Dar es Salaam. Wakurugenzi wote 185 ambao wameteuliwa na Rais John Magufuli wiki iliyopita, wanatakiwa kufika Ikulu na vyeti vyao halisi vya taaluma ili kabla ya kula kiapo cha uadilifu wa uongozi wa umma wahakikiwe na kuthibitishwa.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amesema uhakiki huo wa wakurugenzi hao wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya unafanywa kwa lengo la kujiridhisha baada ya mchakato wa kawaida wa uhakiki kufanywa kwa kutumia vyeti visivyokuwa halisi.
Kauli hiyo ya Ikulu imeibua maswali kutoka kwa watu wa kada mbalimbali nchini kwa kuwa ni mara ya kwanza kutangazwa na kufanyika hadharani, huku kitendawili kikubwa ikiwa ni athari za utaratibu huo.
Maswali yameibuka kwamba nani atapitia vyeti hivyo, namna ya kuhusisha vyuo walivyosoma ndani na nje ya nchi, sababu za vyeti kutopitiwa kabla ya uteuzi na kama wenye vyeti vyenye utata watasubiri kupatiwa majibu au watabatilishwa uteuzi wao. Kutokana na utaratibu huo mpya, huenda baadhi ya wakurugenzi wasio na vyeti wakazuiwa kula kiapo na uteuzi wao kutenguliwa au wenye vyeti vya kughushi wakashtakiwa au wenye vyeti kutoka vyuo visivyotambuliwa wakatemwa. Pia, huenda baadhi wakaamua kujiondoa taratibu kabla ya kufika katika tanuru hilo ili wasiaibishwe.
Utaratibu uliozoeleka, ukurugenzi si nafasi ya kisiasa bali ni ya utumishi wa umma, hivyo hata waliokuwa wakiteuliwa walikuwa wakijulikana kiutendaji na kitaaluma lakini safari hii wateule wengi katika nafasi hiyo ni makada wa siasa. Miongoni mwa wateule hao 185 kuna makada zaidi ya 30 wa CCM walioshindwa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwaka jana huku wakurugenzi 65 tu ndio waliobakizwa.
Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse na Dk Benson Bana, wamesema jambo hilo ni la kawaida na linalenga kurejesha uwajibikaji na kuwa na watumishi wenye sifa katika kila eneo.
Dk Jesse amesema utaratibu wa kuhakiki nakala halisi za vyeti ni mzuri kwa maelezo kuwa miaka ya nyuma huenda haukuwepo.
“Unajua CV (wasifu wa mtu) unaweza kutofautiana na vyeti vyake. Mfano sisi tuliopo chuo kikuu tunahakikiwa vyeti vyetu halisi. Hili ni jambo muhimu maana wote wanaoghushi watabainika. Jambo hili linapaswa kufanywa kwa watumishi wote wa Serikali,” amesema
Kauli hiyo iliungwa mkono na Dk Bana ambaye alisisitiza kuwa huenda mamlaka ya uteuzi inataka kuhakiki nakala halisi za vyeti vya taaluma kwa sababu wahusika wasingeweza kuombwa vyeti kabla ya uteuzi ili kuepusha siri kuvuja na baadhi kuanza kutangaza kuwa watateuliwa kushika wadhifa fulani.
“Hapa chuo kikuu hata sisi tunahakikiwa vyeti licha ya kuwa tumesoma hapahapa na kuajiriwa. Ila kama kuna walioteuliwa ambao hawakidhi sifa zilizopo basi waondolewe na kutangaza hadharani ili liwe funzo kwa wengine,” amesema.
Loading...
Post a Comment