Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Rais Magufuli azindua ndege mbili mpya za ATCL


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Septemba, 2016 amezindua ndege mpya mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400 zilizonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Uzinduzi wa ndege hizo za kisasa zilizotengenezwa nchini Canada, umefanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Ian Myles, Mawaziri, Wabunge, Viongozi wa Wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali na wadau wa usafiri wa anga.

Kabla ya kuzindua ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja, Rais Magufuli ameshuhudia makabidhiano ya mkataba wa ukodishaji wa ndege hizo kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi kwa niaba ya Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) kwenda kwa Katibu Mkuu Uchukuzi Dkt. Leonard Chamriho kwa niaba ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

Taarifa ya ununuzi wa ndege hizo iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa ndege hizo ni mali ya Serikali na zitakodishwa kwa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa lengo kutoa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi.

Imeongeza kuwa ndege hizo zimenunuliwa kwa kuzingatia kuwa zinafaa kufanya kazi katika mazingira ya Tanzania ikilinganishwa na ndege nyingine za jamii yake, na imetaja manufaa hayo kuwa ni pamoja na uwezo wa kuruka na kutua katika viwanja vya lami na visivyo vya lami, matumizi madogo ya mafuta, kuwa na injini zenye nguvu zaidi na kubeba mzigo mkubwa.

"Ni dhairi kuwa ndege hizi zitaimarisha mtandao wa huduma za usafiri wa anga kwa soko la ndani, lakini pia zitaongeza ushindani na kuleta unafuu wa bei kwa watumiaji wa usafiri wa anga, vilevile zitaimarisha sekta za biashara na uwekezaji na kuwezesha watalii kutembelea vivutio vya ndani ya nchi" ameeleza Balozi Kijazi.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na kutimia kwa ahadi aliyoitoa ya kununua ndege mpya ili kufufua usafiri wa anga kupitia ATCL na ameahidi kuwa Serikali imeanza mazungumzo ya kununua ndege nyingine mbili zitakazofanya safari za ndani na nje ya bara la Afrika ambapo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160, na nyingine itakuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 240.

"Kwa sababu fedha za kununulia ndege hizo zote mbili kubwa zipo, tukinunua ndege ya kubeba watu 240 itakuwa inatoka hapa Dar es Salaam hadi Marekani bila kutua popote, itaondoka hapa Dar es Salaam mpaka China bila kutua popote ili watalii wanaotoka China, Marekani, Urusi, Ujerumani na nchi nyingine wasifikie nchi nyingine, watue hapa moja kwa moja na waangalie maliasili zetu tulizonazo, utalii wetu upande, na huo ndio mwelekeo wa nchi yetu tunaoutaka" amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewataka Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuleta mabadiliko yenye manufaa kwa nchi na kuwapuuza watu wanaobeza juhudi hizo wakiwemo waliobeza ununuzi wa ndege hizo kwa kujenga hoja zisizo za msingi.

Aidha, Dkt. Magufuli ameitaka Bodi na Menejimenti ya ATCL kufanya kazi kwa weledi na ufanisi huku akiisisitiza kuondoa kasoro zote zilizosababisha kampuni hiyo kudorola ikiwemo kuchuja na kuwaondoa wafanyakazi watakaoshindwa kuendana na mwelekeo unaostahili, wasio waadilifu na waaminifu, wasaliti na wahujumu.

Rais Magufuli pia amewataka Watanzania wote wafanyabiashara, wakulima na wafanyakazi kusafiri kwa kutumia ndege hizo ili Kampuni ya ATCL ijiimarishe na iweze kujiendesha badala ya kutegemea ndege za Serikali.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

28 Septemba, 2016


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa na maafisa na viongozi wengine mbalimbali akikata utepe kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimshukuru Balozi wa Canada nchini Mhe. Ian Myles baada ya kukata utepe kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakiingia kwenye ndege mojawapo baada ya kukata utepe kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli pamoja na maafisa wengine waandamizi wakiwa kwenye ndege mojawapo baada kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na mkewe Mama Janeth Magufuli wakitoka kwenye ndege mojawapo na kuelekea ingine baada kuzindua rasmi ndege mbili mpya aina ya Bombadier Q400 zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam leo Jumatano Septemba 28, 2016.
BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI

Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top