Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Japan yakoshwa na utendaji wa Serikali ya Magufuli ... Yaahidi kuiongeza ruzuku Tanzania

SERIKALI ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA) imeahidi kuongeza kiwango cha ruzuku kwa Serikali ya Tanzania ili kufadhili miradi ikiwemo kilimo, maji, miundombinu ya barabara na huduma nyingine za jamii ili kuisaidia kufikia maendeleo yaliyokusudiwa kwa wananchi wake.

Ahadi hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Hiroshi (Hiro) Kato alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango jijini Washington D.C nchini Marekani.

Kato alisema Tanzania na Japan ni marafiki wa muda mrefu na kwamba nchi hiyo itaendelea kuisaidia kwa kutekeleza miradi mbalimbali yenye kuleta tija kwa uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania kwa ujumla.

“Hivi sasa tunataka kuanza kutekeleza awamu nyingine ya mradi wa kilimo cha umwagiliaji cha zao la mpunga ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambalo ni muhimu sana,” alisema Kato.

Alisema Japan pia imeamua kuongeza kiwango cha ufadhili kwa Bara la Afrika kutoka Dola milioni 13 ambazo nchi hiyo ilikuwa ikitoa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2013 hadi kufikia dola 30,000 kwa mwaka kuanzia Agosti, 2016 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Alisema pia kuwa ili kuwajengea uwezo na ujuzi vijana wa Kiafrika, Japan imeanzisha programu ya kutoa elimu ambapo hivi sasa vijana 60 kutoka nchi mbalimbali za Kiafrika wamepelekwa nchini humo kujifunza kwenye vyuo vilivyoko huko na watapelekwa kwenye kampuni na mashamba makubwa yanayojihusisha na kilimo ili wapate uzoefu na kuwa chachu ya mabadiliko watakaporejea katika nchi zao.

Kwa upande wake, Dk Mpango aliishukuru Japan kwa kuisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Alitaja baadhi ya miradi ambayo nchi hiyo inafadhili nchini Tanzania kuwa ni ujenzi wa barabara ya Arusha-Holili hadi Taveta nchini Kenya, ujenzi wa barabara ya Juu (Flyover) ulioanza eneo la Tazara ili kupunguza msongamano jijini Dar es Salaam, miradi ya maji na kilimo cha umwagiliaji.

“Asilimia 75 ya wananchi wetu wanategemea kilimo kwa hiyo uamuzi wa Japan wa kuwekeza fedha nyingi kwenye miradi ya kilimo cha umwagiliaji ni jambo tunalolipongeza kwa sababu kilimo kitakuwa na tija na kitaendeshwa kibiashara,” alisema Dk Mpango.

Ameishukuru pia Serikali ya Japan kwa kufanya utafiti na upembuzi yakinifu wa mradi wa kudhibiti mafuriko ya Mto Kondoa, eneo la mkoa wa Morogoro ili kudhibiti mto huo usiharibu miundombinu ya Reli ya Kati.

“Mradi huu ni muhimu sana kwa sababu serikali imekuwa ikiingia hasara karibu kila mwaka kukarabati njia hiyo ya reli baada ya kusombwa na maji, hivyo tunaishukuru Japan kwa kutusaidia kufanya utafiti huo ambao utasaidia kukabiliana na hali hiyo,” aliongeza Dk Mpango.

Ameahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kukusanya kodi na kuziba mianya ya upotevu wa fedha za serikali ikiwemo kuanzisha mahakama maalumu ya kushughulika na mafisadi ili kuleta nidhamu katika utumishi wa umma.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top