Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

BAVICHA WALAANI HOTUBA YA LEMA KUZUIWA BUNGENI


Wakati uchunguzi wa kampuni ya Lugumi inayodaiwa kushindwa kutekeleza mradi wa utambuzi wa vidole kwenye vituo vya polisi ukiendelea, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) limemtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Charles Kitwanga kujiuzulu wadhifa wake kupisha uchunguzi huo.

Limesema haiwezekani waziri anayetajwa kuhusika katika sakata hilo kuendelea na kazi huku Jeshi la Polisi linalodaiwa kutapeliwa na kampuni hiyo likiwa chini ya wizara yake.

Hata hivyo, waziri huyo amewajibu vijana hao wa upinzani kwa kusema hawezi kubishana na watoto na hayo waliyoyatoa ni mawazo yao binafsi wana haki ya kuyasema.

“Nimeshasema mara nyingi, siwezi kuzungumza tena kuhusu haya mambo. Wao kama wamesema waache waseme,” alisema.

Baraza hilo lililoibuka na hoja tatu jana, limesema kama waziri huyo atagoma kujiuzulu kupisha uchunguzi unaofanywa na kamati ndogo ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Rais John Magufuli anapaswa kumwajibisha ingawa suala hilo ni gumu kutokana na uswahiba uliopo kati ya kiongozi huyo mkuu wa nchi na Kitwanga.

Kampuni ya Lugumi ilibainika kutotimiza matakwa ya mkataba wake baada ya kufunga mashine 14 tu kati ya 108 zilizotakiwa kufungwa, licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha kwa mujibu wa mkataba ambazo ni Sh37 bilioni.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2013/14 ndiyo iliyofichua udhaifu huo na baadaye Bunge kuanza uchunguzi baada ya kutoridhishwa na maelezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani na polisi kuhusu mkataba huo.

Kitwanga anahusishwa na Lugumi kupitia kampuni ya Infosys anayodaiwa kuwa ni mmoja wa wanahisa. Infosys ambayo imekanusha kuhusika katika sakata hilo, imedaiwa kuwa iliisaidia kampuni ya Lugumi kupata vifaa kutoka kampuni ya Dell ya Marekani ili viweze kufungwa kwenye vituo vya polisi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Bavicha, Julius Mwita alisema: “Hotuba ya upinzani inaeleza kuwa Lugumi inamilikiwa na Kitwanga na ana ubia hilo siyo siri. Kilichoelezwa kama kingesomwa bungeni kingemfanya apoteze uhalali wa kuwa waziri na tunajua Magufuli hawezi kumfanya chochote maana ni maswahiba.

“Hotuba ile pia ilimtaja Rais ila cha ajabu upinzani wakaambiwa wafute maneno ‘rais’. Rais Magufuli ameshindwa kuitumbua Lugumi na kwa kilichotokea bungeni suala hilo haliguswi.”

Alisema Rais anapaswa kujibu hoja zilizotolewa na wapinzani kuhusu Lugumi na kubainisha kuwa kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza kampuni hiyo haiwezi kutenda haki wakati Kitwanga akiendelea kuwa waziri.

Katibu mwenezi wa baraza hilo, Edward Sembeye alisema: “Katika ripoti ya CAG ameeleza juu ya ununuzi wa ile feri kuwa ni mbovu na haifanyi kazi hivi hili siyo jipu?

Kuhusu suala la Jaji Mkuu, Mwita alisema kitendo cha kuisifia Sheria ya Mtandao alipokuwa London, Uingereza hivi karibuni si kizuri kwa maelezo kuwa kazi ya majaji ni kutafsiri misingi ya kikatiba:“Tunamtaka afute kauli hii na aseme sheria hiyo imetungwa itumike lakini uzuri na ubaya wake hapaswi kuusema maana ni kama anatoa hukumu kabla watuhumiwa hawajafikishwa mahakamani.”
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top