WATENDAJI 12 wa serikali ya Zanzibar, akiwamo Naibu Mhasibu Mkuu wa Serikali wamesimamishwa kazi kutokana na upotevu mkubwa wa fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohamed, alisema kati ya watendaji hao wamo wahasibu wakuu wa wizara sita wanaohusika na upotevu huo wa fedha.
“Kwa masikitiko makubwa naomba kutoa taarifa kuwa tumebaini upotevu wa fedha za serikali ambao tumeanza kuuchukulia hatua,” alisema waziri huyo.
Alisema upotevu huo wa fedha unaonekana sio wa bahati mbaya, bali ni jambo la kupangwa na umetekelezwa kwa njama za watendaji wa vitengo vya fedha uliowahusisha wahasibu.
Aidha, alisema hadi sasa kuna hundi zenye thamani ya Sh. milioni 571 zimeshindwa kulipwa kwa sababu ya uhalifu huo na hatua za awali za kutathmini upotevu huo zinaonyesha kuwa kiasi ambacho kinahusika na wizi huo kinaweza kuwa kikubwa zaidi ya hicho.
“Tulipopata taarifa za awali juu ya upotevu huu hatua za haraka zilichukuliwa na kubaini wahusika wakuu”alisema Dk. Khalid.
Alisema taarifa za awali zinaonyesha upotevu huo wa fedha umetokana na njama za baadhi ya watendaji wa kitengo cha malipo katika Wizara ya Fedha na Mipango wakishirikiana na baadhi ya wahasibu wa wizara tofauti za serikali.
Waziri huyo alisema hatua hiyo imezingatia matakwa ya Sheria ya Fedha za Umma namba 12 ya mwaka 2005 na kanuni zake na Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2014 na kanuni zake.
Alisema kutokana na ukubwa wa upotevu huo wa fedha, hatua itakayofuata ni kuundwa kwa bodi ya uchunguzi ambayo itakuwa na watu wanne watakaoteuliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Alisema azma ya serikali ni kuimarisha utawala bora na kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, hivyo watendaji wote wanapaswa kufahamu kuwa azma hiyo inatekelezwa bila ya kuyumba wala kumuonea haya mtu yeyote.
Post a Comment