Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa nchini (Alat), wanaotokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamesusia uchaguzi kwa madai ya kuminywa kwa demokrasia.
Mkutano huo uliofanyika jana katika ukumbi mpya wa CCM mjini Dodoma, wajumbe wake ni wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri zote, mameya wa miji na majiji na mbunge mmoja kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara.
Nafasi zilizokuwa zikigombewa ni mwenyekiti, makamu wake na wajumbe 16 wa kamati ya utendaji.
Awali, Mwanasheria wa Alat, Cleofas Manyangu aliwataja waliochukua na kurejesha fomu za kugombea uenyekiti ni Gulam Mukadam (Meya wa Shinyanga), Murshid Ngeze (Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bukoba Vijijini), Chief Kalumuna (Meya wa Bukoba Mjini) na Isaya Charles (Meya wa Jiji la Dar es Salaam).
Hata hivyo, alisema waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba ya Alat, kanuni za kudumu na mwongozo ni Mukadam na Ngeze wote kutoka CCM na waliosalia wa Ukawa hawakukidhi.
Alisema Charles na Kalumuna walishindwa kurejesha fomu katika muda uliowekwa wa saa 6.00 mchana siku moja kabla ya uchaguzi na pia hawakupata wadhamini 10 kutoka kanda tano za Alat Taifa.
Kutokana na kauli ya mwanasheria huyo, mwenyekiti wa muda wa mkutano huo ambaye pia ni Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jaffar Mwanyemba alitangaza kuwa wagombea katika uchaguzi huo ni wawili.
Kauli hiyo ilibadilisha hali katika ukumbi, huku wajumbe wa Ukawa wakitaka wagombea wote waruhusiwe kuingia katika kinyang’anyiro hicho.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro aliomba wagombea hao waruhusiwe kwa kuwa maandalizi ya uchaguzi yalikiuka mwongozo, hali ambayo ilifanya baadhi yao kutokidhi vigezo.
Alisema taarifa ya mkutano huo ilitakiwa kuwafikia siku zisizopungua 28 kabla ya uchaguzi, lakini wengi wao walipata barua hizo chini ya muda huo.
Akijibu hoja hizo, Manyangu alisema taarifa za mkutano huo kwa mara ya kwanza zilipelekwa kwenye halmashauri Novemba 2, mwaka jana.
“Tatizo lililotokea ni baadhi ya halmashauri kuchelewa kukamilisha uchaguzi, hali iliyosababisha mkutano kuahirishwa mara mbili,” alisema.
Baada ya hoja hizo, wajumbe wote wanaotokana na Ukawa walitoka nje ya ukumbi, huku wakiahidi kufanya kazi na Serikali Kuu pekee.
Akizungumza nje ya ukumbi, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Charles alisema kutokana na kuchelewa kwa uchaguzi jijini humo hakupata taarifa mapema kuhusu mkutano na uchaguzi huo.
Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe na meya wa Manispaa ya Kigoma walishiriki uchaguzi kama kawaida.
“Mimi sijui chochote. Sijui wametoka kwa sababu gani maana nimefika hapa nikiwa nimechelewa,” alisema Zitto.
Katika uchaguzi huo, Mukadam alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kura 179 kati ya 276 na makamu wake ni Stephen Muhapa aliyepata kura 152 kati ya 272.
Post a Comment