Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

NAPE ASULUBIWA .. AITWA WAZIRI LUMBESA (MZIGO)


Wabunge wamemcharukia Waziri wa Habari, Nape Nnauye kwamba aliwahi kuwaita mawaziri wa Serikali iliyopita mizigo, lakini yeye amezuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, ili wananchi washindwe kumpima kama ni mzigo au lumbesa. 

Hayo yalijitokeza jana wakati wabunge walipochangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari kwa mwaka 2016/2017, iliyowasilishwa bungeni na Waziri Nape. 

Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) alieleza kushangazwa na hatua ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhimiza wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa, lakini haitaki wananchi waone inavyopanga matumizi yake. 

Alisema Nape akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, aliwaita baadhi ya mawaziri ni mizigo, lakini amepewa wizara hiyo amezuia mijadala ya wazi ambayo ingesaidia wananchi kumpima.

“Nilipoona amepewa wizara ya habari nikajua ataruhusu mijadala ya wazi ili tumuone yeye kuwa hatakuwa mzigo, lakini yeye akawa lumbesa. Hilo amelizuia kwa hiyo tunashindwa kumpima,” alisema. 

Alisema waziri huyo hawezi kukwepa lawama ya hicho kinachoendelea cha kuzuia matangazo ya Bunge, kwa vile wanaopiga picha na kuhariri taarifa zinazorushwa ni watumishi wa TBC. 

Udhibiti wa Bunge 
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (Act-Wazalendo), alisema kuwa wabunge wote waliopinga Bunge kutoonyeshwa ‘live’ na kusababisha mtafaruku bungeni, wameitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge. 

“Wabunge hapa tulisimama tukapinga na wapo waliounga mkono, lakini kiti chako kimetuita wabunge wote tuliopinga kauli ya Serikali kwenye kamati ya maadili. Jana mimi nimepata barua,” alisema Zitto. 

“Kwamba mnatubana kusema. Mnazuia Bunge lisionekane. Hata kutoa maoni ndani ya Bunge tunakwenda kuhojiwa? TBC ni chombo cha umma, siyo chombo cha Serikali, inaendeshwa kwa kodi za wananchi,”alisisitiza. 

Baada ya mchango huo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson alisema si kweli wabunge hao wanahojiwa kutokana na michango yao, bali wanahojiwa kutokana na mambo waliyoyafanya kwa kutotii maagizo ya kiti wakati wa mjadala wa ‘Bunge Live’. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), aliunga mkono hoja ya Zitto ya kuifanya TBC iendeshwe kama inavyoendeshwa BBC kwa kupewa  leseni maalumu. 

Pia, aliitaka Serikali kupeleka muswada bungeni utakaowabana wamiliki wa vyombo vya habari kuwa na mikataba na waandishi wanaowaandikia, pia, akadai baadhi ya vyombo haviwalipi waandishi wake. 

Hata hivyo Mbunge wa Viti Maalumu, Agness Marwa (CCM) alitetea uamuzi wa Serikali kuondoa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, akisema wabunge wanaodai hilo ni wale waliokuwa wakiuza sura. 

Katika hatua nyingine, Waitara alisema kitendo cha Nape kuwaalika wabunge kwenye muziki, baada ya bajeti yake kupita ilikuwa ni kuwahonga. 

Juzi jioni wakati akitoa matangazo kabla ya kuahirisha Bunge, Naibu Spika alisema baada ya kupitisha bajeti ya Wizara ya Habari, wanamuziki Diamond Plutnum na King Kiki watatumbuiza katika viwanja vya Bunge. 

“Mnaposema mnabana matumizi hao wanamuziki wameletwa kwa gharama za nani,” alihoji mbunge huyo.

 “Wabunge wote ambao wataenda katika hiyo miziki ili kuunga mkono habari ya Nape mtakuwa mmekula rushwa,” alisisitiza Waitara, kauli ambayo ilimfanya Naibu Spika, Dk Tulia kufafanua, akisema suala hilo lilitangazwa bungeni kama mengine, lisiingizwe kosa la jina la rushwa. 

Upinzani na udikteta 
Msemaji mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Joseph Mbilinyi, alisema kitendo cha Serikali kuminya uhuru wa habari ni kuelekea kwenye udikteta.

 “Kana kwamba haitoshi, Serikali sasa imezuia Televisheni ya Umma, inayoendeshwa na kodi ya wananchi (TBC1) kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mijadala inayofanyika bungeni. Dalili hizi siyo njema kwa ukuaji wa demokrasia na uhuru wa habari hapa nchini na zinatoa taswira ya utawala wa ki-dikteta,” alisisitiza. 

“Tunaitaka Serikali kuliomba radhi Bunge hili, kwa kosa la kuminya uhuru wa habari kinyume na Katiba na kuviacha vyombo vya habari hususan vya umma kufanya kazi zao za kuhabarisha umma kwa uhuru,”alisema.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top