Vilio vya furaha kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki, vimetawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam jana, baada ya kuwasili kwa madereva 10 wa Tanzania waliotekwa na kunusurika nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Madereva hao waliwasili katika uwanja huo saa 9 alasiri, wakitoka Kigali, Rwanda kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda na kukutana na familia zao kwa mara ya kwanza baada ya kuokolewa.
Wakiwa uwanja wa ndege, walizungumza na waandishi wa habari na kueleza namna walivyotekwa na waasi waliovalia sare za jeshi zisizofanana na walivyosafirishwa zaidi ya kilometa 50 porini usiku na mchana, wakitembea kwa magoti na kupoteza tumaini la kupona huku baadhi wakifanikiwa kutoroka na wengine kuokolewa.
Kabla ya kuwasili kwa madereva hao, ndugu hao walikusanyika uwanjani hapo wakiwa na shauku ya kukutana na madereva hao ambao Septemba 14, mwaka huu, walikumbwa na kadhia ya kutekwa na kundi la wanamgambo huku magari waliyokuwa nayo yakichomwa moto na hatma yao kutojulikana.
Hata hivyo, kutokana na juhudi za Serikali ya DRC na Tanzania, madereva hao walifanikiwa kuokolewa na kupatiwa matibabu ambapo jana walirejea nchini rasmi.
Baada ya madereva hao kumaliza kuzungumza na waandishi wa habari, walitoka nje kwenda kuonana na ndugu zao waliokuwa wamekusanywa pembeni, lakini walipowaona tu walishindwa kujizuia na kuwakimbilia madereva hao ambao nao waliwakimbilia huku wakilia na kutamka maneno ya kumshukuru Mungu kwa kuonana tena.
Baadhi ya familia ziliambatana na watoto wa madereva hao, ambao katika hali ya kutia simanzi baada ya kuwaona wazazi wao, waliangua kilio kwa sauti huku wakiwaita baba zao na kuwakumbatia kwa furaha.
Madereva waliookolewa kutoka Tanzania na waliowasili jana ni Kumbuka Selemani, Hussein Mohammed, Bakari Nassoro, Issa Omary, Amdani Zarafi, Adam James, Mbwana Said, Ali Juma, Athuman Fadhil na Amis Mshana.
Familia za madereva zazungumza
Mke wa dereva Ali Juma, Jamila Ali, alisema anamshukuru Mungu kwa kuonana tena na mumewe, jambo ambalo hakulitarajia kwani baada ya kupewa taarifa za kutekwa kwake, walikata tamaa ya kumuona tena. Pia alizishukuru Serikali zote mbili kwa juhudi za haraka, walizochukua baada ya kupata taarifa ya kutekwa kwa mumewe na wenzake.
“Mimi nilipata taarifa kutoka kwa mwanangu mkubwa aliyenisihi nimpigie simu baba yake, lakini baada ya kupiga simu ilikuwa ikipokewa na kuwekwa pembeni bila mtu kuongea, lakini nilisikia watu wakiongea kwa lugha ya kifaransa mpaka nikamaliza vocha yangu ya Sh 10,000,” alisema.
Alisema wakati akipiga simu hiyo, alikuwa hafahamu chochote kuhusu kutekwa kwa mumewe, ila baadaye alisikia kwenye taarifa ya habari, ndipo alipotambua kuwa na mumewe yupo miongoni mwa madereva waliotekwa kutokana na kampuni iliyotajwa ambao ni Simba Logistics.
Mariam Ayoub ambaye ni mke wa Mbwana Said, alisema anamshukuru Mungu baada ya mumewe kurejea salama na kwamba siku ya jana ni ya furaha kwake na familia yake.
Alisema tangu apate taarifa za kutekwa kwa mumewe kupitia taarifa ya habari hakuweza kula, wala kulala usingizi huku akiwa na mtoto mdogo wa mwaka mmoja na nusu.
“Leo nina furaha kubwa wala siwezi kuelezea zaidi,” alisema huku akilia.
Naye dada wa Bakari Nassoro, Halima Juma ambaye alikuwa akielezea furaha ya kuonana na ndugu huku akilia, alisema familia yake ilishakata tamaa ya kumuona tena ndugu yao huyo kutokana na simulizi za kutisha, walizokuwa wakihadithiwa kuhusu waasi wa DRC.
Baada ya kuonana na familia zao, madereva hao walipiga picha ya kumbukumbu na kisha kuondoka uwanjani hapo kila dereva na familia yake.
Madereva wasimulia
Awali wakati akisimulia kama sinema juu ya kilichowapata wakati wakitekwa, Kumbuka Selemani, alisema siku hiyo ya Septemba 14, mwaka huu katika eneo la Namoya Jimbo la Kivu Kusini mwa nchi ya DRC, madereva hao walitoka kushusha mzigo wa saruji kilometa 12 kutoka eneo walilotekewa.
Alisema mara baada ya kushusha mzigo huo wakati wakirejea, walikuwa wakiongozana na magari mengine ya kampuni hiyo ya Simba Logistics yeye akiwa dereva wa gari namba nane.
Alisema wakati akikaribia eneo la Kivu, ghafla alisimamishwa na mtu aliyekuwa amebeba silaha nzito huku amevaa mavazi ya jeshi yasiyoeleweka, kwa maana ya kuchanganywa na kumtaka ashuke kwenye gari hilo na amkabidhi kila kitu, ikiwemo hati yake ya kusafiria na kadi ya gari.
“Wakati nimeshashuka niko chini namkabidhi vitu vyangu, mara lilitokea gari la tisa ambalo baada ya kumuona yule mwanajeshi, lilisimama na kuanza kugeuza kwa maana ya kukimbia. Ndipo yule askari akaachana na mimi akaanza kulirushia risasi lile gari lililokuwa linaendelea kugeuza,” alisimulia.
Alisema risasi zile kwa bahati zilipiga kwenye kioo cha pembeni cha lori lingine la 10 lililokuwa linalokuja ambalo nalo baada ya kuona hali ile liligeuza. “Mimi nilipoona ameelekeza mawazo yake kwenye yale magari nikapata upenyo na kukimbilia porini.”
Alisema aliingia msituni na kuanza kutembea umbali mrefu akitafuta kujiokoa hadi alipoona kikosi kingine cha polisi ambacho alilazimika kukichunguza kwanza ili kujua kama ni wale watekaji au askari halali wa nchi hiyo.
Alisema alibaini kuwa ni askari halali kutokana na mavazi yao kuwa ya kawaida ya kipolisi bila kuchanganywa ndipo alipojitokeza na kujisalimisha kwa kunyoosha mikono juu. Askari wale walimchukua na kumhoji na kisha kumpatia huduma za kawaida ikiwemo chakula.
“Wakati najiandaa kupanda pikipiki kwenda kula nikashangaa namuona na mwenzangu (Mshana) ambaye naye alitoroka nikaunganishwa naye,” alisema.
Kwa upande wake Mshana, alisema naye alisimamishwa na kuamriwa ashuke kwenye gari na kukabidhi kila kitu ikiwemo hati yake ya kusafiria na simu. Aliunganishwa na wenzake aliowakuta tayari wametekwa na kuongozwa kuelekea porini huku wakiwa wamefungwa mikono.
Alisema katika msafara huo, mmoja wa askari alitangulia mbele na wengine walifuatia nyuma na kuongozwa kwenye pori zito ambalo wakati mwingine walilazimika kutembea kwa magoti kwani haikuwezekana kutembea huku umesimama.
“Tulipotembea kama kilometa 13 ikabidi nimwambie mwenzangu (Athuman Fadhil) kwamba tutafute njia ya kujiokoa. Hata hivyo alinijibu kwamba kuwa yeye hawezi kwa kuwa amevaa nguo inayomtambulisha zaidi endapo akitoroka itajulikana na wenzetu watapata shida,” alisema.
Alisema walitembea mbele kidogo ndipo alipobaini umbali kidogo kati yake na askari ambapo pembeni yake kulikuwa na kinjia cha kujipenyeza ndipo alipoamua kutambaa kwa magoti na kujipenyeza kwenye kinjia hicho na kufanikiwa kujificha bila kuonekana.
Alisema mara baada ya wenzake kupita alianza safari kwenye pori hilo bila kujua anakokwenda mpaka alipofanikiwa kukutana na kikosi cha Polisi ambacho kilimchukua na kumpeleka sehemu salama.
Athuman Fadhili ambaye alitekwa hadi kuokolewa na majeshi ya DRC, alisema baada ya mwenzake kutoroka alipata matumaini kuwa atasaidia kuwaletea msaada hivyo waliendelea na safari kama kilometa 30 zaidi kwenye msitu huo mnene.
Alisema katika safari hiyo ya mateso ya siku mbili walitembea usiku na mchana huku wakichanwachanwa na miba, walifika kwenye eneo la kijiji ambacho hata hivyo kilikuwa na nyumba chache, wakaamriwa watembee kwa kutambaa ili wasionekane na wanakijiji hao.
Baada ya kilometa tano kutoka kwenye hicho kijiji walifika kwenye makazi ya muda ya watekaji hao na kukutana na mkubwa wao aliyejitambulisha kama Shehe Hassan aliyeamuru wapewe maji na kuanza kuwahoji majina yao kupitia hati zao za kusafiria na kutaka kujua kuhusu familia zao.
Walibeba mizigo ya waasi
Alisema wakiwa katika eneo hilo, mmoja wa viongozi wa watekaji hao aliyekuwa akizungumza kwa simu na bosi wao mwingine alitoa taarifa kuwa majeshi ya DRC yanawafuatilia hivyo wanatakiwa kujihadhari.
Baada ya mahojiano hayo walipewa chakula na maji na kisha giza lilipoingia walitafutiwa eneo la kulala ambalo ni hema lililowekewa turubai. Alisema majira ya saa sita au saa saba usiku huku mvua kubwa ikiwa inanyesha, waliamshwa na kutakiwa kuendelea na safari kwa kuwa hali ya usalama katika eneo hilo ni tata kutokana na majeshi ya DRC kuzidi kuwakaribia.
“Tulikuwa tumechoka sana kutokana na kubeba mizigo yetu na yao safari nzima lakini tulilazimika kutembea tu. Ilifikia mahali tulitamani kupigwa hata risasi ili tupumzike na kuondokana na mateso tuliyokuwa tunayapata,” alisema Fadhili.
Walitaka dola 4,000 kutoka kwa Dewji
Alisema wakati wakiendelea kutembea, viongozi wa watekaji hao waliendelea kuwasiliana njia nzima na bosi wa Simba Logistics, Azim Dewji na kumpa saa 24 awe ametoa dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva ili waachiwe huru.
“Lakini baadaye wao wenyewe wakaanza kubishana juu ya namna ya kuzipata fedha hizo kutokana na hali halisi ya msitu huo. Wakaambizana fedha hizo zipelekwe kupitia helikopta ya kampuni walikoshushia mzigo wa saruji na madereva hao wapepee bendera kuonesha wako salama na fedha hizo zidondoshwe,”alifafanua.
Alisema walitembea tena umbali kidogo ndipo waliposimama na kupewa chakula aina ya ugali wa mhogo uliokuwa umejaa michanga pamoja na mboga za majani wasiyoyajua na kulazimika kula tu kwa kuwa walikuwa na njaa.
Fadhil alisema waliendelea kubaki katika eneo hilo kwa muda, ndipo watekaji hao walipomtuma kijana wao akanunua unga mjini, baada ya muda alirejea akiwa anatweta na kuwataarifu kwa taharuki kuwa majeshi ya DRC yamekaribia eneo hilo.
Madereva wagawanywa kwa waasi
Kutokana na taharuki ya viongozi hao, kila mtekaji alipewa madereva wawili mpaka watatu awaongoze na kuanza kukimbia huku watekaji hao wakiwa wametangulia mbele.
“Walionesha kuchanganyikiwa kwa kweli wakaanza kutufokea huku wametushikia mitutu ya bunduki na kila kundi likaenda upande wake. Kwa kuwa wao ndio waliotangulia, tukaanza kutoroka mmoja mmoja mpaka kwenye kundi letu tukabaki wawili mimi na Issa,” alisema.
Alisema baada ya kubakia wawili wakaamua pia na wao watoroke kwani hali ilikuwa tete hivyo wakajitosa msituni na kuanza kukimbia hadi waliposikia sauti za maaskari wa DRC zikiwaita.
“Tulisikia wakituita kwa lafudhi yao ya kikongo, watanzania kuya (kuja) watanzania kuya (kuja) jitokezeni sisi ni jeshi la DRC tumewaokoa. Sikuamini masikio yangu tulijitokeza na kupewa msaada haraka,” alisema.
Dewji, Serikali ya Tanzania na Congo wazungumza
Kwa upande wake, Dewji alilishukuru jeshi la DRC na Serikali ya Tanzania kwa kuwa naye bega kwa bega katika harakati za kuwaokoa madereva hao na kubainisha kuwa katika tukio hilo, magari ya kampuni yake ya Simba manne yalichomwa moto na hivyo kupata hasara ya Sh milioni 600.
Alisema alikuwa akiwasiliana na waasi hao kila mara wakimtaka atoe fedha hizo ambazo alikuwa tayari kuzitoa lakini alionywa na jeshi la DRC kuwa endapo atazitoa atawajengea tabia ya utekaji zaidi wanajeshi hao.
Aidha, Dewji alisema Serikali ya DRC imemuahidi kuwa itaendelea kuweka usalama kwa wafanyabiashara wa malori nchini humo na kumhakikishia ulinzi wa doria kila kampuni hiyo itakaposafirisha mizigo yake nchini.
“Hiki kilichotokea ni bahati mbaya, tutaendelea na biashara lakini kwa tahadhari. Biashara yangu inagusa watu wengi si kampuni yangu pekee endapo nitasitisha wengi wataathirika,” alisisitiza.
Balozi wa DRC nchini, Jean Piorre Mutamba, alisema tukio hilo limemshtua na kumpa wakati mgumu, hasa ikizingatiwa kuwa ni balozi mpya aliyewasili nchini hivi karibuni, hivyo alitumia fikra zake zote ili kuhakikisha madereva hao wanaokolewa.
Aliwataka madereva hao kuhakikisha wanawasiliana na ubalozi wa DRC kabla ya kuanza safari ili kuwawekea mazingira ya usalama zaidi na kuwafuatilia.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Susan Kolimba, aliwahakikishia madereva hao kwamba tukio hilo ni la bahati mbaya na kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuwalinda wananchi wake wanaofanya kazi nje ya nchi.
Post a Comment