Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Mkuu wa wilaya awasweka rumande madiwani wa CCM

Zikiwa ni takribani wiki mbili tangu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, Alexander Mnyeti kuwaweka ndani madiwani wanne wa Chadema kwa madai ya kumkwamisha kutekeleza kazi zake, Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zephania Chaula naye amewasweka mahabusu madiwani wawili wa CCM. 

Chaula amewaweka ndani madiwani hao akiwamo wa Kata ya Emboreet, Christopher Ole Kuya na wa Viti Maalumu, Diana Kuluo kwa madai ya kuvunja ofisi ya Kijiji cha Emboreet na kushinikiza wananchi kuandamana ili kumpinga mwenyekiti wa kijiji hicho. 

Chaula alitoa amri ya kukamatwa kwa madiwani hao baada ya kuona wanaongoza kuharibu usalama kwenye eneo hilo.

Alisema madiwani hao waliwaongoza baadhi ya wanakijiji kuvunja ofisi ili kumshinikiza mwenyekiti wa kijiji hicho, John Olendikoni kujiuzulu na kusababisha waandamane kumpinga. 

Mkuu huyo wa wilaya alisema alichukua hatua hiyo baada ya vyombo vya ulinzi na usalama kumpa taarifa kuwa madiwani hao wanaongoza harakati za kumng’oa madarakani mwenyekiti wa kijiji bila kufuata taratibu na sheria. 

“Sitakubali kuona kiongozi yeyote hata kama ni kupitia CCM anafanya makosa, kisha nikamuacha kwani suala la kumtaka mwenyekiti wa kijiji ajiuzulu lina taratibu zake siyo kumwambia atoke kwenye kiti,”alisema Chaula. 

Alisema, awali aliwaeleza wahusika kuvuta subira juu ya suala hilo na kufuata taratibu kupitia vikao, ili kubaini tatizo lililopo kwa madai kwamba siasa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 vimeingizwa kwenye suala hilo. 

“Nimeshawaagiza watengeneze mlango na vyombo vyote vilivyoharibika kwenye ofisi hiyo walipovunja na nimewapa taarifa kuwa nitawachukulia hatua wananchi wakiandamana tena,” alisema mkuu huyo wa wilaya. 

Alisema amewaambia madiwani hao mchakato na taratibu za kumtoa mwenyekiti wa kijiji zinaanzia halmashauri ya kijiji, mkutano mkuu wa kijiji, taarifa kwa mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa.

 “Tunafanya kazi kwa utaratibu siyo shinikizo na nimewapa angalizo wawe viongozi wa kuwapo kwa amani katika eneo hilo na yakizuka mengine nitawaweka ndani tena kisha mahakamani,” alisema. 

Akizungumza baada ya kuachiwa kwenye Kituo cha Polisi Orkesumet, Ole Kuya alisema hawakuwashinikiza wananchi kuandamana ili kumkataa mwenyekiti na kuvunja ofisi ya kijiji. 

“Sisi hatuhusiki kwenye kuongoza harakati hizo, ila ni wananchi wenyewe wameamua kupambana kwa ajili ya kudai haki zao baada ya kuona uongozi wa kijiji unafanya mambo ambayo hawaridhiki nayo,”alisema Ole Kuya. 

Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 kinawapa mamlaka mkuu wa mikoa na wilaya kumuweka ndani mtu kwa saa 48 pale anapobaini mhusika ametenda kosa.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top