Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

SIKU 35 ZA UKUTA Vs SERIKALI

Dar es Salaam. Uamuzi wa Chadema kuanzisha operesheni ya kupinga kile inachokiita ukandamizaji wa demokrasia na kutofuata Katiba na sheria, umeibua kauli tofauti kutoka kwa viongozi wa Serikali na taasisi nyingine, huku ikiwa zimetimia siku 35 tangu operesheni hiyo itangazwe.

Operesheni hiyo imepangwa kuzinduliwa kesho kote nchini kwa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara, hali iliyosababisha maandalizi yake kukumbwa na vitendo vya askari wa Jeshi la Polisi kuwakamata viongozi wa Chadema, akiwemo Edward Lowassa, ambaye amekuwa Waziri Mkuu wa kwanza kati ya kumi walioondoka madarakani, kukamatwa na kuhojiwa.

Jana, Lowassa alitoa taarifa yake kuzungumzia kitendo hicho, akisema kimewakata “mkono wa amani” walioanza kuunyoosha kwa Serikali baada ya kukutana kwa mara ya kwanza na Rais John Magufuli Jumamosi iliyopita na kushikana naye mkono kwenye hafla ya maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Benjamin Mkapa.

Licha ya Lowassa na viongozi wengine wa Chadema kukamatwa juzi wakiwa kikaoni kwenye Hoteli ya Giraffe, jana waliendelea na vikao vya ndani kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho na Hoteli ya Courtyard ambako walikutana na viongozi wa dini, ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kutafuta suluhu.

Operesheni Ukuta ni maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam Julai 25 na 26 baada ya chama hicho kukumbwa na vikwazo kadhaa kuendesha shughuli zake, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara Kahama, viongozi kuzuiwa kuingia ofisini na madai kuwa naibu spika wa Bunge, Tulia Ackson amekuwa akibagua na kukandamiza demokrasia ndani ya chombo hicho.

Akitangaza uamuzi huo Julai 27, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema operesheni hiyo itazinduliwa Septemba Mosi kwa kufanya maandamano na mikutano nchi nzima chini ya kauli mbiu ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).

Tangu wakati huo, Serikali imekuwa ikitoa kauli tofauti kudhibiti maandamano na mikutano hiyo, huku Chadema ikidai kuwa Katiba, Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa zinakipa chama hicho haki ya kuendesha shughuli hizo na hivyo hakitabadili msimamo.

Baada ya kutoa tamko la operesheni hiyo, Julai 29, Rais Magufuli, akiwa mkoani Singida, alifafanua kauli yake ya kupiga marufuku siasa hadi mwaka 2020 aliyoitoa Juni 24 wakati akipokea ripoti ya Uchaguzi Mkuu, akisema alichopiga marufuku ni wanasiasa ambao hawakushinda kwenye uchaguzi, kufanya mikutano ya hadhara.

Pia Rais alisema amezuia wanasiasa kutoka kwenye jimbo lake na kwenda kushiriki mikutano kwenye jimbo jingine, akisema wanaoruhusiwa ni wale walioshinda kwenye uchaguzi tu.

Siku chache baadaye, Jeshi la Polisi lilizuia mkutano wa hadhara ambao Chadema ilipanga kuufanya mkoani Morogoro kwa maelezo kuwa kulikuwa na shughuli nyingine za CCM na maonyesho ya Nanenane, hivyo lingeshindwa kutoa ulinzi.

“Katika tarehe zilizoainishwa hapo juu Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekusudia kufanya mikutano ya hadhara ya wanachama, wapenzi na makada wao katika maeneo hayo hayo,” inasema taarifa ya polisi mkoani Morogoro.

Pia, taarifa hiyo inaeleza kuwa mgomo wa walimu wa shule za msingi na sekondari ulikuwa unaendelea nchi nzima, hivyo jeshi hilo lisingeweza kutoa ulinzi kwa Chadema.

Baada ya hapo kumekuwepo na kauli tofauti kutoka kwa viongozi wa Serikali kupinga operesheni hiyo.

Kauli mbalimbali za viongozi

Julai 28 mwaka huu, Msajili wa Vyama vya Siasa alidai tamko la Chadema kuhusu Ukuta, limejaa lugha za uchochezi, kashfa na kuhamasisha uvunjifu wa amani, kitu ambacho ni kinyume na Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kauli nyingine iliibuka Agosti 11, wakati mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga aliposema Chadema inapaswa kusitisha operesheni Ukuta ili kutoa nafasi kwa mahakama kufanya kazi yake kutafsiri tamko la polisi kuzuia shughuli za siasa.

JWTZ

Agosti 27, wakati msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Ngemela Lubinga akizungumza maadhimisho ya miaka 52 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo, alisema wanajeshi wamejipanga kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika sawasawa, na kwamba Serikali imeshakataza maandamano ya kisiasa.

Alisema maadhimisho ya mwaka huu yatafanywa mitaani na hivyo hawategemei kuona shughuli nyingine za kisiasa.

Mwanasheria Mkuu

Kauli hiyo ilifuatiwa na ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju ambaye aliwaambia wanahabari mapema wiki huu kuwa Chadema inatakiwa iheshimu tamko la Jeshi la Polisi kuzuia mikutano na maandamano yasiyo na kikomo na kwamba wakikaidi tamko hilo watavunja Katiba.

Masaju alisema zuio hilo la mikutano ya kisiasa ni la muda na kwamba hali ikitulia, vyama vitaendelea na shughuli zao.

Wakati wote huo tangu Chadema itangaze operesheni hiyo, Jeshi la Polisi limekuwa likitoa matamko kupitia kwa makamanda wa mikoa, ambao walianzisha mazoezi ya wazi kwenye mitaa ya mkoa mbalimbali nchini, wakisema kuwa wamejipanga kudhibiti Ukuta.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema wameshauvunja Ukuta na watawashughulikia watakaojaribu kufanya maandamano siku hiyo.

Agosti 27, vyama takribani 10 vya siasa viliibuka na kupinga operesheni Ukuta, huku mwenyekiti wa klabu ya vyama hivyo, Fahmi Dovutwa akisema ni wakati wa kumwacha Rais Magufuli kufanya kazi.

Hata hivyo vyama vingine, vikiongozwa na ACT-Wazalendo vimekuwa vikiunga mkono ‘kiaina’ operesheni hiyo, kwa kutaka nchi iongozwe kwa kufuata utawala wa sheria.

Viongozi wa dini

Operesheni ya Chadema pia iliwaibua viongozi wa dini ambao Agosti 27, ambao walitaka kuwepo na maridhiano ili kudumisha amani.

Wakizungumza na Mwananchi, Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Mkuu Abubakar Zubeir na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili na Kilutheli Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo waliwataka viongozi wa Serikali na Chadema kutafuta njia ya muafaka kumaliza msuguano.

Kauli hiyo iliungwa mkono na katibu mkuu mstaafu wa makanisa ya Pentekoste, Askofu David Mwansota na mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako”.

Watu waliohojiwa na Mwananchi kuhusu hali hiyo, walikuwa na maoni tofauti.

“Nadhani viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kutii sheria, lakini vilevile wafuate taratibu. Mlango upo wazi, waonane na viongozi wa Serikali,” alisema mhadhiri wa siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Benson Bana.

Bana alisema ni vyema Chadema wakalisikiliza Jeshi la Polisi kwa kuwa ndilo linalojua viashiria vya uvunjifu wa amani.

Alipoelezwa kuhusu kitendo cha Lowassa kushikana mkono na Rais Magufuli, Profesa Bana alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani hana ridhaa ya kuwasemea wananchi.

“Sawa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Waziri Mkuu mstaafu, lakini haiwezekani mtu mmoja hata kama ni maarufu zaidi, akataka mazungumzo,” alisema.

Alisema wanachotaka kufanya Chadema ni sawa na kupita mtaani na kumtukana Rais kuwa ni dikteta, jambo ambalo alisema halikubaliki.

Aliongeza kuwa Ukuta ni dhambi ya asili na haifai kupandikizwa kwa wananchi.

“Chama cha siasa ni kikundi, vyama vyote vya siasa vina haki sawa, Rais wa nchi akishachaguliwa hana budi kuheshimiwa, hayo maandamano ni kutafuta umaarufu kwa kutumia mbinu za miaka 20 iliyopita,” alisema.

Ushauri kwa Chadema pia ulitolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Utafiti na Taaluma), Profesa Ludovick Kinabo.

“Naomba chochote kisitokee siku hiyo, tusije kuzungumza mengine,” alisema alipoulizwa kuhusu ushauri anaoutoa.

Alisema ni vyema Chadema wakaitii mamlaka kwa kuwa ndiyo inayotawala.

“Lazima tufikirie haya maandamano. Hata kama wakiandamana watu wawili au watatu, wakifa itakuwaje?” alihoji.

Lakini spika wa zamani wa Bunge, Pius Msekwa alisema huu si wakati muafaka wa mazungumzo hata kama Lowassa alijaribu kutafuta mwanya wa kuzungumza na Serikali.

“Mazungumzo hufanyika wakati watu wapo tayari kukubaliana na wana nia. Mazingira haya kwa sasa hayapo,” alisema.

“Mimi nilimsikia Mwanasheria Mkuu alivyosema na hata wewe nadhani umemsikia. Kwa maoni yangu hayo mazingira ya mazungumzo hayapo.”

Alisema msimamo wa Ukuta ni kuvunja sheria na kila anayevunja sheria lazima awajibishwe.

“Kila upande umeshikilia upande wake hakuna mazingira ya maelewano, lakini basi Chadema ifahamu kuwa vyovyote wanavyokusudia kufanya, wanavunja sheria,” alisema.

Alisema madhara ya maandamano hayo yatakuwa kwa wengi hata wasiohusika na huenda wakalipeleka Taifa kwenye maafa.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Nsato Marijani alisema tayari jeshi la polisi lilishatoa katazo la maandamano hayo na hakuna haja ya kurudia amri hiyo.

Kuhusu Lowassa kutafuta fursa ya mazungumzo, Marijani alisema:

“Mazungumzo ya Lowassa kwenye Jubilei sisi yanatuhusu nini? Kwani mazungumzo hayo yalitaka suluhu na Jeshi la Polisi?” alihoji.

“Sisi tunasema wazi kuwa Septemba Mosi kuna mambo mengi ambayo yanafanya tuzuie maandamano ya Ukuta kwa sababu ya viashiria vya uvunjifu wa amani.”

Lakini mhadhiri wa UDSM, Richard Mbunda alisema iwapo wafuasi wa Chadema wataandamana, Jeshi la Polisi linapaswa kubadili mpango wake wa kutumia nguvu kuwazuia, badala yake liwalinde ili kuepusha hali ya hatari.

Alisema watu wa kada mbalimbali wametoa ushauri kuhusu suala hilo, lakini hakuna hatua ya maana iliyofikiwa na kutaka busara itumike zaidi ili nchi isikumbwe na mchafuko ya kisiasa kama yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001.

“Upande mmoja unataka amri yake iheshimiwe, upande mwingine unataka uruhusiwe kufanya mikutano kwa sababu una haki ya kisheria na kikatiba. Tusubiri hiyo siku ifike tuone,” alisema Mbunda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe alisema: “Nadhani mazungumzo ndio suala la msingi katika kuamua kila jambo. Ushauri wangu ni huo maana Chadema wakigoma maelezo wanayopewa sasa, maana yake wamejiandaa kwa mapambano, jambo ambalo si zuri.”

Wangwe alisema kupitia Baraza la Vyama vya Siasa, pande hizo zinaweza kukutana na kujadili suala hilo kwa maslahi ya nchi.

Jana, Lowassa alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akisema kukutana kwake na Rais Magufuli kwenye hafla ya Jumamosi, kulikuwa mwanzo wa juhudi za kuliepusha Taifa kuingia kwenye machafuko, lakini polisi imetibua kwa kuwakamata.

Jeshi la Polisi lilikazia amri yake ya kuzuia mikutano wiki iliyopita, lilipotangaza kupiga marufuku mikutano yote ya ndani yenye viashiria vya kutaka kuvunja amani, likisema hata vikao vya harusi vitakavyoonekana kuwa na chembechembe hizo vitazuiwa na wahusika kukamatwa.

Serikali imepiga marufuku mikutano ya hadhara tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu kwa kuanzia na kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliyoitoa jimboni kwake Ruangwa na baadaye kukanusha bungeni. Jeshi la Polisi na baadaye Rais Magufuli nao walipiga marufuku mikutano hiyo.

Sababu za kuzuiwa maandamano na mikutano hiyo zimetolewa kwa maelezo tofauti; wanasiasa walioshindwa kutokuwa na sababu za kushukuru wananchi, kufariki kwa watu sita mkoani Dodoma kwa ugonjwa usiojulikana, kugundua kuwa mikutano hiyo inalenga kushawishi wananchi kutotii maagizo ya Serikali.

Sababu nyingine zilizotolewa ni mikutano hiyo kuwa na viashiria vya kuvunja amani, Jeshi la Wananchi (JWTZ) kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa na kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu na hivyo siasa kuwekwa kando hadi mwaka 2020 wakati wa kuchagua viongozi wengine.

Picha zilizotumwa na Ikulu Jumamosi zinamuonyesha Lowassa akiwa ameshikana mkono na Rais Magufuli.

Wanasiasa wengine waliowahi kushika nafasi ya Waziri Mkuu ni Julius Nyerere, ambaye baadaye akawa Rais wa kwanza wa Tanzania, Rashid Kawawa, Jaji Joseph Warioba, Dk Salim Ahmed Salim, John Maelecela, Cleopa Msuya, Mizengo Pinda, Edward Sokoine na Frederick Sumaye, ambaye pia alihamia Chadema wakati wa kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita.


Source: Mwananchi
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top