Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

MBOWE: TUPO TAYARI KUTIMULIWA WOTE

Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson sasa amesababisha makubwa zaidi; wabunge kutoka vyama vya upinzani wako radhi kutimuliwa wote iwapo kiongozi huyo ataongoza vikao vyote vilivyosalia na wao kuendelea na msimamo wao wa kumsusia. 

Jana, Dk Ackson aliingia kuongoza kipindi cha maswali na majibu na wabunge wote wa vyama vya upinzani wakatoka ndani ya ukumbi na alipomuachia mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kuendelea na shughuli zilizosalia, walirejea ukumbini. 

“Kama Naibu Spika atakuwepo kwenye kile kiti, hatatuona bungeni, hata kama ni leo, ni kesho hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,”alisema kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe akiwa nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kuongoza wabunge wenzake kutoka ukumbini wakati wa kipindi cha maswali na majibu. 

Kauli hiyo ya Mbowe imekuja siku moja baada ya Dk Ackson kukataa Bunge kujadili sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) waliotimuliwa kwa maelezo kuwa hawafundishwi kwa muda mrefu kutokana na walimu wao kugoma wakidai malimbikizo yao. 

Kitendo cha Dk Ackson kukataa hoja hiyo ijadiliwe, kilisababisha vurugu bungeni kiasi cha kuita askari kuingia kuwatoa wabunge waliokuwa wakipiga kelele na baadaye kuwaamuru waliokataa kukaa waondoke ukumbini. 

Wakiwa nje, walifikia uamuzi wa kususia vikao vyote vitakavyoongozwa na Naibu Spika na wakaanza kutekeleza uamuzi huo jana asubuhi. 

Kauli ya Mbowe pia imekuja siku moja baada ya Kamati ya Maadili, Kinga na Haki za Bunge kuwasimamisha wabunge saba kutoka vyama vya upinzani kuhudhuria vikao vya kuanzia mkutano huu hadi ujao kwa maelezo kuwa walifanya fujo wakati wakipinga hoja ya Serikali ya kusimamisha matangazo ya moja kwa moja ya baadhi ya shughuli za Bunge. 

Jana, Mbowe alisema wako tayari kutimuliwa wote kama uamuzi huo utawapendeza viongozi wa Bunge kwa kuwa siasa inaweza kufanywa ndani na nje ya Bunge. 

Mbowe alisema kuwa hali ilishafika hatua nzuri ya kujenga demokrasia nchini na kwamba pamoja na matatizo yaliyokuwepo, hali ilikuwa ikienda vizuri. 

“Lakini tangu kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano mnaweza kuona Bunge limegeuka kituko. Bunge limegeuka mahali pa kukomoana. Bunge limekuwa mahali pa kutishana,”alisema Mbowe. 

“Naibu Spika anaamua kusitisha mjadala wa maana ili apate muda wa kuwadhibiti na kuwafukuza wabunge bungeni na anaona sifa. 

Tunaacha kujadili hoja ya msingi kama mambo ya Udom. Watoto wadogo wanalala nje haoni ni muhimu, anaona muhimu ni kuwafukuza wabunge wa upinzani.” 

Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema hawezi kukaa, kumsikiliza na kumheshimu Dk Ackson, bali wapinzani wataheshimu anayewaheshimu bila kujali anatoka chama gani na hawatamuheshimu asiyewaheshimu bila kujali cheo chake. 

“Sasa leo (jana) tumekataa kushiriki kipindi cha maswali na majibu kwa sababu yeye (Dk Ackson) anasimamia kipindi hicho na akitoka tutarudi bungeni. 

Akija mwenyekiti, akija Spika mwenyewe tutarudi bungeni. Lakini kama Naibu Spika atakuwepo kwenye kile kiti hatatuona bungeni, hata kama ni leo, ni kesho hata Bunge lote. Tuko tayari kuchukua gharama hiyo,”alisema Mbowe.

Dk Ackson alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanzia Septemba mwaka 2015 hadi Novemba 2015 alipochukua fomu za kugombea uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa tiketi ya CCM. 

Siku moja kabla ya CCM kuchagua mgombea wake, Dk Ackson alijitoa, hatua iliyoonekana ni kumpisha kada mwenye uzoefu zaidi, Job Ndugai. 

Wakati CCM wakisubiri uchaguzi wa mgombea wao, Rais John Magufuli alimteua Dk Ackson kuwa mbunge na baadaye akachukua fomu za kuwania unaibu spika, akiwa mgombea pekee wa chama hicho. 

Tangu aanze kuongoza Bunge, Dk Ackson amekuwa akikwaruzana na wabunge wa upinzani, ambao walishawahi kuhusisha kuteuliwa kwake na Rais kuwa mbunge ili apate mwanya wa kugombea unaibu spika, na mpango wa Serikali kutaka kulidhibiti Bunge. 

Akizungumzia mkakati wao jana, Mbowe alisema kwa kuwa siasa haifanywi bungeni tu, watakwenda kwa wananchi kuwashitaki viongozi wa Bunge. 

Alisema watafanya hivyo kwa kuwa kitendo cha kuwafungia wabunge wa upinzani kuwatetea wananchi ndani ya Bunge, kinaweza kufanywa pia nje ya chombo hicho. 

“Tutawaamsha wananchi nje ya Bunge kwa kuwa ni fursa hivyo tunakutana na wabunge wote waliotimuliwa na tutaungana wote bila kujali chama cha siasa kwa kuwa tumekubaliana kusimamia ajenda ya nchi na si ya chama chochote,” alisema Mbowe. 

LHRC yataka wabunge warudishwe 
Wakati wabunge saba wakianza kutumikia adhabu ya kufungiwa kuhudhuria vikao, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimelitaka Bunge kuwarejesha ili kuendelea na majukumu yao. 

Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho, Dk Helen Kijo Bisimba alisema hoja ya kuwafukuza wabunge hao kwa sababu ya kudai haki ya kurushwa bunge ‘live’ ni kuwapokonya haki Watanzania waliowachagua kwenda kuwawakilisha bungeni. 

“Wabunge hao wamechaguliwa na wananchi na wanatetea bunge hilo kurushwa ‘live’ kwa maslahi ya wananchi waliowatuma, halafu kiti cha Spika kinaamua kuwafukuza bungeni. 

"Endapo ningepewa nafasi ya kuwashauri wapiga kura, ningewaambia kwenda kushiriki vikao vya Bunge wenyewe kwa sababu wabunge wao wameondolewa bungeni, hata mimi mbunge wangu wa Kawe ameondolewa,”alisema.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top