Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo amesema kuwa kwa Tanzania kutopatiwa fedha na Marekani kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Changamoto za Milenia (MCC) ambazo ni Dola za Marekani milioni 472 kwa ajili ya miradi ya barabara, maji na umeme hazitaathiri miradi ya usambazaji umeme vijijini inayofadhiliwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Aliyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akifanya majumuisho ya vikao vyake na wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini ambavyo vilianza tarehe 29 Machi, 2016 na kuhudhuriwa na watendaji wa Wizara, Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) na REA.
Profesa Muhongo alisema kuwa fedha hizo zilikuwa haziendi moja kwa moja katika mfuko wa REA wala serikali kuu kama inavyodaiwa na watu wengi.
“Zile fedha za MCC tulikuwa tunakaa na MCC, tunasema bwana katusaidie kusambaza umeme mfano Shinyanga, kwa hiyo anachukua zile fedha zake anaenda na wakandarasi wake moja kwa moja Shinyanga, huku miradi ya REA ikiendela kama ilivyopangwa, ”alisema Profesa Muhongo.
Alisema kuwa miradi ya MCC ilikuwa ikisaidia juhudi za serikali katika kusambaza umeme vijijini na mijini lakini fedha hizo zilikuwa hazipelekwi REA.
Alisisitiza kuwa kabla ya MCC kuanza kutoa fedha za kuendeleza miradi ya umeme, serikali tayari ilikwishaanza kusambaza nishati hiyo kwa wananchi na kwamba kuna wadau mbalimbali wanaochangia miradi hiyo na hata kama wasipochangia, jukumu la serikali la kuwasambazia wananchi wake umeme linabaki kuwa pale pale.
“Isichukuliwe kwamba fulani asipochangia, sasa taifa zima miradi yake imekufa, hivyo dhana ya kusema kwamba fedha hizo zilikuwa zinapelekwa REA ni upotoshwaji wa hali ya juu, kwamba REA itaathirika kwa kukosa hizo fedha si kweli,”alisema Profesa Muhongo.
Akielezea utekelezaji wa miradi ya REA awamu ya pili, Profesa Muhongo alisema awali jumla ya shilingi bilioni 881 zilitengwa lakini zikaongezeka shilingi bilioni 60 ambapo hadi kukamilika kwa awamu hiyo ya pili jumla ya vijiji 2500 vinatarajiwa kupata umeme, huku wateja wa awali 250, 000 kuunganishwa na huduma hiyo hadi kufikia mwezi Juni, mwaka huu ambao ni ukomo wa utekelezaji wa awamu hiyo.
Kuhusu tathmini ya wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini, Profesa Muhongo alisema kuwa wakandarasi wengi wametekeleza miradi hiyo kwa asilimia kati ya 75 na 85, huku wengine wakivuka wastani wa REA ambao ni asilimia 87.
Katika hatua nyingine, Profesa Muhongo alitoa miezi miwili kwa wakandarasi ambao hawajakamilisha miradi na kusisitiza miradi yote kukamilishwa mwezi Mei au Juni 15, mwaka huu kabla ya kuanza kwa awamu ya tatu inayotarajiwa kuanza ifikapo Julai mosi mwaka huu.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, serikali imebaini kuwa wapo wakandarasi wanaotumia vifaa hafifu kama transfoma na nguzo na kusisitiza ukaguzi kufanyika na kampuni itakayobainika kutumia vifaa hafifu itafutwa mara moja kabla ya awamu ya tatu.
Ili kutekeleza miradi hiyo kwa ufanisi, Profesa Muhongo aliitaka TANESCO kwa kushirikiana na Wizara kuhamasisha wananchi hasa waishio vijijini kujiunga na huduma ya umeme, na TANESCO kusogeza huduma karibu na wananchi ili kuepusha wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya kuunganishiwa umeme au changamoto nyingine zinazotokana na nishati hiyo.
Akizungumzia kuhusu malipo ya wakandarasi hao, Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imeendelea kulipa wakandarasi wote kwa wakati kulingana kazi zinazofanyika.
Wakati huo huo Profesa Muhongo alisema kuwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I kwa sasa inazalisha Megawati 150 na kuongeza kuwa malipo kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya Kinyerezi II inayojengwa na kampuni ya Sumitomo kutoka nchini Japan yameshakamilika
Post a Comment