Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Asilimia 60 ya Watanzania wapinga "udikteta" wa Rais Magufuli

ASILIMIA 58 ya Watanzania wamepinga kauli za baadhi ya wanasiasa kuwa Rais John Magufuli anaendesha nchi kidikteta huku asilimia 31 imesema haina uhakika na jambo hilo.

Aidha, imeelezwa kuwa asilimia 80 ya wananchi wanaona kwamba baada ya uchaguzi juhudi za kimaendeleo zipewe kipaumbele na vyama vya siasa.

Akitoa taarifa za utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Twaweza jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze alisema ni asilimia 11 pekee ya Watanzania ndiyo waliosema nchi hii inaongozwa kidikteta.

“Baadhi ya wanasiasa na wasomi walitafsiri uongozi wa Rais Magufuli kama udikteta na neno hilo likawa mojawapo ya mambo yaliyounda Ukuta, asilimia 11 wanakubaliana na wazo hilo lakini asilimia 58 wanalipinga huku asilimia 31 wanasema hawana uhakika,” alisema Eyakuze.

Alisema kundi kubwa ambalo limejibu kuwa Rais Magufuli ni dikteta ni la vijana na watu matajiri na wenye uwezo wa juu kiuchumi kuliko masikini, wazee na watu wenye elimu ya chini; huku alisema asilimia 29 ya wananchi walio karibu ya vyama vya upinzani wanamuona Rais kuwa ni dikteta na asilimia tano ni wa chama tawala yaani CCM.

Aidha, alisema wananchi wana uelewa tofauti tofauti kuhusu neno udikteta, asilimia 32 walitafsiri kama kutawala kimabavu, asilimia 15 walitafsiri kuwa mtu mmoja ndiye mwenye maamuzi ya nchi nzima, huku asilimia 34 ya watu waliohojiwa hawaelewi maana ya neno hilo.

Katika demokrasia, Eyakuze alisema asilimia 51 ya Watanzania walisema mikutano inasaidia kuiwajibisha serikali huku asilimia 49 ikisema mikutano huvuruga umakini wa serikali na wananchi kudhoofisha shughuli za kimaendeleo.

Katika suala la maandamano, asilimia 50 walisema hawawezi kushiriki maandamano yoyote, asilimia 29 wanaweza kushiriki na asilimia 20 walijibu kuwa hawajui.

“Kati ya takwimu hizo, vijana waliosema wako tayari kushiriki maandamano yoyote na siyo lazima ya ukuta ni asilimia 35, watu wazima ni asilimia 15, wafuasi wa CCM asilimia 27 na wa vyama vya upinzani ni asilimia 43,” alisema Eyakuze.

Aidha alisema kuwa miongoni mwa waliosema kuwa hawatajiunga na maandamano asilimia 45 walisema ni kwa sababu wana wasiwasi itatokea vurugu na asilimia 29 walisema kwa sababu siyo njia sahihi za kutatua matatizo.

Alisema wananchi sita kati ya kumi waliunga mkono kuzuiwa kwa mikutano ya kisiasa wakiwemo wale wa vyama vya upinzani waliunga mkono suala hilo.

“Asilimia 60 waliunga mkono maamuzi ya Rais kuzuia mikutano ya kisiasa huku wazee wengi zaidi ndio walioonekana kuunga mkono zaidi uamuzi huo ambao ni asilimia 70 na vijana asilimia 55 na asilimia 31 ya wafuasi wa vyama vya upinzani wanakubaliana na kuzuiwa kwa maandamano ya Ukuta."

Asilimia 16 wananchi wanafahamu harakati za ukuta na asilimia 79 hawafahamu harakati hizo na miongoni mwa wanaofahamu uelewa wao kuhusu harakati hizo ni asilimia 48. Na kwamba kati ya wanaofahamu ukuta asilimia 50 walijibu wanaunga mkono ukuta na asilimia hamsini hawaungi mkono.

“Asilimia tisa kati ya wanaounga mkono ukuta katika maandamano ya Septemba mosi walipanga kushiriki ambapo ni pamoja na asilimia tatu ya wale wa chama tawala,” alisema.

Katika utafiti huo umeonesha kuwa wananchi hawakubaliani na mbinu zinazotumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani katika kuhakikisha demokrasia inalindwa. Kwa niaba ya CCM, Msemaji wake, Christopher ole Sendeka alisema kundi ambalo linasema Rais ni dikteta ni la watu matajiri ambao wanaona mianya yao ya ulaji imezibwa.

Alisema anaunga mkono utafiti huo kwani umetoa hali halisi ya mambo hayo yaani udikteta, demokrasia na maandamano.

“Naunga mkono utafiti huu, mwanzoni tulikuwa na ukwepaji mkubwa wa kodi, wizi wa mali za serikali anachofanya Rais sasa ni kusimamia nidhamu ndio maana watu wenye kipato cha juu watasema Rais ni dikteta baada ya kuziba mianya yao ya wizi,” alisema Ole Sendeka.

Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zitto alisema ni wajibu wa vyama pamoja na ajenda za kitaifa kuonesha tofauti zilizopo.

Alisema hatuwezi kusema nchi ina udikteta moja kwa moja kwani baadhi ya mambo yanafanyika kwa uhuru, lakini kuna baadhi ambayo serikali pekee ndiyo inayoyasemea.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top