Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Tanesco yajibu mapigo ya Muhongo

SIKU chache baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kueleza kiu ya serikali ya kuona nchi inaondokana na mgawo wa umeme, kudhibiti kukatikakatika kwa umeme, kuzalisha umeme wa uhakika na unaotabirika kwa maendeleo ya viwanda, lakini pia kuwa na umeme nafuu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limekuja na majibu ya hoja hizo, huku likisisitiza kuwa umeme utapanda kwa wateja wa kati na si wa chini.

Majibu hayo yalitolewa juzi usiku kwenye kipindi cha Kipima Joto kinachorushwa hewani na Kituo cha televisheni cha ITV na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco Felchesmi Mramba, huku akishuhudiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi, aliyetoa pia ufafanuzi wa masuala kadhaa.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja kupita tangu Ewura ilipopokea maombi kutoka Tanesco ya kutaka kuongeza bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 18.19 kwa mwaka 2017.

Katika maelezo yake ya juzi usiku, Mramba alisema kutokana na shirika hilo kuwajali wateja wa kipato cha chini, wateja hao hawataathirika na mapendekezo ya bei mpya, na badala yake watabakia na bei iliyopo sasa.

Mkurugenzi huyo pia alisisitiza kuwa shirika hilo halina mpango wa kurudisha tozo ya kuunganishiwa umeme ya Sh 5,000 na gharama ya huduma kwa kila mwezi ya Sh 5,520 ambazo ziliondolewa mwezi Aprili mwaka huu. Mapendekezo ya kupandisha bei ya umeme

Akifafanua mapendekezo hayo, Mramba alisema bei za umeme zinazotumika, zinatakiwa kutumika hadi Desemba 31, mwaka huu na baada ya hapo Januari mwakani sheria inataka bei mpya zitolewe. Alisema pamoja na mapendekezo hayo, walichoomba ni kuongezeka kwa bei kidogo ambayo haiwezi kuwaumiza wananchi, bali itaboresha zaidi huduma na kufanya wazipate kwa uhakika kama alivyoagiza Waziri Muhongo.

“Tanesco ilitakiwa kufanya tathmini ya gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme na kupeleka mapendekezo hayo Ewura, ili kupitiwa na wadau, sasa suala la kupanda au kushuka kwa bei itategemea na mapitio ya tathmini ya gharama za kuzalisha, kusafirisha na kusambaza tulizowasilisha Ewura,” alisema Mramba.

Akizungumzia kuhusu kuondolewa kwa tozo ya gharama za kila mwezi pamoja na tozo ya kuunganishiwa umeme kwa wateja wapya, Mramba alisema katika mapendekezo hayo tozo hizo hazipo na wala hawana mpango wa kuzirudisha na kwamba wateja wa chini wao wataendelea kununua umeme kwa bei iliyopo sasa.

“Tulishaziondoa ili wananchi waweze kupata umeme kwa bei nafuu na hatuna mpango wa kuzirudisha kwa sasa na hata katika mapendekezo yetu wateja wa kima cha chini wao hawataathirika, tunawajali wataendelea na bei ya sasa,” alisema Mramba.

Alisema kilichofanyika ni mabadiliko kidogo hasa kwa wateja wa kati na wengine ambao wamependekeza bei ipande kidogo ili waweze kutoa huduma bora zaidi kama inavyotakiwa.

Umeme wa viwanda Akizungumzia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, Mramba alisema hadi sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazotoza gharama ndogo za umeme wa viwandani.

Alisema hivi sasa tozo za umeme wa viwandani nchini ni kiwango cha senti 6.9 ya dola za Kimarekani kwa uniti moja, wakati nchi nyingine za Afrika Mashariki tozo zipo juu. Akifafanua hilo Mramba alisema Rwanda wanatoza uniti moja ya umeme wa viwandani kwa senti 23 za Dola za Kimarekani, Kenya na Burundi wanatoza senti 8, huku Uganda wakitoza senti 12 za Dola za Kimarekani kwa uniti moja.

Akizungumzia mapendekezo yaliyowasilishwa Ewura, Mramba alisema wameomba tozo ya viwanda iongezeke kutoka senti 6.9 hadi 8 bei ambayo hata hivyo bado itakuwa chini ukilinganisha na tozo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki ukiondoa Kenya na Burundi.

“Pamoja na kupendekeza kuongezeka kwa tozo ya umeme wa viwandani kutoka senti 6.9 hadi 8, bado Tanzania itakuwa nchi inayotoza gharama kidogo na hii itawezesha nchi kuelekea kwenye uchumi wa viwanda,” alisema Mramba.

Aidha alisema katika mapendekezo hayo waliwasilisha kutofautisha wateja baina ya wateja wadogo wa nyumbani na wateja wa viwanda vidogovidogo ambapo awali wote walikuwa kwenye kundi moja.

“Tumewasilisha mapendekezo ya kutenganisha wateja wadogo wa nyumbani na wale wa viwanda vidogo, ambao awali walikuwa kwenye kundi moja, hii itasaidia kuondoa kero ya tozo kwa wateja hao, na sasa watalipa kutokana na matumizi yao,” alisema Mramba.

Alisema dhana kuwa Tanesco ndiyo walioamua kuwasilisha mapendekezo ya bei ya umeme si sahihi na kwamba bei hizo hazijaanza kutumika kwani Tanesco haina mamlaka ya kufanya hivyo na kuongeza kuwa ombi hilo la mabadiliko ya bei limewasilishwa kulingana na agizo la kubadilisha bei za umeme la mwaka 2016.

Katika agizo hilo, bei hizo zilizoanza kutumika Aprili Mosi mwaka huu, zinatakiwa kubadilika mwaka 2017 na kwa mujibu wa Sheria, Ewura iliiagiza Tanesco iwasilishe ombi la mabadiliko ya bei ya umeme kwa mwaka 2017, ambayo ndiyo hayo yaliyowasilishwa.

Ngamlagosi alisema wamepokea ombi la mapendekezo ya Tanesco ya kurekebisha bei ya umeme hadi kufikia asilimia 18.19 kwa mwaka 2017 na kwamba wajibu wao kwa mujibu wa sheria ni kukusanya maoni ya wadau ili kupata mapendekezo yao kabla ya kutoa uamuzi.

Ngamlagosi alisema wamepokea mapendekezo yenye sehemu kuu tatu, moja ni kupanda kwa asilimia 18.19, pili ni kugawanya kundi la wateja wa kawaida wa nyumbani na pendekezo la tatu ni kuwepo kwa kundi la wafanyabiashara wadogo, wateja wa mabango na minara ya simu ili mtumiaji mdogo wa nyumbani asiumie kwa kuwekwa kwenye kundi la watumiaji wa umeme wa viwanda vidogo.

Alisema Tanesco imeomba kundi hilo livunjwe kwenye makundi mawili ili kuwe na kundi la watumiaji wa kawaida wa umeme wa nyumbani ambao awali walichanganywa na viwanda vidogovidogo.

“Tunao wajibu wa kuisikiliza Tanesco kama mteja wetu, na baada ya kupitia ombi lake na kukidhi vigezo tulitangaza ombi hilo kwenye gazeti la serikali kuhusu kutoa maoni, na tumeshafanya hivyo na tumeshakusanya maoni mengi kutoka makundi tofauti hata wauzaji umeme wa Tanesco,” alisema Ngamlagosi.

Alisema maombi hayo yalipokelewa Novemba 4, mwaka huu na waliyapitia na kuona yanakidhi vigezo na wakaitisha mikutano ya wadau kutoa maoni yao kuanzia Novemba 16 na kwamba Novemba 25, mwaka huu watafunga pazia la kupokea maoni.
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top