Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Sakata la Afande Sele lachukua sura mpyaHivi majuzi, paliibuka mjadala mpana mitandaoni kufuatia makala fupi iliyoandikwa na mwamuziki galacha hapa nchini, ambaye pia ni mwanachama wa chama cha ACT- Wazalendo, ndugu Afande Sele, akitoa maoni yake kwa kuwalalamikia baadhi ya wanachama na viongozi wa chama chake hicho, kwa kile anachoamini yeye kwamba wanam-suport Prof Ibrahim Lipumba.

Vijana wengi wasiyo wafuasi wa ACT, walionekana kupendezwa sana na hoja za Afande kiasi cha kui-share kwa wingi Makala ile, na kuweka comments za kutosha. Niliona majibu ya baadhi ya wana-ACT mitandaoni; wengi wao wakisema wanayaheshimu maoni ya Afande, na kwamba watayafanyia kazi, na wengine ambao hawakukubaliana na hoja zake, walimpinga kwa hoja vilevile. Hilo likawa limekwisha.

Baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia ulioandaliwa na ACT- Wazalendo, Afande Sele akaibukia tena, safari hii aki-post sauti yake (Audio) kwenye group la WhatsApp akiendeleza kuwalalamikia tena watu walewale, kwa suala lilelile.

Na hapa ninanukuu baadhi ya maneno yake;
"Ninazungumza yale ambayo niliyopaswa niyazungumze jana kwenye mkutano wa kidemokrasia, kama unavyoitwa, ni mkutano ambao tulisema tunaalika watu wa aina zote, kwahiyo jana ulifanyika, kuna watu walifika, lakini naamini pia kuna watu ambao hawakufika. Na humu kwenye group kuna watu wa aina zote, kwahiyo labda kwa maoni, kwa sababu jana miye sikuwepo pia, sikuwa mwalikwa, ninaweza nikaja tukajadili mambo yangu kwa pamoja..."

Aidha aliongezea katika audio yake hiyo iliyosambaa mno mtandaoni, kwa kusema, "Hata kama ningekuja jana, ningelialikwa, ningeyauliza jana, lakini kwakuwa jana sikualikwa, tunaweza kujadiliana humu kwa pamoja. Pia nisisitize kwamba, ni kuhusu maoni yangu, mimi ni mwanachama wa kawaida, si kiongozi."
Tukianzia hapo, nami acha nitoe maoni yangu kama mfuatiliaji tu wa kawaida.

Ninahisi Afande Sele ana zaidi ya maoni nyuma yake, ninahisi hivyo kutokana na namna ya uwasilishaji wake na ujengaji wake wa hoja. Ukiwa ni mtu makini utabaki na maswali mengi kuliko majibu toka kwenye hoja za mwanamuziki huyo wa zamani;

Kwa maneno yake mwenyewe, Afande anakiri kwamba waliuandaa Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia kwa ajili ya watu wote, na hata yeye ni mmoja kati ya wana-ACT walio-post tangazo la mkutano ule mtandaoni akishiriki kuwaalika wengine, na kwakuwa mkutano ulitoa fursa kwa mtu yeyote kuuliza chochote ikiwa ni pamoja na kushauri ima kukosoa lolote, hivyo wengi walitaraji kumsikia Afande akihoji, kukosoa na kushauri, lakini isivyo bahati hata mkutanoni hakutokea.

Ghafla ameibukia WhatsApp na kudai kwamba hakufika kwa sababu hakualikwa. Ninajiuliza, alitaka kualikwa kama nani ilhali anajipambanua kama mwanachama wa kawaida? Na tunajua taarifa ya mkutano kwa wanachama wa kawaida na wasiyo wanachama, ziliwafikia kupitia matangazo ya mitandaoni na kwingineko!

Tukirejea kwenye mada ya msingi, katika kujenga hoja yake katika hilo group la WhatsApp, huku akisisitiza kwamba yale ni maoni yake binafsi hivyo yaheshimiwe, Afande Sele aliwalalamikia baadhi ya wanachama na viongozi wa chama chake, ambao kwa mtazamo wake wameonesha kuunga mkono upande wa Prof Lipumba badala ya ile wa akina Maalim Seif.

Afande anaamini kwamba Lipumba hana wafusi wengi, na ndiyo maana hata alipoamua kujiuzulu uongozi wa chama cha wananchi CUF bado CUF chini ya mwamvuli wa UKAWA ilipata wabunge wengi, hii ni ishara (kwa mujibu wa Afande) kwamba Lipumba hana wafuasi wengi.

Kwa sababu hiyo, Afande anajaribu kujenga hoja kwamba, kwakuwa ACT- Wazalendo inahitaji wanachama wengi wapya kutoka katika vyama vingine, hivyo katika makundi haya mawili yanayosigana ndani ya CUF, Mwanachama wa ACT hapaswi kuunga mkono upande wa Prof Lipumba kwakuwa hana wafuasi wengi ambao ACT inaweza kuwavuna, hii ndiyo kusema kwamba Afande, anawataka wana-ACT wachague upande wa akina Maalim Seif (UKAWA) kwakuwa wanao wafusi wengi ambao Afande anaamini ACT- Wazalendo itawapora (kama alivyolitumia neno hilo, yeye mwenyewe kwenye Audio yake).

Kwa maoni yangu, kwanza nafikiri Afande amesahau tu kwamba Lipumba hakuhama chama cha CUF, na wala hakumtaka mwanachama ye yote wa CUF asimpigie kura Mbunge ye yote wa CUF (UKAWA), Hivyo kuupima ushindi wa wabunge WA CUF dhidi ya Lipumba ambaye aliendelea kuwa mwanachama wa CUF, sidhani kama ni kipimo stahiki. Pia inaonekana dhahiri kwamba hoja ya Afande si kukataza kuingilia mgogoro wa ndani wa CUF ili kujinufaisha, bali hoja yake ya msingi ni hofu ya kushindwa kwa ACT kujinufaisha kupitia mgogoro huo kwa kuchagua upande wa Lipumba kwa sababu tu hana wafuasi wengi ambao ACT itawavuna.

Kama hivyo ndivyo, basi alipaswa kutuambia, kwamba kwa vipi ACT itawapora hao wanachama na wafuasi wa CUF endapo watachagua kuunga mkono upande wa Maalim Seif? Kwa maana licha ya kwamba siioni namna ya kufanikisha huo mpango wa kimiujiza anaoufikiria Afande wa kuunga mkono upande wenye wafuasi wengi ili baadaye ati uwapore wanachama wa upande huo, lakini pia hilo ni kinyume cha msimamo wa chama, ambao uliwekwa hadharani na Kiongozi wa chama hicho, ndugu Zitto Kabwe, pale alipoalikwa na Clouds Tv, katika kipindi cha360, alitanabahisha kwamba vyama vya siasa havipaswi kuingilia mgogoro huo ambao kwa maneno yake Zitto, unafifiza jitihada za Zanzibar kudai haki ya uchaguzi uliofutwa. Kwakuwa hoja ya Afande Sele imekuja baada ya msimamo huo wa chama chake, ni dhahiri hafuatilii misimamo na matamko rasmi ya chama chake, au pengine anachukua mawazo ya mtu mmoja mmoja na kufikiri kwamba ule ni msimamo wa chama ...

Kwa sababu analalamikia kitu ambacho chama chake pia hakikikubali.
Nilipata wasaa wa kuhudhuria Mkutano Mkuu huo wa Kidemokrasia ambapo nilibahatika kumsikiliza Prof Kitila aliposisitiza kwamba ACT kama chama hawapaswi kusubiri makosa (migogoro) ya vyama vingine ndipo wao wanufaike, huku akisisitiza kwamba hata kama ikitokea yakaibuka makosa ya chama kingine (hapo akimaanisha CCM, basi itakuwa ni bonus tu. Pengine hata hili Afande Sele hakulijua kwakuwa hakuhudhuria mkutanoni.

Maoni yangu yamejikita kwenye suala hili la maoni ya Afande kuhusu mgogoro wa ndani ya CUF kwa sababu ndilo eneo 'la moto' kwa masiku haya. Waaidha, sijataka kujadili maoni yake mengine aliyoyatoa kuhusu kwanini viongozi wa ACT mara wamponde Rais Magufuli kwa jambo hili na mara wamsifie kwa jambo lingine, kwa sababu hilo ni jepesi mno, kwa muungwana hauwezi kuponda kila kitu au kusifia kila jambo. Chukua mfano, katika Audio hiyo, Afande Sele anawatuhumu viongozi wa ACT kwa kumuunga mkono Maalim Seif katika suala la Uchaguzi wa Zanzibar, halafu wanaonekana kumuunga mkono Lipumba asiyekubaliwa na Maalim Seif na Wazanzibar walio wengi.

Yaani Afande hajui kwamba kadhia ya Uchaguzi wa Zanzibar ni jambo moja, na mgogoro wa kimadaraka ndani ya CUF ni jambo jingine, hivyo mtu aweza kuamua kuunga mkono moja na kulipinga jingine. Kama analijua hilo, basi yamkini kwamba Afande anataka ukiamini Maalim Seif hakutendewa haki kwenye Uchaguzi wa Zanzibar, ni lazima umuunge mkono tu hata kwenye masuala ambayo anakosea ... Hii ni Hatari kwa taifa.

Cha ajabu sasa, huyohuyo Afande Sele, anayetaka ACT waunge mkono upande wa CUF (UKAWA), ambao wanampinga Rais Magufuli karibu kwa kila jambo, ameibuka na kumuunga mkono Rais Magufuli na kutaka aachiwe aendelee kutawala hata katika awamu zijazo kwa sababu yeye (Afande) anaamini Rais Magufuli anafaa sana. Sasa hapo utajiuliza, yeye anawalaumu wengine kwa lipi na yeye sasa anatenda lipi.
Haya ni maoni yangu mimi Maundu Mwingizi, na mwingine anaweza kutoa maoni yake zaidi.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top