Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MAKONDA AELEZA KWANINI ALIENDA MSIBANI KWA KABWE LICHA YA VITISHO VINGI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiweka vizuri shada la maua kwenye jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe katika Viwanja vya Karimjee wakati wa kutoa heshima za mwisho kabla ya kuusafirisha kwenda katika Kijiji cha Mamba, Same mkoani Kilimanjaro kwa maziko.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema licha ya kupewa vitisho kumzuia asihudhurie msiba wa aliyekuwa mkurugenzi wa jiji, Wilson Kabwe, amezingatia ubinadamu na kuweka msimamo kuwa ataendelea kutimiza wajibu wake.

Makonda alisema hayo jana wakati wa kuaga mwili wa Kabwe kwenye ukumbi wa Karimjee, kabla ya kusafirishwa kwenda kijijini kwake Mamba Mpinji wilayani Same, Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayofanyika leo.

Awali, mmoja kati ya wanafamilia alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa familia haihitaji ushiriki wowote wa Serikali kwenye maandalizi ya mazishi hayo.

Alitoa kauli hiyo kutokana na Kabwe kusimamishwa kazi kwa amri ya Rais John Magufuli baada ya kusomewa makosa yake na Makonda mbele ya umati wa watu wakati wa uzinduzi wa Daraja la Kigamboni.

Hata hivyo, ndugu wengine walikanusha kauli hiyo na kueleza kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na familia katika kumuuguza Kabwe na kwamba kifo chake hakikutokana na kusimamishwa kazi kwa kuwa wakati uamuzi huo unatangazwa alishaanza kuugua.

Akizungumza kwenye shughuli hiyo, Makonda aliipongeza familia ya marehemu, akisema imevuka mtihani ambao Watanzania wengi wangeshindwa kutokana na kulivisha tukio hilo sura ya tofauti wakati wa msiba.

“Baadhi ya watu waliniambia nisihudhurie msiba na hata baadhi ya vyombo vya habari vikatengeneza mazingira vinayoyaona kwamba yanafaa,” alisema Makonda.

“Ila nitaendelea kutimiza wajibu wangu na wanafamilia mmeliona hilo na niwape pongezi.”

Makonda aliwasihi Watanzania kuwa watulivu na kushauri watumishi wa umma kuwa waadilifu katika kazi zao.

“Maadam Kabwe amelala, tusitumie fursa hii kumrundikia mizigo eti tukifikiri kwamba tutakuwa salama mbele za Mungu. Tuhakikishe kila mmoja anafanya kwa nafasi yake na kwa wajibu wake ili tusiwatwishe mizigo watu waliotangulia mbele za haki.”

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi za kidini, wafanyakazi wa umma na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi.

Akitoa salamu za Rais, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema kifo cha Kabwe kimewasikitisha na kwamba ameacha pengo, si kwa familia pekee bali hata serikalini.

Simbachawene alisema Kabwe amekuwa mtumishi wa umma kwa miaka 37 na kwamba yapo mengi aliyoyafanya, mazuri na mabaya lakini kwa sasa yakumbukwe yale mema na kuyaendeleza.

“Rais (Magufuli) na Serikali tunatambua mchango mkubwa alioutoa marehemu (Kabwe) katika utumishi wake kwa miaka 37, tunaahidi kuyaendeleza yale yote aliyoyaacha,” alisema Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Kibakwe (CCM) mkoani Dodoma
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top