Jana tarehe 21/8/2016 chama cha wananchi cuf kilifanya mkutano mkuu maalumu wa taifa katika ukumbi wa hotel ya blue pearl –ubungo plaza, dar es salaam.
Chama cha cuf kinapenda kutoa taarifa rasmi za awali juu ya kilichotokea. Baraza kuu la uongozi la taifa la chama cha cuf liliitisha mkutano mkuu huo kwa madhumuni ya kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi wazi ikiwemo ya mwenyekiti wa chama taifa kutokana na aliyekuwa mwenyekiti wa chama taifa prof. Ibrahimu lipumba kujiuzulu katika nafasi hiyo tarehe 5/8/2016.
Mkutano mkuu maalum wa taifa ulitimiza akidi ya wajumbe halali waliopaswa kuhudhuria katika mkutano huo. Kwa mujibu wa katiba ya chama (1992) ibara ya 79(3) toleo la mwaka 2014 wajumbe wa mkutano mkuu walimchagua mheshimiwa julius mtatiro kuwa mwenyekiti wa kuongoza kikao hicho cha mkutano mkuu kutokana na nafasi hiyo ya mwenyekiti wa chama taifa kuwa wazi .
Wajumbe wa mkutano mkuu walizikubali na kuzithibitisha ajenda mbili za mkutano huo zilizoandaliwa na kuwasilishwa na baraza kuu la uongozi taifa ambazo ni;
Ajenda ya kwanza kupokea taarifa ya barua ya kujiuzulu kwa prof. Ibrahim lipumba, na ajenda ya pili ni kujaza nafasi wazi ya mwenyekiti wa chama taifa, makamu mwenyekiti taifa na wajumbe wanne wa baraza kuu la uongozi taifa.
Baada ya kuwasilishwa ajenda ya kwanza na wajumbe kupata nafasi za kuijadili ajenda hiyo kwa uwazi na kina, huku kukiwa na mitazamo tofauti, ghafla aliyekuwa mwenyekiti wa chama taifa prof. Ibrahimu lipumba alilazimisha kwa nguvu kuingia ndani ya ukumbi akifuatana watu ambao si wajumbe wa mkutano mkuu huo na kuanzisha vurugu ndani ya ukumbi wa mkutano.
Viongozi wa chama na mwenyekiti wa mkutano huo waliweza kuwatuliza wajumbe na kuendelea na kikao.
Kuhusu hitimisho la mjadala wa ajenda ya kwanza juu ya taarifa ya barua ya kujiuzulu kwa Prof. Ibrahim Lipumba.
Kwa mujibu wa katiba ya chama (1992) ibara ya 117 (2) baada ya mjadala wajumbe walikubaliana kufanya maamuzi juu ya kukubali na au kukataa kujiuzulu kwa prof. Ibrahimu lipumba.
Wajumbe wa mkutano mkuu walipiga kura na matokeo ni kuwa wajumbe walioafiki maamuzi ya kujiuzuru kwa prof. Ibrahimu lipumba walikuwa wajumbe 476 na waliokataa kujiuzulu kwake walikuwa wajumbe 14 na wajumbe wengine hawakupiga kura ya kukubali au kukataa.
Baada ya matokeo hayo kutangazwa na wajumbe kurejea katika ukumbi kuendelea na ajenda ya pili, huku mheshimiwa prof. Ibrahimu lipumba wakati wote akiwa ndani ya ukumbi akishuhudia maamuzi hayo ya wajumbe, wajumbe wachache waliokuwa wakikataa kujiuzulu kwa prof ibrahimu lipumba wakishirikiana na wale alioingia nao walianzisha vurugu za kutotaka kuendelea kwa ajenda ya pili ya kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi zilizowazi.
Kutokana na hali hiyo ya kufanya vurugu ndani ya mkutano mkuu, viongozi wa chama taifa walishauriana na kuona kuwa busara ni kuahirisha zoezi hilo la kujaza nafasi, na mwenyekiti wa kikao cha mkutano mkuu maalumu wa taifa mheshimiwa julius mtatiro alifunga mkutano huo mpaka hapo wajumbe watakapoarifiwa tena.
Baraza kuu la uongozi taifa lilifanya mchujo wa wagombea tisa waliojaza fomu na kupitisha majina matatu ya wagombea wa nafasi hiyo ya mwenyekiti wa chama taifa ambao ni mheshimiwa twaha taslima, riziki shaali mngwali na juma mkumbi.
Kwa nafasi ya makamu mwenyekiti waliopitishwa kugombea ni mheshimiwa salim biman na mheshimiwa mussa haji kombo.
Msimamo wa chama juu ya kadhia
Chama cha wananchi-cuf kinapenda kuwataarifu na kuwahakikishia wanachama, wapenzi wa chama chetu na marafiki zetu wote kuwa cuf ni taasisi kubwa ya kisiasa nchini iliyo na viongozi makini na mahiri.
Tunawaomba wajumbe wote wa mkutano mkuu wa taifa na wanachama wetu wote na watanzania kwa ujumla kuwa watulivu katika kipindi hichi, na kuzipuuza taarifa zote zenye lengo la kupotosha usahihi wa suala hili.
Mchakato wa kukamilisha zoezi la kujaza nafasi wazi za uongozi wa chama taifa upo palepale na baada ya kukamilisha taratibu za ndani ya chama tutatoa taarifa kwenu na kwa watanzania wote.
Ni muhimu kukumbukwa kwamba ajenda ya kwanza ya msingi katika mkutano mkuu huu imekamilika kwa wajumbe wengi wa mkutano mkuu wa chama taifa kukubali kujiuzulu kwa mheshimiwa prof. Ibrahimu lipumba.
HAKI SAWA KWA WOTE
SALIM BIMAN
MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAWASILIANO KWA UMMA.
Post a Comment