Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), inatarajia kukutana Desemba 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam, imefahamika.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Msemaji wa chama hicho, Seleman Mwenda, ilisema mkutano huo utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu (CC), kitakachofanyika Desemba 11 hadi 12, jijini Dar es Salaam.
Ingawa hadi sasa ajenda za vikao hivyo hazijajulikana, lakini wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, kufanyika kwa vikao hivyo kunatajwa kuwa ni mkakati wa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli kutaka kuisuka upya CCM.
Baadhi ya wachambuzi hao wanasema uteuzi wa wajumbe watatu wa sekretarieti ya chama hicho kuwa mabalozi ni mwendelezo wa mkakati huo kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho mwakani.
Mbali na hao mjumbe mwingine wa sekretarieti, Dk Asha -Rose Migiro aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na nafasi yake ndani ya chama kuchukuliwa na Pindi Chana ambaye naye ameteuliwa kuwa balozi.
Katika Serikali ya awamu ya nne, Pindi Chana alikuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na baadae mwaka huu aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Dk. Emmanuel Nchimbi, kuteuliwa kuwa balozi kunathibitisha kuhusu uwapo wa mkakati wa Rais Magufuli kusuka upya chama hicho kwa kuweka sura mpya.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye pia ni Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa chama hatarajiwi kuwapo katika safu hiyo mpya, kwani tayari yupo serikalini.
Mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Bara), Rajabu Luhwavi ambaye ameteuliwa kuwa balozi anazidi kutoa taswira kuhusu mkakati wa Rais Magufuli kusuka upya chama hicho.
Katika hotuba ya Rais Dk. Magufuli baada ya kukabidhiwa uenyekiti wa chama hicho alisema miongoni mwa mambo atakayoyatekeleza ni kuimarisha utendaji kazi wa chama, huku akimnukuu hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa kusema kuwa chama legelege huzaa serikali legelege.
“Nitashirikiana nanyi kujenga chama madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri Serikali ili itekeleze ipasavyo majukumu yake, ikiwezekana tutapitia upya katiba na kanuni zetu ili kukidhi mazingira ya sasa na kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo.
“Tutahakikisha pia tunakuwa na safu bora ya uongozi katika ngazi zote kuanzia shina hadi taifa. Tutaangalia muundo (structure) wa chama chetu katika ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyokuwa na tija katika chama na hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Magufuli alihoji kuhusu uhalali wa kuendelea kuwapo vijana wa chipukizi ndani ya chama hicho pamoja na baadhi ya safu za uongozi ndani ya chama hicho.
“WanaCCM ni lazima tujiulize je ni kweli katika zama hizi bado tunahitaji mtoto wa miaka 8 hadi 15 kuwa chipukizi kwa ajili ya kumtumia kwenye siasa badala ya kumwacha asome? Kama akiwepo chipukizi wa CCM, chipukizi wa NCCR au Chadema ama TLP tutakuwa tunajenga nchi ya namna gani?
“Je bado kuna umuhimu wa kuwa na makamanda wa vijana ambao mara nyingi wenye kupewa vyeo hivyo ni wale wenye uwezo wa kifedha pekee? Je walezi kwenye Umoja wa Wanawake (UWT) bado wanahitajika? Je washauri ndani ya Jumuiya ya Wazazi wanahitajika?" Alihoji Dk. Magufuli.
Post a Comment