CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hadi sasa hakijui alipo msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Ben Saanane.
Kimevitaka vyombo vya dola, kuchukua hatua za haraka kuhakikisha msaidizi huyo anapatikana haraka.
Saanane inadaiwa alitoweka katika mazingira ya kutatanisha tangu Novemba 18, mwaka huu. Juhudi za kumtafuta katika vituo vya polisi, hospitalini na vyumba vya kuhifadhia maiti, zimefanyika bila mafanikio.
Kauli hiyo imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Saanane ambaye hajulikani aliko.
Alisema hata wao hawajui alipo, hawafahamu kama yuko hai au ameshikiliwa mahali. Kwamba wanachokijua ni kwamba hawajui aliko.
“Katika mazingira haya, tunaiomba serikali na vyombo vyake vya ulinzi, ituambie kama imemkamata na inamshikilia Ben Saanane tuanzie hapo…lakini kama hawajamkamata na hawamshikilii, serikali na vyombo vyake watueleze mawasiliano yake ya mwisho yalikuwa lini, na nani, wapi na yalihusu nini,” alisema.
Alisema kwa kuwa serikali ndiyo yenye udhibiti wa mipaka yote nchini, iwaeleze kama kuna rekodi yoyote inayoonesha Ben aliondoka nchini kwa kupitia mipaka hiyo, kama ni mipaka ya nchi kavu, majini au viwanja vya ndege.
Katika hatua nyingine, alisema pamoja na majibu hayo, lakini pia wanaitaka serikali pamoja na vyombo vyake vya dola, kufukua miili ya watu waliokufa katika mto Ruvu na ifanyiwe uchunguzi ili wajulikane watu hao ni akina nani, ili isije kuwa miongoni mwa watu hao ni Saanane.
Lissu alisema kuwa mawasiliano ya mwisho kati ya Saanane na Mbowe, yalikuwa ni Novemba 14, mwaka huu wakati Saanane akiwa Dar es Salaam na mwenyekiti huyo akiwa Dodoma.
“Alimwambia mwenyekiti uko wapi, akamwambia nakwenda kwenye maziko ya Samuel Sitta, mawasiliano ya mwisho ni ya tarehe 14 Novemba,” alisema Lissu.
Alisema pamoja na kwamba Saanane alikuwa ni msaidizi wa Mbowe katika masuala ya kisiasa na kijamii, lakini hakuwa akitembea na mwenyekiti huyo na kwamba shughuli zake alikuwa akifanyia katika Makao Makuu ya chama hicho.
Lissu alisema kuwa wapo watu wanahoji inawezekanaje Mwenyekiti hajui mahali alipo msaidizi wake, lakini wanapaswa kufahamu kuwa Mbowe hakuwa akitembea na Saanane.
Alisema baada ya maziko ya Sitta, viongozi wote wa chama hicho walikuwa wakizunguka katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kufanya shughuli za chama, lakini katika kipindi chote hicho, mwenyekiti huyo hakuwa na msaidizi wake huyo, kwa kuwa hatembei naye na si jambo la ajabu.
“Baada ya hizi ziara, tulienda nchi za nje…katika kipindi chote hiki Mwenyekiti hakuwa na Ben na vilevile nataka niweke hii vizuri, Mwenyekiti hakupata wasaa wa kusema Ben yuko wapi, kwa sababu hatembei naye, hayuko naye muda wote.”
“Sasa kuna watu wanaosema Mwenyekiti ndiye anayejua, atuambie yuko wapi, Mwenyekiti hajui, mimi sifahamu aliko Ben, tungekuwa tunafahamu tungeshasema,” alisema.
Alisema kwa mara ya kwanza alipigiwa simu na mdogo wake Ben, aliyemtaja kwa jina la Dorice Desemba 4, lakini hakumpata na alimtumia ujumbe kumwambia kuwa kaka yao Ben amepotea, hawajui aliko na alikuwa akitaka ushauri ambapo alimjibu waliripoti jambo hilo polisi na kwenye vyombo vya habari.
Alisema si kwamba wamenyamaza kimya, kwa kuwa wanajua alipo msaidizi huyo na kwamba watu wanaodai hivyo si sahihi.
Alitaka mtu yeyote mwenye taarifa kuhusu Saanane alipo, azitoe taarifa hizo hadharani, polisi, kwenye chama, vyombo vya habari au kwa ndugu zake.
Post a Comment