Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

RAIS MAGUFULI AWAGEUKIA WAKANDARASI ... AKEMEA VITENDO VYA RUSHWA NA KUWATAKA WAWE WAZALENDO KWA TAIFA LAO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakandarasi kote nchini kufanya kazi kwa kutanguliza maslai ya taifa, badala ya kutaka kupata faida kubwa kupita kiasi kutoka kwenye zabuni za miradi ya ujenzi wanayopata kutoka serikalini.

Dkt. Magufuli amesema hayo leo tarehe 26 Mei, 2016 alipokuwa akifungua mkutano wa mashauriano wa bodi ya usajili wa wakandarasi kwa mwaka 2016 unaofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es salaam.

Rais Magufuli amesema serikali yake ipo tayari kuwapa kipaumbele wakandarasi wa Tanzania pale inapotangaza zabuni za miradi ya ujenzi, lakini amewataka kujirekebisha kwa kupanga viwango vinavyostahili vya gharama za ujenzi wa miradi hiyo ambavyo serikali itaridhika.

“Nawatolea mfano, idara ya mahakama imetangaza kujenga mahakama za mwanzo na za wilaya, kwenye bajeti wana shilingi bilioni 24, makadirio ya kitaalamu yanaonesha kila jengo lisizidi shilingi milioni 200, wakandarasi wazalendo walipoomba katika nyaraka zao wametaka jengo moja lijengwwe kwa shilingi bilioni 1 na milioni 400, sasa nakuuliza Mheshimiwa Mwenyekiti na ndugu wakandarasi, hata kama una upendeleo, upendeleo huo utapasua moyo.

“Hata kama utakuwa na upendeleo kiasi gani kwa wazalendo utashindwa, sasa mimi niwaombe ndugu zangu wakandarasi, pamoja na nia nzuri ya serikali kuwasaidia wakandarasi wazalendo ni lazima na ninyi muwe na nia nzuri ya kuisadia nchi” Amesema Rais Magufuli

Pamoja na hilo, Rais Magufuli ametaka wakandarasi hao kuacha kutoa rushwa kwa watendaji wa serikali pale wanapoomba zabuni za ujenzi na badala yake amewataka kutoa taarifa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) ili watendaji hao wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Mimi niwaombe wakandarasi, msikubali kutoa rushwa, na muwafichue watendaji wanaoomba rushwa, atakapokuomba wewe rushwa hujui amewaomba wangapi, na utakapotoa rushwa huna hakika kama ile tenda utaipata, wengine wameishia kutoa rushwa hapa, rushwa hapa, rushwa hapa mpaka anafilisika, kazi huipati na rushwa umeitoa”Amesisitiza Dkt. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli ametoa wito kwa wakandarasi hao kujipanga ipasavyo ili waweze kupata zabuni katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi itakayofanywa hapa nchini ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga hapa Tanzania, Ujenzi wa Reli ya Kati na Ujenzi wa Viwanda.

“Sina uhakika kwamba mmejipangaje wakandarasi wa Tanzania katika kuhakikisha hiyo kazi mnaipata ya kujenga bomba kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga.

“Nitasikitika sana kilometa zote 1,410 pasiwepo mkandarasi hata mmoja wa kutoka Tanzania, wenzetu wanajipanga, na ninavyoona wakandarasi wa Tanzania wameendelea sana, lakini nashindwa kuelewa kuna tatizo gani linatufanya kutojua changamoto zinazotukabili, tumejipanga kujenga reli ya kati (Standard Gauge) kwenye bajeti ya mwaka huu tunaanza na kilometa 100, lakini kuna fedha nyingine zitatolewa na serikali ya China, tutajenga zaidi ya kilometa 1,200 (Standard Gauge, Central Corridor) itakayounganisha Mwanza, Kigoma, Burundi na Rwanda. Wakandarasi wa Tanzania mmejipangaje? " ameuliza Rais Magufuli.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Kamishna Valentino Mlowola ambaye amesema Taasisi hiyo ipo tayari kukabiliana na rushwa iliyopo katika sekta ya ujenzi ambayo ni miongoni mwa sekta zenye rushwa kubwa na ametaka wakandarasi watoe ushirikiano kukomesha tatizo hilo.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam

26 Mei, 2016
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top