Loading...
CUF wamjibu Msajili Jaji Mutungi
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tarehe: 24 Septemba, 2016
The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimepokea kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa
Chama cha Civic United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, jana usiku.
Baada ya kupokea Ushauri huo, The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kinapenda kueleza yafuatayo:
1. Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992) haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi
ya vikao vya Chama.
2. Msimamo huo wa kisheria wa nchi hii umetiliwa nguvu na kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UAMUZI wa tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua kwamba:
“… I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make.”
Tafsiri ya uamuzi huo ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa na maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”
3. Kwa msingi huo, CUF hatukuomba ushauri kwa Msajili na hivyo tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.
4. Kwa msingi huo huo, tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya siasa na na kuyatolea uamuzi. Uwezo huo ni wa Mahakama. Hivyo tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote kupuuza ushauri huo wa Msajili na wamwachie mwenyewe ndoto zake na propaganda za kitoto.
5. Ni fedheha na aibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa mwenye hadhi ya Ujaji kukubali kutumiwa kiasi hicho na kushindwa hata kufanya rejea kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu tulioutaja hapo juu ambao umeweka bayana kwamba hana madaraka na uwezo aliojifanya anao. Itakumbukwa kwamba Wabunge wa CUF walifanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma tarehe 15 Septemba, 2016 na kumtahadharisha Msajili asikubali kutumiwa kufanya alichokuwa anatakiwa kukifanya. Ni bahati mbaya sana kwamba amefanya kile kile ambacho Wabunge wa CUF walieleza kwamba walikuwa na taarifa kuwa ameagizwa kukifanya.
6. Tunajua kwamba baada ya hatua hiyo ya Msajili kufanya kazi asiyo na uwezo wala mamalaka nayo na katika kutimiza malengo ya wanaotuma, mchana wa leo Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni kimevamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam na kupiga watu na kufanya uharibifu wa mali. Tunamwambia Msajili wa Vyama vya Siasa atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na kikundi hicho ikiwemo watu watakaoumizwa na uharibifu wa mali utakaofanywa kutokana na tamko lake hilo ambalo halina msingi wa kisheria.
7. Tunatambua yote haya yanafanywa kwa sababu watawala wameingiwa kiwewe kutokana na hatua kubwa ambazo zimefikiwa na CUF katika kupigania haki yake ya ushindi ulioporwa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015. CCM haijakaa sawa tokea iliposhindwa vibaya na CUF katika uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani mwaka 2015 na sasa imepata mfadhaiko kutokana na jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyosimama kidete kutetea maamuzi hayo ya
kidemokrasia na haki za binadamu za Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla. Ni vyema watawala na kibaraka wao Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake pamoja Msajili anayewatumikia wakatambua kwamba CUF
haiyumbishwi na michezo yao ya kitoto na itaendelea kusimamia malengo yake ya kupigania haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar na Tanzania kikamilifu.
8. Chama kinasisitiza tena kwamba maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la tarehe 28 Agosti, 2016 ni halali na yako pale pale na kwamba Prof.
Ibrahim Lipumba si Mwenyekiti wa CUF na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa wataendelea kubakia wamesimamishwa au kufukuzwa isipokuwa tu
iwapo vikao vya Chama vitakapofanya maamuzi mengine.
9. Chama kinawataka viongozi wake wote na wanachama wake katika ngazi zote kuanzia Taifa hadi Tawi kuendelea na kazi zao za ujenzi wa Chama
kama kawaida na kuendelea kufuatilia harakati za Chama chao kupigania ushindi wetu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
HAKI SAWA KWA WOTE
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU - CUF
Post a Comment