Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Kilichoamuliwa sakata la UVCCM Arusha



VMM/U.80/8/Vol.I/55      20/09/2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa imekutana Jumatatu Tarehe 19/09/2016 katika Ukumbi wa UVCCM Makao Makuu, Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Sadifa Juma Khamis (MCC)(MB). Kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili na Nidhamu ya UVCCM Taifa, pamoja na mambo mengine kilipokea na kujadili Uhai wa Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya ya Vijana Mkoani Arusha.
Kikao kilipokea Taarifa na kutafakari, kujadili na kufanya maamuzi yafuatayo:-
1. NDUGU LENGAI OLE SABAYA MWENYEKITI WA UVCCM MKOA WA ARUSHA
Kwa nyakati tofauti Ndugu Sabaya alisimamia na kuyaongoza makundi ya Vijana wa CCM na wasiokuwa wa CCM ili kumkataa Katibu wa UVCCM aliyehamishiwa Mkoani Arusha Ndugu Said Goha kuchukua nafasi ya Ndugu  Ezekiel Mollel licha ya yeye kupewa heshima na kuelimishwa na Vikao vya Taifa na Viongozi mara kadhaa kupitia Mwenyekiti wa UVCCM Taifa kuhusu mamlaka za Kikanuni, Kanuni ya UVCCM Kanuni ya Utumishi na Kanuni ya Maadili.
Ndugu Sabaya amesababisha taharuki iliyopelekea Ofisi ya UVCCM Mkoa wa Arusha kufungwa kwa minyororo hadi Jeshi la Polisi kuingilia kati. Vile vile taharuki hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa Vijana wa Mkoa wa Arusha kugawanyika katika makundi na kupelekea hali ya Kiusalama na Maadili kwa Jumuiya na Chama kuwa ya wasiwasi.
Ndugu Sabaya kufikishwa Mahakamani akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kujifanya Mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Huku kosa la pili katika muda usiojulikana akidaiwa kughushi vitambulisho vya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) chenye namba MT 86117 wakati akijua ni kinyume cha Sheria za nchi.
Kamati ya Utekelezaji ilipitia tuhuma mbali mbali za vielelezo vya utapeli na ulaghai unaodaiwa kutendwa na Ndugu Lengai Sabaya katika maeneo tofauti huku akijua ni kinyume na miiko ya Maadili ya Uongozi wa UVCCM na CCM.
Kwa makosa yote hayo Ndugu Lengai Ole Sabaya ameyafanya kwa kukiuka Kanuni ya Uongozi na Maadili ya CCM Fungu la (3) ukurasa wa 16 na 17, na fungu la nne (4) ukurasa wa 29, 30 na 31. Pia makosa hayo ameyatenda kinyume na taratibu za Uongozi na Maadili za UVCCM, Ibara ya 6.3.2 Ibara ya 7.5.1, 7.5.4 na 8.2.5.
Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa imependekeza kwa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kumvua uongozi Ndugu Lengai Ole Sabaya, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha.
Wakati tukisubiria maamuzi ya Chama Cha Mapinduzi, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imemsimamisha Uongozi wa Nafasi yake ndani ya UVCCM kutokana na kesi iliyoko Mahakamani na kumtaka kuanzia leo tarehe 20/09/2016 asijihusishe na shughuli zozote za Uongozi wa UVCCM hadi hatima ya tuhuma zake itakapoamuliwa na Mahakama na Vikao husika vya UVCCM na CCM.
2. NDUGU EZEKIEL MOLLEL
Ndugu Ezekiel Mollel alipokuwa Katibu wa Vijana Mkoa wa Arusha alipewa barua ya Uhamisho, kama inavyoelekezwa na Kanuni ya Utumishi ya UVCCM kifungu cha 3(13) ukurasa wa 21 na 22 inayozungumzia Uhamisho wa mtumishi, Nukuu
“Mfanyakazi yeyote atakayekataa kutii amri ya Uhamisho bila sababu zinazokubalika atachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni hizi”, kama ilivyo katika kifungu cha 7(4)(b)(x). Katika kifungu hiki yameainishwa makosa mengi lakini aliyoyatenda Ndugu Mollel ni haya yafuatayo:-  Kuachishwa na Kufukuzwa Kazi” Nukuu “Mfanyakazi yeyote wa UVCCM ikithibitika kuwa amefanya mojawapo ya makosa yafuatayo ataachishwa Kazi”

(i) Kuwa ni mwenye hatia ya kitendo cha ukosefu wa Adabu mahali pa kazi au wakati wa kazi.

(ii) Kwa makusudi kukataa kutii amri/maagizo halali ya Wakuu wa Kazi au kukataa kutii amri ya Uhamisho.

(iii) Kushiriki kwa njia moja au nyingine katika kutenda mambo yaliyo kinyume na Maadili ya Uongozi UVCCM na CCM.
Makosa haya ameyarudia Ndugu Ezekiel Mollel aliwahi kusimamishwa kazi mwaka 2015 akiwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Manyara, jambo ambalo lilipelekea kumnyang’anya Kituo na Kumsimamisha Kazi kwa muda, pamoja na yote hayo bado Ndugu Ezekiel Mollel hakuweza kujirekebisha hata pale aliporudishwa Kazini na kupelekwa Mkoa wa Arusha.

Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa imebariki maamuzi yaliyochukuliwa na Sekretarieti ya Baraza Kuu ya UVCCM Taifa iliyokutana tarehe 14/09/2016. Kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa imependekeza kwa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kumfukuza Kazi mara moja Ndugu Ezekiel Mollel.

TUHUMA ZA KUIBUA UFISADI
Kuhusu madai ya tuhuma zinazotolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha kuwa kuna ufisadi na baadhi ya Viongozi wa Makao Makuu ya UVCCM Taifa wanahusika.
Ikumbukwe kuwa Umoja wa Vijana wa CCM ulianza kujitathimini na kuhakiki Mali za Jumuiya tokea mwezi Desemba, 2015.

Umoja wa Vijana wa CCM Taifa kwa agizo la Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa mwezi Julai, 2016 ulikamilisha uhakiki wa Mali zote za UVCCM Taifa, Mikoa na Wilaya na kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi.

Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa Mikoa  iliyobainika kuwa taarifa zake hazikuwa na ukweli na kubainisha matakwa ya uhakiki kama walivyoagizwa.

Kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa kilichokutana tarehe 18/08/2016 Mjini Dodoma kupokea na kupitia taarifa za uhakiki Mali za UVCCM ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya kiliagiza Sekretarieti ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa kuwaita Viongozi wa Mkoa wa Arusha ili kuendelea kujiridhisha na taarifa walizowasilisha Makao Makuu kwa vile zimebainika kuwa na mapungufu makubwa.

Katika Taarifa hiyo iliyowasilishwa kwa maandishi na kuthibitishwa na Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa wa Arusha hakuna sehemu ambayo kumeainishwa ubadhirifu ama upotevu wa fedha kinyume na madai yaliyoibuliwa siku za karibuni baada ya Viongozi hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kutokana na makosa ya Maadili ya Uongozi.

Hata Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa wa Arusha ilipoitwa katika kikao cha Kamati ya Maadili cha tarehe 19/08/2016 kilichofanyika Mjini Dodoma walikana na kudai wao hawajawasilisha malalamiko yoyote kuhusu tuhuma wanazozitoa na kusema wanaendelea na kufanyia kazi na kurekebisha mambo ya msingi kuhusu Uchumi wa Mkoa wao.

Kufuatia hatua hiyo Kamati ya Maadili na Nidhamu na Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa iliagiza Ofisi ya Katibu Mkuu iendelee kufuatilia kwa karibu jambo hilo ili kubaini ukweli baada ya kujiridhisha kuweko na harufu ya ubadhirifu, jambo ambalo limepelekea Viongozi hao kutosema ukweli pamoja na kusisitizwa mara kadhaa kwa maandishi bado taarifa zao hazikujitosheleza.

Ofisi ya Katibu Mkuu ilitoa miongozo ya uhakiki kupitia barua Kumb. Na. VMM/C/C.30/15/77 ya tarehe 6/04/2016 na VMM/C/C.30/15/107 ya tarehe 28/07/2016 na VMM/C/C.30/15/112 ya tarehe 29/07/2016.

Kamati ya Utekelezaji imeagiza Sekretarieti kuendelea na hatua zake za kufuatilia jambo hilo na taarifa iwasilishwe haraka iwezekanavyo.

Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imeteua wajumbe watatu wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Mhe. Mboni Mhita (MB)(MNEC) kufuatilia kwa karibu suala la Arusha na taarifa iwasilishwe katika vikao husika.

Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imeendelea kusisitiza UVCCM ni Taasisi kubwa hivyo uendeshaji wake wa kazi ni uzingatiaji wa Kanuni, Taratibu na Miongozo hivyo haitamkingia kifua mtu katika jambo ambalo linahatarisha uhai au uhujumu wa rasilimali za Jumuiya.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top