Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefanya mazungumzo na mfanyabiashara tajiri kuliko wote Afrika, Alhaji Aliko Dangote anayemiliki kiwanda cha saruji kilichopo Mtwara na wawili hao wamepeana ahadi zitakazonufaisha pande zote mbili.
Wawili hao wamekubaliana kuwekeana mazingira mazuri ya kufanya kazi, kuendelea na uzalishaji, kutumia malighafi ya hapa nchini kama makaa ya mawe, kutumia gesi asilia, na kuleta malori 600 yatakayofanya kazi ya kusambaza saruji, ikiwa ni sehemu ya maazimio ya mkutano wa jana.
Dangote amekuja nchini ikiwa ni siku chache tangu kiwanda chake cha saruji kilichopo mkoani Mtwara kusimamisha uzalishaji kwa “sababu za kiufundi”, huku uongozi ukieleza kuwa kufanya biashara Tanzania ni gharama kubwa, kauli iliyoibua mjadala hasa kuhusu upatikanaji wa nishati inayotokana na makaa ya mawe na gesi asilia.
Hata hivyo, Waziri wa Nishati Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage walitoa ufafanuzi wakisema makaa ya mawe kutoka mgodi wa Ngaka mkoani Ruvuma yanatosha, bei yake ni nafuu kuliko makaa yanayoagizwa kutoka Afrika Kusini na ni bora.
Licha ya uongozi wa kiwanda hicho kusema wamesimamisha uzalishaji ili kurekebisha mitambo, baadhi ya wazabuni waliokuwa wakipeleka makaa ya mawe walisema si rahisi kupata shehena kubwa kwa wakati mmoja.
Taarifa zaidi zilisema mzozo ulianza kwenye upatikanaji wa gesi kabla ya kuhamia kwenye makaa ya mawe yanayodaiwa kutotosheleza mahitaji, hali iliyosababisha uongozi wa kiwanda hicho kuagiza makaa kutoka nje ya nchi na kwa sasa kutumia dizeli.
Kuja kwa Dangote kunaelezwa ni kutafuta suluhu ya mzozo huo.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais (Ikulu) jana ilisema Rais Magufuli amemhakikishia mfanyabiashara huyo kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote nchini katika kutimiza lengo lake la kuwa na Tanzania ya Viwanda.
“Rais Magufuli amesema kuhusu kiwanda cha kuzalisha Saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara hapakuwa na tatizo lolote ila kulikuwa na watu ambao walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya biashara za ujanja kitu ambacho Serikali yake haikiruhusu,” inasema taarifa hiyo.
Pia Rais Magufuli amemtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC) ambalo amesema ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.
‘’Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha, uwasiliane na viongozi wa Serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili,’’ alisema Rais Magufuli.
Dk Magufuli alisema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia kuhifadhia saruji kabla ya kuisafirisha, lakini wakajitokeza watu ambao wametaka kumuuzia kwa Sh43 bilioni kitu ambacho Rais amesema hakina uhalisia wowote bali ni watu ambao wanataka kutengeneza faida kitu ambacho hakiwezekani.
Taarifa hiyo ya Ikulu inasema Dangote alionyesha kushangazwa na baadhi ya vyombo vya habari kutangaza kuwa amefunga kiwanda kwa sababu amekatazwa kuagiza makaa ya mawe kutoka nje, kitu ambacho amesema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko kuagiza nje.
“Katika kuthibitisha hilo, tayari mfanyabiashara huyo ameingiza malori mapya 600 kwa ajili ya kusambazia saruji yake,” inasema taarifa hiyo ya Ikulu.
Magari 651 yatua Mtwara
Wakati Dangote akisema hayo jijini Dar es Salaam, mkoani Mtwara magari 651 yaliwasili jana kwa meli, kuwasili kwake kukiwa kumefanikishwa na kampuni ya usafirishaji ya Diamond Shipping Agency.
Meneja wa kampuni hiyo, John Limomo alisema meli ilishusha magari hayo jana akisema ni ya kampuni ya Dangote Tanzania Industries.
“Ameongeza kuwa lengo la kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida, ana lengo la kuisaidia Serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya kuagiza kutoka nje mali ghafi ambazo zinapatikana nchini.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Alhaji Dangote amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa ataendelea kufanya kazi na Serikali na kamwe hana nia yoyote ya kufunga kiwanda chake kama inavyodaiwa na baadhi ya vyombo vya habari, bali ana mpango wa kuangalia fursa nyingine zaidi za uwekezaji hapa nchini kutokana na uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Madalali kikwazo
Suala la kuwepo kwa watu wa kati wanaotia doa uwekezaji wa Dangote lilielezwa hivi karibuni na aliyekuwa wakala wa Dangote wakati wa kuingia makubaliano na Serikali, Esther Baruti.
Akizungumza hivi karibuni katika kipindi cha Power Breakfast cha kituo cha Clouds FM, Baruti alisema kilichosababisha kiwanda hicho kisitishe uzalishaji ni fitina za watu wenye masilahi katika upatikanaji wa gesi.
Hata hivyo alipotakiwa awataje alisema hawezi kwa sababu ya kuhofia usalama wake.
“Gesi ipo, lakini kuna watu wa kati wanaoingia kwenye mchakato wa kupata gesi ambao wana wanamchanganya Dangote. Lakini hivi vitu ni rahisi ambavyo akiongea na Serikali vitakwisha,” alisema Esther.
Mmoja wa wasafirishaji wa makaa ya mawe aliyepewa zabuni na kiwanda cha Dangote, Gabriel Munasa alisema japo makaa hayo yapo, lakini hupatikana kwa shida.
“Sisi wasafirishaji, expenditure (matumizi) tuliyokuwa tunatumia pale ni makubwa kiasi kwamba tunagombana na menejimeti ya Dangote. Tatizo pale makaa ya mawe hayapatikani kwa kiwango cha kutosha,” alisema Munasa.
Kiwanda hicho kimejengwa kwa gharama ya zaidi ya dola 500 milioni za Kimarekani na zaidi ya watu 10,000 walitarajiwa kupata ajira kutokana na uzalishaji wa kiwanda hicho.
Matukio makuu Afrika 2024
3 hours ago
Post a Comment