JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
 |
Ndugu Wanahabari, tukiwa tunaelekea sikukuu ya pasaka, Serikali ya Mkoa wa Dodoma imeona ni vyema ikakutana na wawakilishi wa vyombo vya habari hapa Mkoani Dodoma, ili kupitia vyombo vya habari, tupate fursa ya kuweka wazi kwa wananchi wa Dodoma na watanzania kwa ujumla masuala ya msingi ambayo yamejiri hapa Mkoani Dodoma.
Awali, usiku wa kuamkia jana kuna tukio tunaloweza kuita la ujambazi lilitokea kama majira ya saa 8 usiku ambapo kundi la watu takribani saba (7) ambao bado hawajafahamika walivamia ofisi za Halotel Mkoani Dodoma kwa lengo la kutaka kufanya uhalifu ambapo waliwavamia askari wawili waliokuwa wakilinda Ofisi hiyo, ambapo pamoja na athari nyingine zilizojitokeza; walipora silaha aina ya SMG na kumjeruhi askari mmoja ambaye alilazwa kwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuruhusiwa jana hiyohiyo.
Hadi hivi sasa Jeshi la polisi Mkoa wa Dodoma linaendelea kulifanyia kazi suala hilo ambapo hadi tunavyozungumza sasa tayari silaha hiyo iliyoporwa imeshapatikana, uchunguzi zaidi wa suala hilo unaendelea kubaini watu wote waliohusika. Kufuatia suala hilo, Serikali ya Mkoa wa Dodoma, kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana anapenda kutoa tamko lifuatalo:
· Kwanza kabisa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana analaani vikali tukio hilo la uhalifu na kuwa halivumiliki na halikubaliki katika Mkoa wa Dodoma na Mikoa mingine hapa nchini na amewataka wananchi wema kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Dola ili kuwabaini wahusika na kukomesha matukio kama hayo.
· Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana analiagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanafanya uchunguzi na kuwabaini wale wote waliohusika katika tukio hilo la uhalifu,ili kuwatia mbaroni na kuwachukulia hatua kali za kisheria. Aidha amelitaka jeshi la polisi kujipanga vizuri na kuhakikisha kuwa tukio hili ni la mwisho na halijitokezi tukio jingine la aina hii.
· Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Jordan Rugimbana ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama kuna dalili zozote za kuwepo kwa uzembe wa aina yoyote kwa askari hao waliokuwa wanalinda Ofisi hiyo, na endapo itabainika kulikuwa na uzembe basi Jeshi la polisi lichukue hatua kali kwa askari hao waliohusika.
|
on Sunday, March 27, 2016
Post a Comment