herman Protas Kawele.
Nguzo ya Bendera ikichimbiwa ofidini hapo.
“Cha kushangaza mpaka tumehamia hapa hatujui mtendaji wetu wa mtaa yuko wapi na nikimpigia simu wakati mwingine inaita tu bila kupokelewa, tulihamia hapa Februari 8, mwaka huu baada ya kukosa pa kwenda tukaona jengo la serikali ambalo liko wazi ni hiki choo na shule ya sekondari tu.
“Tuko hapa tunapigwa na jua, mvua yetu hiki choo kilijengwa na serikali hivyo kwa upande wa wanawake huku hakikuwahi kutumika maana wakazi wengi wa hapa wana vyoo vyao majumbani, kwa upande wa wanaume kinatumika.
“Tunaomba serikali iangalie mfumo wa watendaji wa mitaa kwani wanatuumiza sisi wenyeviti kwa sababu wapo kimasilahi zaidi siyo kwa kuihudumia jamii,” alisema Mwenyekiti Herman.
Pia aliiomba serikali iwape kibali cha kujenga ofisi pembeni mwa choo hicho kwani kuna nafasi ili kuepukana na adha ya kupanga nyumba za watu kwa sababu wananchi wa eneo hilo wako tayari kuchangia ujenzi huo.
“Niliitisha mkutano wa hadhara na wananchi waliafikiana kwamba kila nyumba itoe elfu mbili za kuchangia ujenzi hivyo muhtasari wa kikao pia niliupeleka kwa afisa mtendaji wa kata bado tunaomba tu kibali cha serikali kwa ajili ya eneo hilo la kujenga, maana kila mwezi manispaa inatoa kodi elfu thelathini na pale tulipokuwa kodi ilikuwa elfu sabini hivyo tulikuwa tukiongezea fedha zetu za posho ya kila mwezi ili kuweza kulipa kodi,” alisema mwenyekiti.
Baada ya paparazi wetu kushuhudia wajumbe na mwenyekiti wakifanyia kazi nje na mafaili kuhifadhiwa ndani ya choo, alimtafuta Afisa Mtendaji wa Kata, Salum Mzee ambaye alikuwa na haya ya kusema;
“Shida ipo kwa mwenyekiti kwani alikuwa na mgogoro na yule mwenye nyumba nikaenda kuwasuluhisha yakaisha lakini kwa maamuzi yake aliwachukua na walio chini yake na kuhamia huko chooni.
“Suala la kujenga ofisi nilimwambia inahitaji kufuata utaratibu kwani hawezi kuvunja sheria kwa tabia yake binafsi kwa sababu suala la kujenga lazima upitie kwenye ngazi mbalimbali ikiwemo kuandika barua kwa mkurugenzi na maafisa wa ardhi waidhinishe, zoezi la kuwachangisha wananchi nililisitisha.”
Post a Comment