Aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Rajabu Rutengwe
Baadhi ya wasomi wamedai kumshangaa na wengine kueleza changamoto zinazowakabili wanaotaka kujiajiri.
Baada ya kutoswa kwa Dk Rutengwe ambaye amebobea katika masuala ya utafiti ‘alimpigia magoti’ Dk Magufuli akikiri kushindwa kuendana na kasi yake ya ‘Hapa Kazi Tu’ na kumuomba amkumbuke kwa maelezo kuwa kitendo cha kutoteuliwa kimemuacha njia panda na ana familia kubwa inayomtegemea.
Kauli ya msomi huyo aliyoitoa wakati akimkabidhi ofisi Mkuu mpya wa Mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe ilizua mjadala mkali katika vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii.
Mmoja wa wananchi katika mtandao wa kijamii wa facebook aliandika: “Hivi kweli daktari hana pa kwenda? Dk Rutengwe ana shahada ya uzamivu katika masuala ya usalama wa chakula na teknolojia kutoka Chuo Kikuu cha Vaal, Afrika Kusini lakini leo anasema hana pa kwenda?. Mbona siasa inatufanya kuuza utu wetu kwa kiasi hiki? Ina maana hadi umri huu alikuwa hajajiandaa kimaisha hadi aje kulialia kwa Magufuli amhurumie?”
Mwananchi mwingine katika mtandao wa Jamii Forum aliandika :“Anamuomba Dk Magufuli amhurumie kama vile anaomba sala ya toba eti anasema ‘Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana.”
Licha ya kauli hizo, wapo baadhi ya watu waliomtetea na kutaka hoja alizozitoa kuchambuliwa na kufanyiwa kazi kwa maelezo kuwa yapo ya kweli aliyoyaeleza.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema si lazima mtu aliyesoma awe ameelimika.
“Unaweza kuelimika lakini ukawa hujasoma kwa kiwango kikubwa na unaweza ukasoma kwa kiwango cha juu lakini usielimike. Huyu bwana (Dk Rutengwe) amebobea katika utafiti anaweza kufundisha au kuwa mshauri,” alisema Dk Bana.
Akimtolea mfano Rais mstaafu wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad aliyerejea darasani kufundisha, Dk Bana alisema anashangazwa kuona Dk Rutengwe akihaha kutafuta ajira wakati anaweza kuitumia elimu yake kuendesha maisha yake.
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Richard Mbunda alisema tatizo linaloikabili nchi ni kuwa na mfumo mbovu wa ajira ambao huwakumbatia hata wanaotaka kujiajiri.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala aliungana na Mbunda na kusisitiza kuwa hata mtu akiamua kukopa benki ili kupata mtaji, anakumbana na riba kubwa huku akitakiwa kutimiza masharti lukuki ambayo wengi huwashinda.
Dk Rutengwe anena
Wakati wasomi wakikosoa mfumo wa ajira nchini na wananchi wakimponda, Dk Rutengwe, jana alilieleza gazeti hili kuwa kwa sasa hana mpango wa kuajiriwa na amejikita katika kilimo cha mboga wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Akizungumza huku akiwa shambani kwake Bagamoyo, Dk Rutengwe alisema, “Yaani kama ungeniona hapa shambani usingeamini, nipo katika bustani kubwa nalima nyanya, pilipili, bamia na mbogamboga.
Pia nina kitalu cha miembe na asubuhi (jana) nilikuwa nalisha mifugo.” Alisema kwa sasa hafikirii tena kuajiriwa na kusisitiza kuwa anataka kujikita kwenye kilimo kwani hiyo ndiyo taaluma yake.
Post a Comment