Hatimaye mjane aliyemwaga machozi mbele ya Rais John Magufuli akidai kudhulumiwa mali ya urithi, amepewa nyumba na shamba baada ya Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Crispin Meela kusuluhisha mgogoro wa umiliki wa mali hizo.
Hivi karibuni akiwa mjini Babati, Rais Magufuli alimuagiza Meela ahakikishe mjane huyo, Mwanaidi Mussa anapewa mali zake ikiwamo nyumba na shamba zilizokuwa zinadaiwa kuchukuliwa na mke mdogo kinyume cha sheria.
Meela alimkabidhi nyumba na shamba la ekari 2.5 mjane huyo juzi na kuagiza mke mdogo kama hakuridhika na uamuzi, akakate rufaa mahakamani.
Meela pia aliwataka wananchi kuacha kurubuniwa na watu wachache wenye maslahi binafsi na badala yake wafuate maelekezo yanayotolewa na vyombo vya sheria.
“Migogoro ya mirathi imeendelea kukithiri katika maeneo mengi nchini kutokana na watu kutofuata sheria za mirathi na wengine wakitaka kunufaika na mali zinazoachwa na marehemu,”alisema Meela.
Mwanaidi ambaye amezeeka, alidai kwa muda mrefu amewaomba viongozi wa Serikali ya mtaa anaoishi wamsaidie, kutatua tatizo lake lakini walimpuuza.
Mke mdogo, Asia Musa alidai kuwa nyumba hiyo aliyokabidhiwa Mwanaidi, aliijenga na mumewe kauli ambayo ilikinzana na ya mke mkubwa aliyedai kuwa wakati Asia anaoelewa alikuta nyumba ameshaijenga na mumewe.
Post a Comment